Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu (Watu wenye Ulemavu) Mhe. Dkt. Abdallah Possi akitoa maelekezo kwa Mkuu wa Wilaya ya Masasi Mhe. Selemani Mzee (wa kwanza kulia) wakati wa ziara yake katika shule ya Masasi yenye kuhudumia wenye ulemavu Mkoani Mtwara.
(PICHA ZOTE NA OFISI YA WAZIRI MKUU).
Na. Mwandishi Wetu
Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia masuala ya Watu wenye Ulemavu, Mhe. Dkt. Abdallah Possi ameitaka jamii kuzingatia haki na usawa kwa watu wenye ulemavu nakuondokana na imani potofu za kuona watu wenye ulemavu hawana uwezo wa kufanya shughuli za maendeleo.
Mhe. Possi ameyasema hayo kwa nyakati tofauti alipotembelea Vituo na Shule zinazohudumia watu wenye mahitaji maalum vya Nandanga, Rasi Bula, Shule ya msingi Nyangao mkoani Lindi pamoja na makazi ya wenye ulemavu na Ukoma ya Mkaseka, Chuo cha wenye Ulemavu cha Mtapika, shule ya Lulindi na Masasi mkoani Mtwara.
Katika ziara hiyo Mhe.Possi alisisitiza jamii zibadili mitazamo hasi juu ya masuala ya haki na usawa kwa watu wenye ulemavu kwa kuwashirikisha katika shughuli zote na kuwapa vipaumbele vya fursa sawa.
“Ninasisitiza jamii ibadili mitazamo dhaifu juu ya haki na usawa wa kuwashirikisha watu wenye ulemavu kwani wana uwezo wa uzalishaji endapo tutawapa fursa sawa kama ilivyokuwa kwa wakina mama walipoachwa nyuma muda mrefu ila jamii imeona fursa ndani yao, iwe hivyo hivyo kwa watu wenye ulemavu” alisema.
Aidha Waziri Possi ameweka mkazo juu ya kuwahusisha na kutokuwaona kuwa ni kundi la kuachwa nyuma na kama tegemezi.
“sheria zipo wazi kabisa zinazotuelekeza juu ya haki na usawa kwa watu wenye ulemavu kwa mujibu wa matakwa ya Sheria ya watu wenye Ulemavu namba 9 ya mwaka 2010 inayoeleza haki za watu wenye Ulemavu kuwahudumia kwa haki na usawa na kuboresha maeneo muhimu ikiwemo fursa za kielimu, ajira, kiuchumi na kijamii,” alieleza.
Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Ruangwa Mhe. Joseph Mkirikiti alikiri kuyapokea yote aliyoeleza Mhe.Waziri katika ziara yake na kuipongeza Serikali kwa juhudi za kuisaidia jamii bila kujali hali zao na tofauti zao.
“Ninaipongeza Serikali ya Awamu ya Tano inayowajali wanyonge na kujali haki zao pamoja na mhe. Waziri kwa kuona umuhimu wa kututembelea wana Ruangwa na tunaahidi kukuweka katika kumbukumbu zetu maana umewagusa wakazi wa Mtwara hususani wazee na watu wenye ulemavu.”Alisisitiza Mkuu wa Wilaya hiyo.
Nae Afisa Mfawidhi kituo cha Kulelea wazee wenye ukoma cha Mkaseka Bw. Cleophace Nguli aliiomba Serikali kuendelea kuwakumbuka watu wenye ulemavu ikiwa ni watu waliosahaurika na kuendelea kupongeza hatua zilizopo kwa sasa.
Hakuna maoni :
Chapisha Maoni