KLABU Bingwa ya Afrika Mashariki na Kati, Azam FC, leo asubuhi kabla ya kuanza rasmi mazoezi ya maandalizi ya mzunguko wa pili wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara (VPL) utakaoanza rasmi Desemba 17 mwaka huu, wachezaji na benchi la ufundi walisimama kwa dakika moja kuomboleza kifo cha mchezaji wa timu ya vijana ya Mbao, Ismail Khalfan.
Khalfan alifariki dunia jana wakati akikimbizwa hospitali baada ya kudondoka uwanjani kufuatia kugongana na beki wa Mwadui kwenye mchezo wao wa michuano ya Ligi ya Taifa ya Vijana kituo cha Bukoba mkoani Kagera kinachohusisha timu za Kundi B.
Kikosi hicho kimerejea tena kwenye mazoezi kufuatia kuwa mapumzikoni kwa muda wa takribani wiki mbili mara baada ya kumalizika kwa mzunguko wa kwanza.
Ni wachezaji watatu tu wa Azam FC waliokosekana kwenye mazoezi hayo wakiwa na ruhusa maalumu, ambao ni beki Erasto Nyoni, washambuliaji wapya kutoka Ghana, Samuel Afful na Yahaya Mohammed, wanaotarajiwa kuanza rasmi kujifua na wenzao kuanzia kesho Jumanne.
Wachezaji wengine walioshindwa kufanya mazoezi ni winga Khamis Mcha, anayesumbuliwa na maumivu ya nyonga ambaye alipewa programu maalumu ya mazoezi na Mtaalamu wa Viungo wa Azam FC, Sergio Perez Soto, huku beki wa kushoto, Gadiel Michael, akiwa ameteguka mkono alioumia wakati akifanya mazoezi binafsi wakati wa likizo iliyopelekea kufungwa plasta gumu ‘p.o.p’.
Akizungumza na mtandao rasmi wa klabu www.azamfc.co.tz kuhusu programu yake ya wiki hii, Kocha Mkuu wa Azam FC, Zeben Hernandez, ameelezea kufurahishwa na namna wachezaji wake walivyorejea mazoezini wakiwa na hali nzuri licha ya kutoka mapumzikoni hali ambayo inampa wakati mzuri kukiandaa kikosi chake kuelekea mechi za mzunguko wa pili.
“Tumeanza mazoezi leo kwa spidi kubwa kwa ajili ya kuingia kwenye mzunguko wa pili wa ligi, tumeanza kwa mazoezi mara moja leo, kesho (Jumanne) tutafanya mara mbili asubuhi na jioni kwa ajili ya kuwa fiti zaidi tayari kuingia kwenye ushindani, kwa sasa tunawasubiria wachezaji wambao hawajafika (Erasto, Yahaya, Afful), ambao watajiunga nasi kesho,” alisema.
Katika kuimarisha safu yake ya ulinzi, Azam FC imemrejesha kikosini beki wake wa kati, Abdallah Kheri, aliyekuwa akicheza kwa mkopo kwenye timu Ndanda ya Mtwara katika mzunguko wa kwanza wa ligi.
Azam FC inayoshika nafasi ya tatu kwenye msimamo ikiwa na pointi 25, inatarajia kufungua dimba la raundi ya pili ya ligi, kwa kukipiga na African Lyon Desemba 18 mwaka huu, mchezo unaotarajiwa kufanyika katika Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam.
Hakuna maoni :
Chapisha Maoni