WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa ametoa
wiki moja kwa Afisa Elimu Mkoa wa Pwani, Yussuph Kipengele kupeleka
walimu wa kufundisha masomo ya kidato cha tano na sita katika shule
za sekondari za Mkongo na Utete wilayani Rufiji.
Ametoa agizo hilo leo (Jumatatu,
Septemba 26, 2016) wakati akizungumza na wananchi katika mkutano wa
hadhara uliofanyika kwenye viwanja vya Jumba la Maendeleo wilayani
Rufiji.
Waziri Mkuu ametoa agizo hilo baada
ya Mbunge wa Rufiji, Muhammed Mchengelwa kumwambia kuwa wilaya hiyo
inakabiliwa na changamoto ya ukosefu wa walimu wa kidato cha tano na
sita licha ya kuwa na shule.
"Hatuwezi kuwa na shule ambazo
hazina walimu, nasikia hapa anayefundisha ni Mkuu wa shule na mwalimu
mmoja tu, wakati kule Kibaha kuna walimu walmerundikana ,sasa fanya
realocation tarehe 4,Oktoba uniletee taarifa walimu wamefika
Rufiji.",alisema Waziri Mkuu.
Akizungumzia suala la upungufu wa
watumishi wa umma kwenye sekta mbalimbali, Waziri Mkuu alisema baada
ya kazi ya uhakiki watumishi hewa itakapokamilika, serikali
itaangalia kwenye maeneo yenye upungufu na hivyo kutangaza ajira.
"Hivi sasa serikali
inakamilisha masuala ya uhakiki wa watumishi, tukimakamilisha na
kujua idadi ya watumishi na maeneo yenye upungufu tutaanza tena
kuajiri, tulisitisha kupisha kwanza kazi hii,alisema Waziri Majaliwa.
Kuhusu migogoro ya wakulima na
wafugaji Waziri, Mkuu alisema watendaji wa halmashauri na vijiji
wanapaswa kutenga maeneo ya wafugaji na wakulima na kutaka mifugo
isiongezwe kwenye maeneo ambayo hayajaruhusiwa.
Alisema wenyeviti wa vijiji
wanapaswa kusimamia utekelezaji wake katika mpango wa matumizi bora
ya ardhi na kwamba atakayeruhusu idadi kubwa ya mifugo kuingia
kijijini zaidi ya ile iliyokubalika atawajibishwa ikiwemo kufukuzwa
kazi na hatua nyingine za kisheria.
"Hatuwezi kuendelea kuwa na
watumishi wasio na nidhamu, wale wote watakaoingia mifugo zaidi ya
uwezo wa kijiji wafukuzwe kazi na kuchukuliwa hatua, lakini pia
wafugaji ni marufuko kuingiza mifugo kwenye mazao ya wakulima"alisema
Waziri Mkuu.
Kuhusu ujenzi wa barabara ya lami
kwenda makao makuu ya wilaya ya Rufiji, Utete, Waziri Mkuu aliahidi
kuchukua ombi hilo na kusema bajeti ijayo litatengewa fedha kuwa
ajili ya kufanya maandalizi ya upembuzi kuona gharama yake kabla ya
kutangaza zabuni ya ujenzi.
Kuhusu utengenezaji wa madawati,
Waziri Mkuu alisema ifikapo Oktoba 30, mwaka huu kila wilaya nchini
inapaswa iwe imekamilisha utengenezaji wa madawati hayo kwenye shule
nchini.
Aidha, alisema ipo miradi mingi
inayoendeshwa kwa maslahi binafsi ukiwemo mradi wa Bonde la
Rufiji(RUBADA), ambao wamebaini kuna ubabaishaji mkubwa, hivyo
wamepeleka timu ya wataalamu kuhakiki ili wale wabadhirifu
wachukuliwe hatua.
(mwisho)
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
JUMATATU, SEPTEMBA 26, 2016
Hakuna maoni :
Chapisha Maoni