.

.

.

.

.

.

.

.
KARIBUNI TUHABARIKE, TUELIMISHANE, TUPEANE HABARI ZA KUKUFANYA UTABASAMU KIDOGO NA MATUKIO YALIYOFANYIWA UCHUNGUZI WA KINA TOKA KILA PEMBE CONTACTS: +255 787 377 722 Email: drweyunga@gmail.com PIA UNAWEZA KUNI FOLLOW KUPITIA INSTAGRAM YANGU @drweyunga | TANGAZA NASI ILI UWAFIKIE WATU WENGI ZAIDI.

Ijumaa, 25 Novemba 2016

WAZIRI MKUU AHOJI TANZANIA KUTOKAMILISHA MKATABA WA MAWAKILI

*Ampa wiki moja Waziri kumueleza sababu

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa ametoa wiki moja kwa Waziri wa Katiba na Sheria, Dk. Harrison Mwakyembe kumpa maelezo kuhusu sababu za Tanzania kutokukamilisha mkataba wa Mawakili wa Afrika Mashariki kutambuana katika utendaji wao.

Ametoa agizo hilo leo (Ijumaa, Novemba 25, 2016) wakati akimuwakilisha Rais Dk. John Magufuli katika ufunguzi wa mkutano wa 21 wa mwaka wa Chama cha Wanasheria wa Afrika Mashariki kwenye Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNICC) jijini Dar es Salaam.

“Nimeshtushwa kidogo kusikia kwenye taarifa yenu kuwa mkataba huo uliolenga nchi zote za Afrika Mashariki hautaihusisha Tanzania kutokana na kutokukamilisha sehemu yao ya kuufanyia kazi, nitahitaji maelezo,”

“Nitapenda kupata maoni yako wewe mwenyewe Mheshimiwa Waziri wa Katiba na Sheria wa Tanzania kwa vile wewe ni Mwanasheria mwandamizi na siyo Mwanasheria wa Tanganyika Law Society peke yake kwa nini Tanzania haijakamilisha mkataba huu,” amesisitiza.

Waziri Mkuu amesema kwa mujibu wa maelezo ya awali aliyopewa kuhusu mkataba huo, utakuwa na umuhimu mkubwa kwenye ukanda wa Afrika Mashariki kama ilivyo kwenye sekta nyingine zinazoshirikiana ikiwemo uhandisi, uhasibu, uthamini na uchoraji wa majengo.

Katika hatua nyingine Waziri Mkuu amewataka Wanasheria hao kuzisaidia nchi zao ili ziondokane na umaskini uliokithiri na Serikali zipate muda wa kushirikisha watu wake katika kufanya kazi kwa lengo la kuwapatia maendeleo.

Amesema nchi zilizoendelea na zinazoendelea, baada ya chaguzi hufanya shughuli za ujenzi wa taifa lao na maendeleo ya watu wake. Ili kudumisha demokrasia wana muda wa mikutano na maandamano na kazi.

“Hawaandamani tu bila kupata kibali cha Polisi, hawaruhusiwi kuzuia magari yasipite, kuzuia kazi isifanyike. Mfano kifungu cha 115 cha Sheria ya Taifa ya Uchaguzi, kinataka kesi zinazotokana na uchaguzi ziwe zimefunguliwa mahakamani ndani ya siku thelathini tangu kutangazwa kwa matokeo ya uchaguzi na ziwe zimesikilizwa na kutolewa maamuzi ndani ya miezi kumi na miwili tangu tarehe ya kufunguliwa mahakamani,” amesema..

Amesema “kwa uelewa wa kawaida, Kifungu hiki ni kuwa jamii inataka masuala ya siasa za uchaguzi yawe na muda wake wenye ukomo maalum ili baada ya hapo wananchi waelekeze muda, nguvu na rasilimali zao nyingine katika kazi au shughuli nyingine za maendeleo na ujenzi wa Taifa lao”.

Aidha, Waziri Mkuu amesema eneo jingine ambalo ni muhimu kulitupia jicho ili kukuza ushindani wa kibiashara katika Jumuia ya Afrika Mashariki ni la uendeshaji wa mashauri mahakamani hasa kwa mashauri ya madai.

“Wote tunakubaliana kuhusu misingi na haki za kidemokrasia kuwa kila mtu anayo haki kikatiba na kisheria kusikilizwa madai yake na kutetea haki zake; na kuwa chombo chenye mamlaka ya kutoa haki ni Mahakama”. Amesema.

Amesema kuna taarifa za kuwepo kwa kesi zenye kuhusisha mali za thamani kubwa zinazochukua muda mrefu sana kumalizika mahakamani huku baadhi ya sababu za kuchelewa kwa kesi hizo ni utoaji wa maombi ya kuziahirisha mara kwa mara kwa sababu binafsi jambo linalosababisha uendeshaji wa kesi kuwa mgumu na kuchukua muda mrefu.

Waziri Mkuu amesema wakati mwingine hata kesi zilizosikilizwa huendelea kubaki mahakamani muda mrefu kutokana na maombi na rufaa za hapa na pale zinazoishia kumnyima mwenye haki fursa ya kutekelezewa haki yake.

“Ni wazi kesi kama hizi zinapohusisha mahusiano ya kibiashara na au mitaji mikubwa ya biashara, matokeo yake ni kudumaza na hata kuua biashara, achilia mbali ushindani wa kibiashara. Ni wajibu wenu Wanasheria kupata ufumbuzi wa tatizo hili lenye athari hasi kibiashara,’ amesema.

Amesema haki ya wadaiwa kusikilizwa kikamilifu na Mahakama, haki na uhuru mlionao Mawakili kuwawakilisha wadaiwa wao bila hofu au shinikizo lolote, viwe chachu ya maendeleo ya ushindani wa kibiashara na visiwe kikwazo.

IMETOLEWA NA: 

OFISI YA WAZIRI MKUU, 
2 MTAA WA MAGOGONI, 
S. L. P. 3021, 
11410 DAR ES SALAAM. 
IJUMAA, NOVEMBA 25, 2016.

Hakuna maoni :

Chapisha Maoni