WAZIRI wa Fedha na Mipango, Philip Mpango ameipongeza Benki ya NMB kwa kuwajali wajasiliamali wadogo na wakati. Waziri Mpango ametoa kauli hiyo leo jijini Dar es Salaam alipokuwa akizinduwa maonesho ya mabenki na taasisi za kifedha katika ukumbi wa Mlimani City.
Alisema Serikali inatambua mahitaji makubwa ya kufanya maboresho na kuziwezesha benki na taasisi nyingine za kifedha kuweza kufikia watu wengi kwa maana ya mitaji ya kutosha ya kuongeza uwekezaji wa ndani, ikiwa ni pamoja na kuweka msukumo zaidi kujenga mazingira rafiki kwa wadau wa sekta hiyo iweze kupanua huduma nchini.
Serikali inatambua changamoto anuai zinazowakabili wajasiliamali hasa wadogo na wakati hapa nchini ikiwemo kushindwa kupata mikopo kwa urahisi jambo ambalo linakwamisha mipango waliojiwekea. Aliziomba taasisi za fedha yakiwemo mabenki kubuni programu na madirisha maalumu ya kuwasaidia wajasiliamali wadogo na wakati wanaofanya jitiata kubwa kuwekeza katika viwanda vidogo.
"Napenda kuipongeza benki ya NMB kwa kuwajali wajasiliamali wadogo na wakati na hata kuamua kudhamini maonesho ya mabenki na taasisi za kifedha ili kuwakutanisha wafanyabiashara kujadili changamoto mbalimbali zinazowakabili. Mkusanyiko huo utachangia kuona fursa za mitaji zinazopatikana NMB pamoja na taasisi nyingine za kifedha na kuzichangamkia kwa maendeleo ya biashara zao," alisema Waziri Mpango.
Hakuna maoni :
Chapisha Maoni