Na Shamimu Nyaki-WHUSM
Naibu Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Mhe.Anastazia James Wambura ametoa agizo kwa wasanii nchini kuhakikisha wanasajili kazi zao katika Baraza la Sanaa la Taifa (BASATA) ili watambulike kwa mujibu wa Sheria.
Agizo hilo amelitoa jana Jijini Dar es Salaam alipokuwa anazindua Tamasha la Siku ya Msanii Duniani lilioandaliwa na Baraza la Taifa la Sanaa (BASATA) ambapo amewaahidi wasanii kuwa wakijisajili watatambulika na itakuwa rahisi kwa Serikali kujua changamoto wanazozipata na kuzitatua kwa urahisi.
“Napenda mtambue kwamba suala la Urasimishaji linakwenda sambamba na uwepo wa Haki Miliki ya kazi za ubunifu, nawashauri mtunze Haki Miliki zenu na msiziuze na wale wabunifu wapya na ambao hamjasajili kazi zenu nawaomba mfanye hivyo ili kuepuka uharamia”.Alisisitiza Mhe. Anastazia.
Aidha Mhe.Naibu Waziri amewaomba wadau wote wa Sanaa kutoa maoni yao katika kuboresha tasnia hii yenye kubeba maeneo kama Muziki, Filamu, Maonyesho, Ususi, na Uchoraji ili kuwezesha tasnia hii kujulikana na kuboresha mapato ya Wasanii.
Kwa upande wake Katibu Mtendaji wa Baraza la Sanaa la Taifa (BASATA) Bw. Godfrey Muingereza amewataka Wasanii kutunza vibali wanavyopatiwa na Baraza hilo kwani ndio utambulisho wao popote wanapokuwa na inakuwa rahisi wao kusaidiwa wanapopata changamoto.
“Wengi wenu mmejisajili lakini wale wachache ambao bado naomba mfanye hivyo ili sisi tuwatambue na Sheria ya Haki Miliki pia iwatambue”.Aliongeza Bw.Muingereza.
Naye Msanii wa Uchongaji Bibi Hapiness Mmbaga amewashauri wanawake kupenda fani hiyo na kuacha dhana inayosema kuwa kazi hiyo ni kwa ajili ya wanaume tu kwani ulimwengu wa sasa umebadilika hakuna tena kuchagua aina ya kazi ya kufanya.
Tamasha la siku ya Msanii duniani linaadhimishwa kwa mara tatu mfululizo ambalo linalenga kuthamini mchango wa kazi za Sanaa hapa nchini ambao kauli mbiu yake ni “Nguvu ya Sanaa”na kilele chake itakuwa ni tarehe 26 mwezi oktoba mwaka huu.
Hakuna maoni :
Chapisha Maoni