WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amewataka watalaamu wa ujenzi wa mradi wa nyumba za makazi Magomeni watumie utaalamu wao vizuri na wakamilishe kwa wakati.
Ametoa agizo hilo leo mchana (Ijumaa, Novemba 18, 2016) wakati alipokagua ujenzi wa nyumba hizo zinazojengwa na wataalamu kutoka Wakala wa Majengo Tanzania (TBA) eneo la Magomeni Kota jijini Dar es Salaam.
Waziri Mkuu amewataka wataalamu hao waendelee kufanya kazi hiyo kwa kufuata misingi ya weledi wa taalauma yao kwani Serikali inawaamini. “Muhimu mjue kwamba mmepewa dhamana hii kubwa ya kukamilisha ujenzi huu ili wananchi waliokuwa wanaishi hapa waweze kurudi katika makazi yao,” amesema.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Ushauri wa TBA, Mhandisi Edwin Nnunduma amesema awamu ya kwanza ya ujenzi huo itahusisha majengo matano ya makazi. “Kati ya majengo haya matano, manne yatakuwa na ghorofa nane na moja litakuwa na ghorofa tisa, ambapo wakazi zaidi ya 600 waliokuwa wanaishi eneo hili tangu zamani watakabidhiwa,” amesema.
Mhandisi Nnunduma amesema majengo hayo yanajengwa kwa teknolojia ambayo imezingatia uwezo wa wakazi wake ambapo ina majiko yanayoweza kutumia kuni na mkaa.
Amesema mradi huo ambao unajengwa kwa awamu tofauti utahusisha ujenzi wa nyumba za makazi, maduka makubwa na ya kisasa pamoja na ofisi.
Mhandisi huyo amesema awamu ya kwanza iliyoanza Oktoba Mosi, mwaka huu inahusisha ujenzi wa nyumba za makazi ya wananchi waliokuwa wanaishi katika eneo hilo ambayo inatarajiwa kukamilika Oktoba, mwakani.
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
2 MTAA WA MAGOGONI,
S. L. P. 3021,
11410 DAR ES SALAAM. IJUMAA,
NOVEMBA 18, 2016.
Hakuna maoni :
Chapisha Maoni