Na Lulu Mussa TABORA
Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais anayeshughulikia masuala ya Muungano na Mazingira Mhe. Jauary Makamba amempongeza Bw. Leordard Kushoka kwa kubuni kiwanda kinachotengeza nishati mbadala rafiki kwa mazingira.
Akiwa Mkoani Tabora, Waziri Makamba alipata fursa ya kutembelea kiwanda hicho na kusema kuwa Serikali inathamini sana ubunifu na uvumbuzi hasa unao okoa mazingira. “Bwana Kushoka mimi nakupongeza sana, niliona jitihada zako kupitia kipindi cha televisheni na kuamua kukuita na kukusaidia” alisisitiza Waziri Makamba.
Katika kuthamini mchango wa Kiwanda hicho cha “Kuja na Kushoka” Ofisi ya Makamu wa Rais imemsaidia Bw. Kushoka kupata haki miliki ya Kiwanda hicho.
Awali Bw. Leonard Kushoka, Mkurugenzi wa Kuja na Kushoka Tools Manufacture Group amesema kuwa kiwanda chake kimefanikiwa kutoa ajira kwa vijana 13 na kufanikiwa kubuni teknolojia mbalimbali rafiki kwa mazingira ambapo mpaka sasa wamefanikiwa kuwafikia vijana zaidi ya 50 katika Wilaya za Tabora Manispaa, Urambo, Kaliua, Mlele pia Katavi na kufanikiwa kuwafundisha utengenezaji wa Majiko banifu yanayopunguza matumizi ya kuni na mkaa kwa asilimia 50.
Pia Kiwanda hicho kimefanikiwa kubuni mashine ambayo ina uwezo mkubwa wa kuzalisha kilo 160 kwa saa kwa kutumia dizeli lita 5 na kuzalisha wastani wa Kilo 1000 za mkaa mbadala na pia Kiwanda hicho kimefanikiwa kubuni mtambo kwa kukaushia tumbaku kwa kutumia taka kavu au mabaki yote ya mazao kama maganda ya karanga, randa za mbao, magunzi ya mahindi na masuke ya mpunga.
Bw. Kushoka amesema kuwa “Mtambo huu umetoa matokeo mazuri katika ukaushaji wa tumbaku kwani wastani wa matumizi ya taka kilo 3 hukausha kilo moja ya tumbaku kwa kutumia mabani ya kisasa”
Bw. Kushoka amemuomba Waziri kuisaidia Kampuni hiyo kupata mafunzo mbalimbali ya namna bora zaidi ya kubuni na kuendeleza uzalishaji wa nishati mbadala hasa katika nchi zinazofanya vizuri zaidi.
‘Kuja na Kushoka” ilianzishwa rasmi mwaka 2000 na kupata usajili mwaka 2013 na kupewa hati (TMC/CO/CBO/48).
Waziri Makamba akiwa katika Mkoa wa Tabora pia amepata fursa ya kutembelea Wilaya ya Nzega na Igunga, akihitimisha ziara yake ya Mikoa 10 hapa nchini yenye changamoto za kimazingira.
Hakuna maoni :
Chapisha Maoni