UONGOZI wa Klabu Bingwa ya Afrika Mashariki na Kati Azam FC, unayofuraha kuwaataarifu wapenzi wa soka kuwa jioni ya leo umefanikiwa kuingia mikataba na washambuliaji nyota kutoka Ghana, Samuel Afful na Yahaya Mohammed.
Zoezi la kuingiana mikataba limehudhuria na baadhi ya viongozi wakuu wa timu wakiwemo Ofisa Mtendaji Mkuu, Saad Kawemba, Meneja Mkuu, Abdul Mohamed, Kocha Mkuu Zeben Hernandez pamoja na wakala anayewasimamia wachezaji hao, Kingsley Atakorah, ambaye pia ni Ofisa Mtendaji Mkuu wa Adom Wonders Academy ya nchini Ghana.
Wakati Afful, 20, akisaini mkataba wa miaka mitatu, Mohammed aliyetua nchini leo mchana akitokea Ghana naye amesaini kandarasi ya miaka miwili tayari kabisa kuanza kuitumikia timu hiyo yenye maskani yake Azam Complex, Chamazi, Dar es Salaam.
Afful ambaye mpaka sasa yumo katika vikosi vya timu za vijana za Ghana chini ya umri wa miaka 20 na 23, anajiunga Azam FC akitokea timu ya Sekondi Hasaacan ya Ghana, ambayo aliifungia mabao tisa timu hiyo msimu uliopita.
Moja ya rekodi yake ni kuifungia bao muhimu timu ya Taifa ya Ghana chini ya umri wa miaka 20 (U-20) mwaka jana dhidi ya Zambia kwenye ushindi wa mabao 2-1, lililoipa nafasi ya kushiriki fainali za Kombe la Dunia nchini New Zealand, baada ya kutinga nusu fainali ya Mataifa ya Afrika kwa Vijana (U-20) zilizofanyika Senegal mwaka jana.
Mohammed, 28, ambaye ni mshambuliaji mzoefu anayetokea Aduana Stars, alikuwa ni mfungaji bora namba mbili wa Ligi Kuu ya Ghana msimu uliopita akifunga mabao 15, pungufu ya mabao mawili na kinara Latif Blessing (Liberty Proffessional) aliyetupia 17.
Azam FC tunaamini ya kuwa ujio wa nyota hao, utazidi kuipa nguvu timu yetu kuelekea kwenye michuano inayotukabili mbeleni, mzunguko wa pili wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara (VPL), Kombe la Kagame (CECAFA Kagame Cup) tukiwa kama mabingwa watetezi, Kombe la Shirikisho (Azam Sports Federation Cup) na Kombe la Shirkisho Afrika (CC) mwakani.
Azam FC tunapenda kuwafahamisha mashabiki wetu kuwa tutaendelea kuyafanyia kazi mapendekezo ya benchi la ufundi kwa kukifanyia marekebisho kikosi chetu katika usajili huu wa dirisha dogo uliofunguliwa jana, lengo ni kukipa nguvu zaidi kikosi ili kifanye vizuri zaidi katika michuano ya hapa nchini pamoja na ile ya Kimataifa.
Azam FC itaendelea kuwathamini mashabiki wake na tunaamini ya kuwa uwepo wenu utaendelea kutupa nguvu zaidi katika mapambano yetu makubwa ya kila siku na yaliyoko mbele yetu, tunachowaahidi ni kuendelea kuwapa furaha zaidi kwa kupata matokeo bora uwanjani na tunawaomba muendelee kuwa pamoja nasi.
Imetolewa na Uongozi wa Azam FC
Novemba 16, 2016.
Hakuna maoni :
Chapisha Maoni