WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amezindua miongozo ya Mfumo wa Anwani za Makazi na Postikodi na kuziagiza taasisi za umma na binafsi zianze kutumia mfumo huo ili kuchochea kasi ya maendeleo nchini.
“Nawaagiza na BRELA (Wakala wa Usajili wa Leseni na Biashara) kuhakikisha wanajumuisha anauani za makazi kwa waombaji wa leseni za biashara ili kurahisisha utambuzi na uhakiki,” amesema.
Waziri Mkuu ametoa agizo hilo leo (Jumatano, 14 Septemba, 2016), wakati akizindua miongozo ya Mfumo wa Anwani za Makazi na Postikodi kwenye ukumbi wa Msekwa, Bungeni mjini Dodoma.
Amesema mfumo huo lazima uweke msukumo mpya wa kimkakati ili kuhakikisha uwekaji wa miundombinu ya Anwani za Makazi na Postikodi unatekelezwa ipasavyo na unachangia maendeleo ya mtu mmoja mmoja na Taifa kwa ujumla.
Amesema mfumo huo unatakiwa ukamilike nchi nzima kabla ama ifikapo Juni, 2018 ila kasi ya utekelezaji wake inakwamishwa na changamoto mbalimbali ikiwemo uhaba wa fedha na barabara au mitaa mingi kutokuwa na majina.
“Hivyo, naelekeza kila mdau atimize wajibu wake katika utekelezaji na matumizi ya Mfumo wa Anwani za Makazi na Postikodi kulingana na maelekezo yaliyo kwenye miongozo hii,” amesisitiza.
Waziri Mkuu amesema Serikali ya awamu ya tano inapenda watendaji wake kuwa wabunifu, hivyo changamoto hizo zitatuliwe haraka na Ofisi ya Rais, TAMISEMI.
Pia ameziagiza Halmashauri zote nchini kuzitafutia ufumbuzi changamoto ambazo hazihitaji fedha ama gharama kubwa kama kuhakikisha barabara na mitaa yote inakuwa na majina yaliyorasimishwa na kudhibiti mipango miji dhaifu na ujenzi holela.
Amesema Halmashauri zinatakiwa kuwa na takwimu za idadi ya barabara na mitaa na nyumba katika kila kata na kuwa na taarifa za wakazi wa kila kata, kujenga uelewa na uwezo wa mfumo kwa wadau na wananchi na kuimarisha matumizi ya daftari la wakazi.
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
S. L. P. 980,
DODOMA.
JUMATANO, SEPTEMBA 14, 2016
Jisajili kwenye:
Chapisha Maoni
(
Atom
)
Hakuna maoni :
Chapisha Maoni