.

.

.

.

.

.

.

.
KARIBUNI TUHABARIKE, TUELIMISHANE, TUPEANE HABARI ZA KUKUFANYA UTABASAMU KIDOGO NA MATUKIO YALIYOFANYIWA UCHUNGUZI WA KINA TOKA KILA PEMBE CONTACTS: +255 787 377 722 Email: drweyunga@gmail.com PIA UNAWEZA KUNI FOLLOW KUPITIA INSTAGRAM YANGU @drweyunga | TANGAZA NASI ILI UWAFIKIE WATU WENGI ZAIDI.

Jumatano, 12 Oktoba 2016

MJI WA DODOMA LAZIMA UPANGWE – WAZIRI MKUU

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema mji wa Dodoma ni lazima upangwe ili uwe tofauti na miji mingine hapa nchini.

Waziri Mkuu ametoa kauli hiyo leo mchana (Jumatano, Oktoba 12, 2016) wakati akizungumza na Mkurugenzi Mtendaji wa kampuni hiyo, Bw. Abeid Abdallah ambaye alifika ofisini kwake Magogoni, jijini Dar es Salaam na kuelezea nia yake ya kutaka kuwekeza mjini Dodoma.

Amesema Serikali haitaki kurudia makosa yaliyofanyika kwenye miji mingine. 

“Katika kuupanga ule mji, ni lazima mji upangwe kama ambavyo miji mingine mikuu inapangwa. Kila eneo kutakuwa na nyumba za aina fulani. Hatuwezi kuachia watu wajenge popote na wanavyotaka, mji unakuwa haupangiki. Na hilo ndilo kosa lililofanyika kwenye miji mingine mikubwa ambayo tunayo kwa sasa.”
Amesema Kamati ya Kitaifa ya Maandalizi ya kuhamia Dodoma imepewa jukumu la kupitia upya Master Plan ya mji wa Dodoma na kuainisha maeneo ambako nyumba za aina mbalimbali zitajengwa.

“Kimsingi tunataka tuanze kujenga miji iliyopangiliwa na Dodoma tunataka uwe wa mji kwanza kuujenga vizuri kwa standard ya sasa. Kutakuwa na nyumba za ghorofa katika maeneo fulani, na nyumba za kawaida katika maeneo fulani. Mkurugenzi wa CDA amekwishaandaa ramani rasmi,” amesema.

Akizungumzia kuhusu ujenzi kwenye maeneo ambayo tayari wananchi wanaishi, Waziri Mkuu amesema Serikali itaweka utaratibu ili kuwe na mikataba baina ya mwekezaji na mwananchi anayemiliki eneo husika ili asinyimwe haki ya kumiliki eneo lake.

“Kama tutahitaji eneo ambalo tayari lina makazi, taratibu zetu ni zilezile kwamba tutaweka mikataba kati ya mwekezaji na mwananchi. Kama anataka kujenga kwenye eneo lile, basi lazima amhusishe mwenye eneo na kama anataka kujenga ghorofa ni lazima ahakikishe mwenye eneo anapata umiliki kama tulivyofanya kule Magomeni,” amesisitiza.

Kwa upande wake, Mkurugenzi huyo, Bw. Abdalla amemweleza Waziri Mkuu kwamba wako tayari kushirikiana na Serikali katika zoezi la Serikali kuhamia Dodoma kwa lengo wa kuwasaidia wananchi wa kipato cha chini kupata makazi bora na ya kudumu.

IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
2 MTAA WA MAGOGONI,
S. L. P. 3021,
11410 - DAR ES SALAAM.
JUMATANO, OKTOBA 12, 2016.

Hakuna maoni :

Chapisha Maoni