(Picha na Zainul Mzige wa Modewjiblog)
WAKATI Umoja wa Mataifa (UN) ukiadhimisha miaka 71 tangu kuanzishwa kwake, imeahidi kuwatumia vijana katika utekelezaji wa malengo yake 17 ya maendeleo.
Mwakilishi Mkazi wa UN nchini, Alvaro Rodriguez amesema ili kufanikisha hilo, UN pamoja na mashirika mengine itatoa mafunzo ya vitendo kwa vijana zaidi ya 50,000 ifikapo mwaka 2017 ambao wataingizwa katika mpango wa utekelezaji wa malengo hayo.
“UN itaendelea kushirikiana na vijana pia itatoa elimu ya vitendo.Hadi sasa vijana zaidi ya elfu kumi wamepewa mafunzo na wanatambua malengo hayo, na kwamba UN na wadau wengine wanatarajia kufundisha vijana zaidi ya 50, 000 ifikapo mwaka 2017, ili ifikapo 2030 vijana wengi wawe wanajua malengo hayo na namna ya kuyatekeleza,” amesema.
Amesema miongoni mwa mafunzo yatakayotolewa kwa vijana hao ni pamoja na jinsi ya kufanikisha malengo 17 ya maendeleo endelevu ya umoja huo na jinsi ya vijana watakavyoweza kujiajiri.
Aidha, Rodriguez amesema tatizo la ukosefu wa ajira kwa vijana linasababisha umasikini kwa kuwa nguvu kazi hiyo inashindwa kuwajibika katika kuliletea taifa maendeleo.
“Ongezeko la vijana na mahitaji yao ni moja ya changamoto kubwa nchiniTanzania, tunahitaji kuhakikisha kwamba vijana wanawajibika katika kujiendeleza ili kupata maendeleo chanya katika maisha yao, ili kufanikisha hayo vijana wanatakiwa kuwa na ufahamu na taaluma katika kuwezesha mabadiliko ya uchumi nchini Tanzania,” alisema Rodriguez na kuongeza:
“Vijana wasisahau kuwa wao ni chachu ya amani na maendeleo na UN tutaendelea kushirikiana nao kuhakikisha vijana wanakuwa wadau wa taratibu na kanuni zilizosababisha kuundwa umoja huu, wakijua na kutambua malengo ya dunia,” amesema.
Rodriguez amesema UN itaendelea kushirikiana na serikali ya Tanzania katika kuleta maendeleo nchini.
“UN itashirikiana na serikali ya Tanzania kuleta maendeleo ikiwemo kuboresha utoaji wa huduma za kijamii,” amesema.
Kwa upande wa mgeni rasmi Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Augustine Mahiga amesema serikali inatambua mchango wa umoja huo katika kuleta maendeleo nchini na kwamba itaendelea kushirikiana na umoja huo.
“Serikali ya awamu ya tano tangu kuanza kwake imefanya mambo mengi ili kuleta maendeleo, imedhibiti mianya ya ukwepaji kodi, imefanikiwa kutanua wigo wa ukusanyaji mapato na kuondoa rushwa. Hatuwezi kushinda pekee katika kuleta maendeleo ya wananchi, serikali iko tayari kushirikiana na jumuiya zote duniani,” amesema.
Hakuna maoni :
Chapisha Maoni