Waziri wa Fedha na Mipango Dkt. Philip Mpango akiwa na Katibu Mkuu Bw. Dotto James (kulia) wakiandika pointi muhimu wakati Rais wa Benki ya Dunia, Dkt. Jim Yong Kim, alipowahutubia Mawaziri wa Fedha na Makatibu wakuu (Magavana) kutoka nchi za Kiafrika wanaoshiriki Mkutano wa Mwaka wa Benki ya Dunia na Shirika la Fedha Duniani-IMF, Jijini Washington DC-Marekani.
Benny Mwaipaja, MoFP Washington DC, Marekani 10.10.2016
MAWAZIRI wa Fedha na Magavana wa Benki Kuu kutoka nchi mbalimbali za kiafrika, wanachama wa Benki ya Dunia na Shirika la Fedha la Kimataifa-IMF, wamekutana Jijini Washington DC, Marekan,i na kuzitaka Taasisi hizo kuweka mipango inayoakisi na kutatua changamoto zinazolikabili bara hilo ikiwemo, uhalifu, umasikini, mizozo ya kivita na majanga yanayotokana na mabadiliko ya tabia nchi
Aidha, Viongozi hao wamezitaka taasisi hizo kuweka uwiano wa uwakilishi wa uongozi wa juu ili kuhakikisha kuwa maslahi mapana ya nchi hizo yanalindwa na maendeleo endelevu yanafikiwa kwa haraka.
Akizungumza kwenye moja ya mikutano hiyo, Waziri wa Fedha na Mipango, Dkt. Philip Mpango, ambaye kiutaratibu ni mmoja wa Magavana wa Benki ya Dunia na IMF, amesema kuwa mashirika hayo ya fedha ya kimataifa yanamchango mkubwa kwa maendeleo ya nchi za kiafrika ikiwemo Tanzania.
Hata hivyo amesema kuwa mdororo wa uchumi duniani, ambao unaonesha kuwa viwango vya ukuaji wa uchumi vilivyokadiriwa kufikiwa kwa asilimia 3, havitafikiwa ambapo takwimu zinaonesha kuwa ukuaji wake hivi sasa ni asilimia 1.5 tu, unaashiria namna nchi wanachama zinatakiwa kujipanga kuhakikisha kuwa uchumi unapanda.
Dkt. Mpango amesema kuwa uchumi wa Tanzania unakua kwa kasi kwa wastani wa asilimia 7 kwa mwaka lakini changamoto kubwa iliyopo ni kuhakikisha kuwa uchumi huo unaonekana katika maisha ya kawaida ya wananchi wake
“Kila mara utasikia malalamiko ya wananchi kwamba uchumi wetu unakua kwa namba tu hawaoni ni kwa kiasi gani uchumi huo wanauona katika maisha yao ya kawaida kwa hiyo ili uchumi uhesabike kuwa unakua ni lazima uwe jumuishi na ushirikishe watu wengi” alisema Dkt. Mpango
Amesema kuwa hali hiyo itawezekana ikiwa sekta zinazochangia maendeleo kwa kasi zaidi kama kilimo, uvuvi, biashara ya miamala ya simu, miundombinu na viwanda, zitaimarishwa ili kukuza ajira na kuongeza kipato cha wananchi.
“Tunataka kilimo kiwe cha kisasa na cha kibiashara kwa kutumia zana na pembejeo bora za kilimo, uongezaji wa thamani ya mazao na kuwa na masoko ya uhakika ili kukuza ajira nyingi hususani kwa vijana” Aliongeza Dkt. Mpango
Amebainisha kuwa Tanzania itaendeleza uhusiano mzuri uliopo kati yake na Benki ya Dunia na Shirika la Fedha Duniani-IMF na kuwataka watanzania waelewe kuwa mikopo na ruzuku zinazotafutwa na serikali yao ni kwaajili ya kuwaletea maendeleo kwa kuwekeza kwenye miradi yenye tija.
Hakuna maoni :
Chapisha Maoni