




Picha na – OPMR – ZNZ.
Benki ya Kimataifa ya Exim ya Serikali ya Jamuhuri ya Watu wa China imeahidi kuendelea kushirikiana na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar katika kusaidia Maendeleo ya Wananchi wake kupitia miradi tofauti inayoanzishwa.
Kauli hiyo imetolewa na Makamu wa Rais wa Benki hiyo Bwana Sun Ping wakati wa mazungumzo yake na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi anayeuongoza Ujumbe wa Viongozi Wanne wa Serikali akimalizia ziara yake ya Kiserikali ya Siku Tano Nchini China.
Bwana Sun Ping alisema Taasisi hiyo ya Fedha ya China imeridhika na hatua kubwa ya maendeleo iliyofikiwa na Zanzibar katika kuimarisha uchumi wake kiasi kwamba Benki hiyo itaangalia namna za kusaidia nguvu katika kuona miradi inayoanzishwa inatekelezwa.
Makamu wa Rais wa Benki hiyo ya Exim alimueleza Balozi Seif na Ujumbe wake kwamba Tanzania ndio nchi pekee iliyopewa kipaumbele na benki hiyo katika kupatiwa mikopo na misaada ikilinganishwa na Nchi nyengine Barani Afrika.
Akitoa shukrani zake Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi aliipongeza Benki hiyo ya Exim kwa ukarimu wake wa kuunga mkono miradi ya Maendeleo inatotekelezwa na Zanzibar kwa njia ya misaada na hata mikopo.
Balozi Seif alisema yapo mafanikio makubwa yaliyopatikana miongoni mwa Wanachi waliowengi Zanzibar kufuatia kuibuka kwa miradi kadhaa ya Kiuchumi na maendeleo iliyopata msukumo kupitia Benki hiyo ya Kimataifa ya Exim.
Othman Khamis Ame
Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar
23/11/2016.
Hakuna maoni :
Chapisha Maoni