.

.

.

.

.

.

.

.
KARIBUNI TUHABARIKE, TUELIMISHANE, TUPEANE HABARI ZA KUKUFANYA UTABASAMU KIDOGO NA MATUKIO YALIYOFANYIWA UCHUNGUZI WA KINA TOKA KILA PEMBE CONTACTS: +255 787 377 722 Email: drweyunga@gmail.com PIA UNAWEZA KUNI FOLLOW KUPITIA INSTAGRAM YANGU @drweyunga | TANGAZA NASI ILI UWAFIKIE WATU WENGI ZAIDI.

Jumanne, 25 Oktoba 2016

SERIKALI KUZIBA PENGO LA WAHADHIRI WAANDAMIZI NCHINI

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema Serikali itaendelea kutafuta fedha
za mafunzo kwa ajili ya wahadhiri wa vyuo vikuu nchini ili kuziba pengo la wahadhiri waandamizi lililopo hivi sasa lakini pia amevitaka vyuo hivyo viweke utaratibu wa kuachiana nafasi ama kurithishana kazi (succession plan).

Amesema yeye binafsi anatambua upungufu uliopo umesababishwa na masharti ya ajira za mkataba kwa wahadhiri waandamizi kuwa miaka 65 na
maprofesa kuwa miaka 70.

Ametoa kauli hiyo leo (Jumanne, Oktoba 25, 2016) wakati akifunga kilele cha maadhimisho ya miaka 55 ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam yaliyoanza jana kwenye ukumbi wa Nkrumah. Kampasi ya Mwalimu J. K. Nyerere, jijini Dar es Salaam.

“Ninatambua kuwa katika vyuo vya umma kuna upungufu mkubwa wa wahadhiri waandamizi na maprofesa na hivyo kuathiri hali ya utoaji wa
taaluma kwa fani za ‘Post-Graduates’. Ninajua kuwa pamoja na sababu
nyingine, hali hii inachangiwa pia na masharti ya ajira za mikataba kwa wahadhiri waandamizi kuwa miaka 65 na maprofesa kuwa miaka 70.
 

Serikali itaendelea kuweka kipaumbele cha upatikanaji wa fedha za kutosha kwa ajili ya mafunzo,” amesema.

“Lakini vyuo vya elimu navyo havina budi kuweka taratibu na mipango endelevu ya kurithishana (kuachiana nafasi) ‘Succession Plan’. Jambo
hii ni muhimu sana kwani bila hivyo, wakati wote kutakuwa na pengo
kubwa katika utoaji wa taaluma,” amesisitiza.

Amesema Serikali itatoa ushirikiano wa kutosha katika utekelezaji wa
mipango hii ya kuwa na watalaamu wa kutosha katika vyuo huku ikiendelea kutekeleza majukumu ya kuwaajiri wanataaluma na wafanyakazi wapya pale wanapohitajika.

Akizungumzia kuhusu maslahi ya watumishi wa vyuo hivyo, kikiwemo Chuo
Kikuu cha Dar es Salaam, Waziri Mkuu amesema Serikali ya awamu ya tano
imedhamiria kuhakikisha inaondoa malimbikizo ya madai kwa watumishi
wote wa umma na hivi sasa inakamilisha uhakiki wa taarifa za kiutumishi kwa watumishi wa umma ili kubaini watumishi hewa.

“Hadi kufikia tarehe 20 Oktoba, 2016 zoezi linaloendelea hivi sasa, limesaidia kuwabaini watumishi wa umma hewa wapatao 16,500. Baada ya zoezi hilo, tutarudia uhakiki wa madeni yote yaliyowasilishwa Serikalini na kisha tutalipa madeni ya watumishi wote,” amesema.

“Ninafahamu kuwa yapo madai mbalimbali ikiwemo malimbikizo ya mishahara kwa watumishi hususan baada ya kuanza kwa muundo wa pamoja
wa wanataaluma wa vyuo vikuu vya umma. Serikali inaendelea na
maboresho na kuimarisha maslahi kwa watumishi wote wa umma kupitia
bodi ya mishahara na motisha; na mara tutakapokamilisha, tutapanga
upya mishahara na motisha kwa watumishi,” amesema.

Akifafanua kuhusu mikopo ya wanafunzi wa elimu ya juu, Waziri Mkuu
amesema Serikali inaendelea kufanya uhakiki wa taarifa za waombaji wa
mikopo. Ametoa wito kwa wanufaika na waombaji wote wa mikopo wahakikishe kuwa wanatoa taarifa zilizo sahihi na za uhakika.

Hata hivyo, Waziri Mkuu amesema Serikali ilikwishaongeza bajeti ya
mikopo ya elimu ya juu kutoka sh. bilioni 340 mwaka 2015/2016 hadi sh.
bilioni 483 kwa mwaka 2016/2017.

Mapema, akielezea utendaji kazi wa chuo hicho katika miaka yote 55, Makamu Mkuu wa Chuo hicho, Prof. Rwekaza Mukandala amesema chuo hicho kinakabliwa na changamoto ya uhaba wa wanataaluma waandamizi wa fani
mbalimbali.

“Chimbuko la changamoto hii ni kusitishwa kwa ajira katika taasisi za umma kwenye miaka ya 1990. Kutoajiriwa kwa wanataaluma chipukizi kwa miaka mingi, kulivuruga utaratibu wa miaka mingi wa kurithishana uzoefu baina ya wanataaluma wanaostaafu na wale ambao wangelichukua
nafasi zao,” amesema.

“Hali hii iko kwenye vyuo vikongwe ambako mamia ya wanataaluma wazoefu
wanastaafu kwa wakati mmoja na wengi wa wanataaluma walioajiriwa hivi
karibuni bado wako masomoni au wangali chipukizi katika taaluma zao na
hivyo hawana uwezo wa kutosha kubeba majukumu ya kufundisha katika
ngazi za digrii za umahiri na uzamivu,” amesema.

Hata hivyo, ameishukuru Serikali kwa kutoa fedha za kuwadhamini wahadhiri chipukizi ambao wako sehemu mbalimbali wakipata mafunzo. Pia amemshukuru Rais Dkt. John Pombe Magufuli kwa uamuzi wake wa kujenga
hosteli yenye uwezo wa kuchukua wanafunzi zaidi ya 3,800 na hivyo kutarajiwa kupunguza tatizo la malazi.

Wakati huohuo, Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Dkt. Leonard Akwilapo alisema wizara hiyo imetenga kiasi
cha sh. bilioni 9 kwa ajili ya kufanya ukarabati wa miundombinu kwenye
chuo hicho zikiwemo maabara.

IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
2 MTAA WA MAGOGONI,
S. L. P. 3021,
11410 - DAR ES SALAAM
JUMANNE, OKTOBA 25, 2016.

Hakuna maoni :

Chapisha Maoni