Naibu Waziri, Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia Sera, Uratibu, Bunge na Vijana, Dk. Abdallah Possi amesema kwamba Serikali itaendelea kusapoti michezo kwa sababu ya umuhimu wake, lakini akataka kutafutwa mbinu za kuhakikisha wadhamini wanasapoti timu za taifa na klabu mbalimbali zinazoshiriki ligi zinazosimamiwa na Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF).
Dk. Possi aliyekuwa mgeni rasmi katika hafla ya kuwapongeza vijana wa Timu ya Taifa ya Tanzania wenye umri wa chini ya miaka 17 ‘Serengeti Boys’, alisema kwamba fursa ipo ya kufanya vema katika michezo na ndiyo maana Serikali inasapoti michezo kwa sababu ya kuleta faraja, kuunganisha au kuleta umoja katika nchi yoyote kadhalika ni ajira.
Dk. Possi aliyesifu juhudi za TFF na timu hiyo, aliwapoza vijana hao akiwaeleza kuwa “Juhudi zilifanyika na mnaona kiwango kilichotumika kuandaa timu yenu. Matokeo mliyopata ndiyo mchezo. Kushindwa haina maana tumeishia hapa,” alisema Dk. Possi alipokuwa akiwapongeza vijana hao katika hafla hiyo iliyofanyika Uwanja wa Karume, Dar es Salaam.
Ili kuepuka gharama kubwa za kuendesha timu hizo ambako Serengeti Boys imetumika karibu bilioni moja, Dk. Possi amesema kwamba kunahitajika kutengenezwa mfumo wa kupata wadhamini ili baadaye bidhaa za TFF zigombaniwe na hata kampuni zinazofanya biashara inayofanana zinaweza kuingia kudhamini katika ligi moja au klabu kwa sababu zitavuna maslahi.
Akiwageukia wachezaji, Dk. Possi alisema wachezaji hawana budi kuwa na nidhamu ya hali ya juu si katika kuonyesha kusabahi tu, bali kutunza mwili. “Mtafika mbali kama mkiwa na nidhamu ndani na nje ya uwanja. Mna walimu, mna viongozi, ni vema mkawa mnawasikiliza wengine,” alisema Dk. Possi huku akitaja majina ya nyota waliofanikiwa kwa kuwa na nidhamu na wengine ambao walioanguka kwa kuwa na nidhamu mbovu.
Kabla ya kumkaribisha Dk. Possi, Rais wa TFF Jamal Malinzi alianza na kutoa taarifa ya matokeo huko Congo Brazzaville, akisema: “Ilikuwa siku mbaya sana kwangu. Watoto walikwenda kufia nchi. Lakini jahazi halijafika mwisho, kuvunjika kwa mpini, sio mwisho wa uhunzi. Userengeti Boys unakwisha na sasa unakuja Ungorongoro Heroes timu ya taifa ya vijana wenye umri wa chini ya miaka 20.”
Malinzi aliyetumia nafasi hiyo kumpa nafasi tena Kocha Mkuu wa vijana hao, Bakari Nyundo Shime alisema kikosi hicho kinapambana kucheza fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika za mwaka 2019 na ili kujindaa timu hiyo inatarajiwa kwenda Korea Kusini kwenye mashindano maalumu itawasaidia kuongeza uwezo wenu, kutembea na kutafuta soko la kimataifa la soka.
Alisema kwamba mara baada ya timu hiyo kurejea, itakuwa inakusanhyika kila baada ya miezi mitatu ili kufanya mazoezi ya pamoja na kupata mchezo angalau mmoja wa kirafiki huku akitangaza kuwa vijana wa Mwanza, wanaosoma katika shule ya Alliance wanatarajiwa kuunda kikosi kipya cha timu ya vijana wenye umri wa chini ya miaka 17.
“Timu ile ya Mwanza ambayo kwa sasa ina vijana wa chini ya miaka 15, ndio watakaounda kikosi cha fainali za vijana ambazo zitafanyika hapa nchini mwaka 2018. Desemba watoto wale watacheza mechi ya kwanza ya kimataifa kwenye Uwanja wa Taifa, ambako watapigiwa wimbo wa taifa,” alisema Malinzi na kuongeza kuwa vijana walioibuliwa kutoka michuano ya Airtel Rising Stars nao watajumuishwa.
“Ligi ya wanawake inayokuja. Ndiyo nayo itazaa timu bora ya wanawake ambayoi itashiriki fainali za Kombe la Dunia hapo mwaka 2019. Ili tuweze kufanya yote haya, tunahitaji fedha na tayari tumeanzisha mfuko maalumu wa kuchangia timu hizi unaitwa TFF Fund ambao utakuwa na mtendaji wake na ofisi yake,” alisema na kuongeza, “Yote haya yanalenga Tanzania kucheza fainali za Kombe la Dunia za mwaka 2016.”
Timu hiyo iliyofanyiwa hafla, ilikuwa ikipambana kucheza fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika, lakini ikaondolewa na Congo Brazzaville kwa kufungwa bao 1-0 dakika za majeruhi hivyo kuondolewa kwa sheria za bao la ugenini. Mchezo wa kwanza Tanzania ilishinda 3-2 na katika mchezo wa marudiano, ilipoteza.
Kamati ya Bodi ya Ligi ya Uendeshaji na Usimamizi wa Ligi imeipiga faini ya sh. 5,000,000 (milioni tano) klabu ya Simba, kuiagiza ilipe gharama za uharibifu wa viti uliofanywa na washabiki wake katika mechi ya Ligi Kuu ya Vodacom kati ya timu yake na Yanga iliyochezwa Oktoba Mosi mwaka huu Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Pia Kamati hiyo katika kikao chake kilichofanyika jana (Oktoba 4, 2016), imelaani kitendo hicho na kuionya klabu hiyo kuwa vitendo vya aina hiyo vikiendelea itakabiliwa na adhabu kali zaidi ikiwemo kucheza mechi bila washabiki. Adhabu dhidi ya Simba imetolewa kwa mujibu wa Kanuni ya 42(3) na 24(7) za Ligi Kuu.
Kwa taarifa zaidi, fuata link hapo chini
Hakuna maoni :
Chapisha Maoni