Na Benny Mwaipaja, WFM, Dar es salaam
Waziri wa Fedha na Mipango, Dkt. Philip Mpango, ameahidi kushirikiana na Taasisi zote zilizo chini ya Wizara yake kwa kuhakikisha zinajiendesha kwa faida ili Serikali ifaidike na mapato yatokanayo na biashara za Taasisi na Mashirika yote kwa lengo la kukuza uchumi wa nchi pamoja na kupunguza umaskini.
Dkt. Mpango aliyasema hayo katika uzinduzi wa Bodi ya Wajumbe wa Shirika la Bima la Taifa (NIC), uliyofanyika katika Ukumbi wa Mikutano wa Mwalimu Nyerere, jijini Dar es Salaam.
Katika uzinduzi huo Waziri Mpango ameishauri NIC kutoa elimu ya kutosha kwa Wananchi walioko vijijini na mijini ili watambue umuhimu wa Bima mbalimbali zinazotolewa na Shirika hilo.
Aliongeza kuwa Shirika hilo linatakiwa kubuni mikakati mizuri ya kuongeza huduma za bima nchini hasa katika Sekta ya Kilimo, Ufugaji na Uvuvi kwa kuwa sekta hizo zimeajiri idadi kubwa ya wananchi ililiweze kupata faida na kutoa gawiwo kwa serikali.
“Naishauri Bodi iwe bunifu na kuhakikisha kuwa huduma za bima zinaelekezwa kwa wananchi waliowengi vijijini ambao wanakosa huduma hizo kwa kipindi kirefu ili waweze kunufaika na huduma hizo badala ya kung’ang’ania mijini kama zinavyofanya Benki” alisisitiza Dkt. Mpango
Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Bima la Taifa (NIC), Bw. Sam Kamanga, amesema kuwa Menejimenti itashirikiana bega kwa bega na Bodi iliyozinduliwa ili kurudisha hadhi ya Shirika hilo, lakini pia itafanya kazi kwa uaminifu na umakini mkubwa ili kuongeza idadi ya wateja ambao watachangia mapato ya Serikali.
Amesema kuwa Shirika hilo limejiekeza kupanua wigo wa utoaji wa huduma zake kwa kuanzisha Bima kwaajili ya wakulima, wafugaji na wavuvi kwa kuwa eneo hilo halijaweza kufikiwa na huduma hizo.
Kwa upande wa Mwenyekiti wa Bodi ya Shirika hilo, Bw. Laston Msongole, amesema kuwa Bodi hiyo itahakikisha kuwa shirika hilo linakuwa la kisasa na lenye tija kwa taifa.
Amesema katika kipindi kifupi cha kulifufua shirika hilo limeweza kupata faida ya zaidi ya shilingi Bilioni 6.8 hatua iliyoliwezesha kuwalipa wateja wao madai yao ya bima.
“Katika Kipindi cha mwaka mmoja wa Serikali ya awamu ya Tano, NIC imewalipa wateja wake madai yao yanayofikia kiasi cha shilingi Bilioni 1.26 sawa na asilimia 9.8 ya makusanyo yote ya biashara ya Bima katika kipindi cha Oktoba 2015/2016.
Ameiomba serikali iridhie maombi ya Shirika hilo ya kuiruhusdu iuze baadhi ya rasilimali zake yakiwemo majengo na viwanja ili lipate mtaji wa kutosha na kuliwezesha kulipa madai ya wateja wao ambao wameanza kulitumia tena shirika hilo kwa kasi baada ya kuboreshwa.
Shirika la Bima la Taifa (NIC) linashughulika na biashara ya Bima za Maisha na zisizo za maisha, ikiwemo kuuza bima za mali na ajali ambazo ni Bima za moto, magari, meli, ndege, wizi na ujenzi hali kadhalika kushughulikia biashara ya soko la pamoja la mashariki na kusini mwa Afrika (COMESA) na taasisi nyingine za kikanda.
Hakuna maoni :
Chapisha Maoni