WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa
amemsimamisha kazi Mkurugenzi wa Mamlaka ya Maji Lindi (LUWASA),
Mhandisi Adam Alexander kwa kosa la matumizi mabaya ya ofisi pamoja
na kushindwa kusimamia ujenzi wa kituo cha kuzalisha maji katika
Manispaa ya Lindi.
Waziri Mkuu amemkabidhi Mhandisi
huyo kwa Kamanda wa TAKUKURU Mkoa wa Lindi, Bw. Stephen Chami na
kumuelekeza afanye uchunguzi zaidi juu ya suala hilo.
Waziri Mkuu ametoa agizo hilo leo
(Jumatano, Oktoba 19, 2016) wakati alipotembelea mradi wa maji wa
Ng'apa ambapo ameagiza nafasi hiyo ikaimiwe na Mkurugenzi Msaidizi wa
mamlaka hiyo, Mhandisi Idrisa Sengulo.
"Kamanda wa TAKUKURU fanya
mapitio ya kina ya mshahara wake. Yeye anasema analipwa Wizarani,
mimi najua analipwa na LUWASA. Angalia kazi aliyokwenda kuifanya Dar
es Salaam kama inalingana na siku alizokaa,” amesisitiza Waziri
Mkuu.
Mhandisi hiyo anakabiliwa na tuhuma
mbalimbali ikiwemo matumizi mabaya ya fedha za ofisi pamoja na
kupokea mshahara bila la kulipa kodi ya mapato ya mshahara (PAYE),
kujilipa kiwango kikubwa cha posho pamoja na kusafiri kwa muda mrefu.
Waziri Mkuu amesema Serikali haiwezi
kuvumilia kuona wananchi wanapata shida huku watendaji waliopewa
dhamana ya kuwatumikia hawaonekani kwenye vituo vyao vya kazi. "Huyu
nimemuita mimi aje huku, hadi jana alikuwa Dar es Salaam."
Alipoulizwa sababu za kutokuwepo
ofisini kwake kwa muda mrefu, Mkurugenzi huyo alisema kwamba alikuwa
Dar es Salaam akiandika maombi ya fedha kwa ajili ya kutatulia
changamoto mbalimbali zinazoikabili mamlaka hiyo.
"Unatumia siku ngapi kuandika
proposal, msomi unatumia mwezi mzima kuandika proposal na unakaa Dar
es Salaam hata Katibu Mkuu wako hajui na huko unajilipa posho tu!
Tena baada ya kulipwa sh.120,000 kwa siku wewe unajilipa sh.150,000.
Hatuwezi kuvumilia hali hii,” amesema.
Waziri Mkuu amemaliza ziara yake
siku tatu mkoani Lindi na amerejea jijini Dar es Salaam.
(mwisho)
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
2 MTAA WA MAGOGONI,
S. L. P. 3021,
11410 - DAR ES SALAAM
JUMATANO, OKTOBA 19, 2016.
Hakuna maoni :
Chapisha Maoni