Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), Jamal Malinzi amepokea kwa masikitiko makubwa taarifa za kifo cha Katibu wa zamani wa Chama cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Kagera (KRFA), Tryphone Peter Bayona.
Bayona, alifariki dunia jana jioni Novemba 23, 2016 akiwa na umri wa miaka 59. Alikuwa anapata matibabu kwenye Hospitali ya Mkoa Kagera.
Kutokana na msiba huo mzito kwa familia ya mpira wa miguu Mkoa wa Kagera, Rais wa TFF Malinzi, amemtumia salamu za rambirambi Katibu wa KRFA, Saloum Chama akielezea kwamba mkoa umepata pigo kubwa katika tansia ya soka hasa eneo la utawala.
Pia ametuma salamu hizo za rambirambi kwa familia ya marehemu Bayona, ndugu, java na marafiki ambayo kwa muda wa wiki mbili walikuwa wakimuuguza na kutokana na kifo hicho, amewataka kuwa watulivu kipindi hiki kigumu cha maombolezo ya mpendwa wao.
Rais Malinzi amemuelezea Bayona kuwa alikuwa ni mtu wa mpira wa miguu kwani hadi mauti yanamkuta, alikuwa Mwenyekiti wa Chama cha Soka Wilaya ya Bukoba Mjini.
Amesema historia ya Bayona ambayo Rais Malinzi aliangazia ni kuwa katibu msaidizi kuanzia mwaka 1991 akimsaidia Katibu wa KRFA wakati huo Ndugu Saloum Chama ambaye baadaye alihamia kwenye siasa na kuwa Diwani kuanzia mwaka 2000 hadi 2010.
Kwa kipindi ambacho Chama alikuwa diwani, Bayona alikuwa katibu wa KRFA kuanzia mwaka 2000 hadi 2012 kabla ya kuachia kiti hicho tena kwa Chama ambaye kwa kushirikiana na wadau wengine, wanaendeleza mpira wa miguu mkoa wa Kagera. Kwa nafasi ya ukatibu mkuu KRFA, moja kwa moja alikuwa Mjumbe wa Mkutano Mkuu wa TFF.
Mbali ya kuwa kiongozi kwenye chama - KRFA, Bayona anakumbukwa zaidi kwa utendaji wake akiwa Katibu Mkuu wa Klabu ya Balimi ambayo ilifanikiwa hadi kucheza Ligi Daraja la Kwanza.
Familia inaratibu mazishi ya Marehemu Bayona anayetarajiwa kuzikwa katika makaburi ya Bwanji yalioko Kiziba Wilaya ya Bukoba Vijijini, mkoani Kagera.
Bwana ametoa, bwana ametwaa. Mungu ampumzishe kwa amani marehemu Bayona.
IMETOLEWA NA SHIRIKISHO LA MPIRA WA MIGUU TANZANIA
Hakuna maoni :
Chapisha Maoni