WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa ameuagiza uongozi wa mkoa wa Lindi kuhakikisha wanawakamata na kuwachukulia hatua watu wote wanaoharibu mazingira kwa kufyeka na kuchoma moto misitu kwa sababu wanaharibu mazingira na kusababisha ukame.
Amesema mkoa huo upo hatarini kugeuka jangwa na tayari vyanzo vingi vya maji vimeanza kukauka kwa sababu ya uharibifu wa mazingira unaotokana na watu kufanya shughuli za kijamii kwenye vyanzo vya maji.
Waziri Mkuu ametoa agizo hilo leo (Jumanne, Oktoba 18, 2016) wakati akizungumza kwa nyakati tofauti na wananchi wa wilaya ya Ruangwa katika mikutano iliyofanyika kwenye vijiji vya Nanjaru, Nachinyimba, Nambiranje, Mkaranga, Nandenje, Nachinyimba na Mandarawe.
Amesema wakulima wa ufuta wanatakiwa kuendelea kutumia mashamba yao ya zamani na kuacha tabia ya kufyeka misitu kila mwaka na badala yake waanzishe mpango wa upandaji miti ili kuepusha taifa kugeuka kuwa jangwa.
“Vyanzo vya maji vimekauka kwa sababu tumekata miti mingi. Mito yote iliyokuwa inatiririsha maji imekauka. Viongozi wa mkoa hakikisheni misitu inalindwa na atakayekutwa analima kwenye vyanzo vya maji akamatwe,” amesema.
Waziri mkuu aliongeza kuwa “Ukataji miti huu unaoendelea katika maeneo yetu hakutosababisha kukosekana kwa maji tu, bali hata mazao yatapungua. Jambo hili itasababisha njaa katika vijiji vyetu, hivyo tuache kukata miti.
Waziri Mkuu amesema kwa sasa Serikari inatumia gharama kubwa kuchimba visima virefu kutafuta maji. Amesema zamani walikuwa wanachimba mita 20 au 30 wanakuta maji na gharama yake ilikuwa sh. milioni 35, ambako kwa sasa wanalazimika kuchimba mita zaidi ya 150 kwa gharama y ash milioni 75 kwa kisima kimoja.
Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Lindi, Bw. Godfrey Zambi,amewataka watendaji wa kata na vijiji kuimalisha ulinzi wa maeneo ya misitu na maji, na atakayeshindwa atachukuliwa hatua kali za kisheria.
“Hatuko tayari kutengeneza jangwa hivyo tutapamba na wale wote wenye tabia za kuchoma moto misitu au kulima kwenye vyanzo vya maji,” amesema.
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
JUMNNE, OKTOBA 18, 2016
Hakuna maoni :
Chapisha Maoni