Bocco ametoa kauli hivi karibuni mara baada ya kumalizika kwa mchezo uliopita wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania (VPL) dhidi ya Tanzania Prisons walioifunga bao 1-0, huku akifanikiwa kutupia bao hilo pekee lililorudisha morali ndani kikosi hicho baada ya kutofanya vizuri kwenye mechi mbili za ufunguzi wa mzunguko wa pili walipocheza ugenini na African Lyon (0-0) na Majimaji (1-1).
“Kwanza tunawashukuru mashabiki wetu kwa uvumilivu waliouonyesha, kwa sapoti waliotupa katika kipindi chote kigumu tulichopitia, kama wachezaji na timu kwa ujumla tunawaomba waendelee kuwa na moyo huo huo na pia tunawatakia kheri ya mwaka mpya (2017) na wamalize mwaka huu vizuri, tuendelee kuwa pamoja ili kuisaidia timu yetu iweze kufanya vizuri,” alisema Bocco wakati akizungumza na mtandao rasmi wa klabu www.azamfc.co.tz
Bocco ambaye ameipatia mafanikio makubwa Azam FC kwa mabao yake muhimu tokea timu hiyo ikiwa madaraja ya chini hadi kupanda Ligi Kuu mwaka 2008, aliendelea kusema kuwa wamepitia changamoto nyingi sana kwa mwaka huu unaoisha huku akidai kuwa wamejifunza kupitia hayo na wanachoangalia kwa mwaka mpya ni kuipeleka mbele zaidi timu hiyo ili kufikia mafanikio.
“Changamoto zilikuwepo nyingi na ni sehemu ya maisha, sisi kama timu tunajua mpira unachangamoto zake na tumezipokea kama binadamu na sisi wachezaji changamoto iliyokuwa katika kazi yetu haikuwa ndogo na tunamshukuru Mungu kwa kuweza kutusaidia tumeweza kupigana nazo na hatukuweza kukata tamaa, kikubwa tunachofanya hivi sasa ni kuangalia mbele zaidi ili kuipatia timu mafanikio kwa mwaka unaokuja,” alisema.
Azam FC mbali na kuwa bingwa mtetezi wa michuano ya Klabu Bingwa ya Afrika Mashariki na Kati (CECAFA Kagame Cup), inamaliza mwaka huu ikiwa imefanikiwa kukata tiketi ya kushiriki michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika mwakani pamoja na taji la Ngao ya Jamii baada ya kuichapa Yanga kwa mikwaju ya penalti 4-1 kufuatia sare ya mabao 2-2 ndani ya dakika 90 za mchezo huo uliofungua pazia la ligi msimu huu.
Ujio wa Mapinduzi Cup
Wakati kikosi cha timu hiyo kikielekea mchana wa leo Jumamosi visiwani Zanzibar kwenda kushiriki michuano ya Kombe la Mapinduzi, Bocco amesema kuwa wao kama wachezaji wanaenda kushindana na hatimaye kurejea na ubingwa wa michuano hiyo.
“Mashindano ya Mapinduzi si mageni kwa Azam FC, michuano hiyo si mepesi ni migumu, sisi kama wachezaji tunaenda kushindana naamini ni sehemu moja ya msimu huu ambayo tukiweza kuchukua kombe itakuwa ni faraja kwa klabu na mashabiki wetu pamoja na sisi wachezaji, tukitoka huko hata tukirudi kwenye ligi tutakuwa na morali nzuri ya kuendeleza ushindi kwenye ligi, michuano ya FA na Kombe la Shirikisho Afrika,” alimalizia Bocco.
Azam FC inayodhaminiwa na kinywaji safi cha Azam Cola kinachosisimua mwili na kuburudisha koo pamoja na Benki ya NMB, inaenda huko ikiwa na kumbukumbu nzuri ya kulitwaa taji hilo mara mbili (2012,2013), ambapo itaanza kufungua dimba Jumatatu ijayo kwa kuvaana na Zimamoto saa 10.15 jioni.
Mabingwa hao wa Ngao ya Jamii wapo Kundi B pamoja na timu nyingine za Yanga na Jamhuri
Hakuna maoni :
Chapisha Maoni