WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amemuagiza Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu kuboresha upatikanaji wa huduma katika hospitali ya Rufaa ya mkoa wa Dodoma kwa kuhakikisha inakuwa na dawa na vifaa tiba vya kutosha.
Ametoa agizo hilo jana (Jumamosi, Oktoba Mosi, 2016) wakati alipotembelea hospitali hiyo akiwa kwenye ziara ya kukagua maeneo ya kutolea huduma za jamii mjini Dodoma.
Waziri Mkuu amesema wakati Serikali ikishirikiana na uongozi wa mkoa huo katika kumaliza changamoto zinazoikabili hospitali hiyo manispaa nazo zinajukumu la kuboresha utoaji wa huduma za afya katika zahanati na vituo vya afya.
“Waziri Afya atawajibika kuimarisha hospitali ya mkoa na Manispaa waimarishe huduma katika zahanati zote na vituo vya afya ndani ya mkoa kwa kuziwezesha kuwa na majengo ya kutosha, kuongeza idadi ya watumishi na kuhakikisha zinakuwa na dawa na vifaa tiba,” alisema.
Aidha, Waziri Mkuu aliwataka watumishi wa hospitali hiyo kufanya kazi kwa uaminifu na uadilifu na isitokee watu wakakosa dawa au vipimo kwa sababu mmoja wao amechukua na kupeleka kwenye duka lake binafsi.
Pia Waziri Mkuu alimuagiza Mganga Mkuu wa Mkoa Dk. James Kiologwe kutafuta vijana watakaoweza kusafisha na kutengeneza bustani ya maua kwenye eneo lililoko karibu na uzio wa hospitali hiyo ili liwe na mandhari ya kuvutia.
Awali Mganga Mkuu wa mkoa, Dk. James Kiologwe aliiomba Serikali kupandisha hadhi hospitali hiyo na kuwa ya kanda kwa sababu mbali ya mkoa wa Dodoma, hospitali hiyo inahudumia wagonjwa wengine kutoka mikoa ya Iringa, Tabora, Singida na Manyara.
Akizungumzia upatikanaji wa tiba wakati Serikali imeanza kuhamia Dodoma, Dk. Kiologwe alisema mkoa huo unaweza kukabiliana na ongezeko la watumishi kwa una hospitali tano ambazo zina madaktari bingwa wa fani mbalimbali.
“Tunazo hospitali tano ambazo ni Benjamin Mkapa, Mirembe, DCMC, St. Gemma na hii ya ya Rufaa ya Mkoa zenye uwezo wa kutoa huduma za upasuaji, huduma kwa mama na mtoto, magonjwa ya moyo, mishipa, figo na saratani na huduma za mionzi,” alisema.
Katika hatua nyingine Dk. Kiologwe alisema hospitali hiyo imedumia wagonjwa wa nje 158,375 walipatiwa huduma katika hospitali hiyo katika kipindi cha Julai 2015 hadi Juni 2016 ambapo ni sawa na wastani wa wagonjwa 13,198 kwa mwezi.
“Magonjwa yanayoongoza kwa wagonjwa wa nje ni mivunjiko, shinikizo la damu, kisukari, homa ya mapafu na upungufu wa damu,” alisema.
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU
S. L. P. 980,
DODOMA.
JUMAPILI, OKTOBA 02, 2016
Hakuna maoni :
Chapisha Maoni