.

.

.

.

.

.

.

.
KARIBUNI TUHABARIKE, TUELIMISHANE, TUPEANE HABARI ZA KUKUFANYA UTABASAMU KIDOGO NA MATUKIO YALIYOFANYIWA UCHUNGUZI WA KINA TOKA KILA PEMBE CONTACTS: +255 787 377 722 Email: drweyunga@gmail.com PIA UNAWEZA KUNI FOLLOW KUPITIA INSTAGRAM YANGU @drweyunga | TANGAZA NASI ILI UWAFIKIE WATU WENGI ZAIDI.

Jumanne, 10 Januari 2017

BALOZI SEIF AWATAKA VIJANA KUWA CHANZO CHA MAENDELEO

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi akivishwa Skafu na Vijana wa Chipukizi kabla ya kuyafunga matembelezi wa UVCCM yaliyohitimishwa hapo Afisi Kuu ya CCM Kisiwandui Mjini Zanzibar.
Vijana wa UVCCM wapatao 400 wakihitimisha matembezi yao ya kuadhimisha miaka 53 ya Mapinduzi ya Zanzibar yaliyopokelewa na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi hayupo pichani.

Balozi Seif akipokea Picha ya Muasisi wa Mapinduzi ya Zanzibar Marehemu Mzee Abeid Aman Karume iliyotumiwa na Vijana hao katika matembezi yao.

Wa kwanza kutoka kulia ni Kaimu Katibu Mkuu wa Umoja wa Vijana wa CCM Tanzania Ndugu Shaka Hamdu Shaka NA Makamu Mwenyekiti wa Umoja huo Bibi Mboni Muhita.
Balozi Seif akipokea Picha ya Muasisi wa Muungano wa Tanganyka na Zanzibar Marehemu Mwalimu Julius K. Nyerere iliyotumika kwenye matembezi hayo.
Vijana wa UVCCM wakimkabidhi Bendere ya Zanzibar Balozi Seif waliyoitumia kama kielelezo kwenye matembezi yao ya kuunga mkono sherehe za kutimia miaka 53 ya Mapinduzi ya Zanzibar.
 Balozi Seif akipokea Bendere ya Serikali ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania iliyotumiwa na Vijana hao kwenye matembezi yao tokea walipoanza juzi katika Kijiji cha Donge Mkoa wa Kaskazini Unaguja. Picha na –OMPR – ZNZ.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alisema Taifa linawategemea Vijana wakati wowote katika dhana nzima itakayothibitisha kwamba wanasimamia kwa vitendo Mapinduzi katika kuondoa maovu yote yanayolikabili Taifa.

Alisema Serikali zote mbili ile na Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania na iIe ya Mapinduzi ya Zanzibar zinataka kuona Vijana wake wanakuwa chem chem ya Maendeleo badala ya kuwa dimbwi la matatizo mitaani.

Balozi Seif Ali Iddi alitoa kauli hiyo wakati akiyafunga Matembezi ya Umoja wa Vijana wa Chama cha Mapinduzi { UVCCM } kuunga mkono maadhimisho ya sherehe za kutimia miaka 53 ya Mapinduzi ya Zanzibar ya mwaka 1964 hapo Afisi Kuu ya CCM Kisiwandui Mjini Zanzibar.

Alisema Vijana ambao ndio warithi wa kulinda Mapinduzi ya Zanzibar dhana iliyoanzishwa na muasisi wa Mapinduzi hayo Mzee Abeid Amani Karume wana wajibu wa kusimamia vita vya mapambano dhidi ya matumizi ya dawa za kulevya, udhalilishaji wa wanawake na watoto, uonevu pamoja na ufisadi.

Balozi Seif alikariri maneno ya Marehemu Mzee Abeid Amani Karume yaliyoeleza maana halisi ya Mapinduzi daima ambayo sio kupindua watu bali ni kuondoa matendo mabaya katika jamii na kusimamia haki na mazuri yote.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar alisema Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar itaendelea kuondoa matendo yote maovu ikiwemo uzembe, uonevu na ubaguzi mambo yanarejesha nyuma au kukwamisha juhudi za Taifa za kuleta Maendeleo ya Umma.

Alieleza faraja yake kuona ushiriki wa Vijana katika matembezi hayo ni mkubwa kiasi kwamba wanalidhihirishia Taifa na Viongozi wake jinsi gani walivyokomaa kisiasa pamoja na utayari wao unathibitisha kwamba wako imara kutetea kwa vitendo Mapinduzi ya Zanzibar yaliyoondoa madhila ya Kikoloni.

Akizungumzia changamoto kubwa zinazowakabili Vijana hasa ukosefu wa ajira ambalo limekuwa likizikumba nchi mbali mbali Duniani Balozi Seif alisema Takwimu za Kimataifa zinathibitisha wazi kwamba zaidi ya Vijana 73 Milioni wanakadiriwa kuwa hawana ajira.

Alisema kwa bahati mbaya mara nyingi changamoto hii ya ukosefu wa ajira kwa Vijana huhusishwa kuwa ndio chanzo cha vitendo viovu vinavyofanywa na Vijana katika Mataifa mbali mbali Duniani.

Balozi Seif alifahamisha kwamba Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imeandaa Mipango imara ya kukabiliana na changamoto hiyo hali inayobainisha kuwa sio nzuri na jamii imekuwa ikishuhudia nafasi moja ya ajira nchini kugombewa na vijana zaidi ya 20.

Alisema miongozi mwa mipango hiyo ni kuongezwa kwa nafasi za mafunzo ya amali Nchini ambapo Vituo Vipya Viwili vya amali vinategemewa kujengwa huko Makunduchi Mkoa Kusini kwa upande wa Unguja na Mtambwe Mkoa wa Kaskazini kwa upande wa Pemba.

Balozi Seif alisema Vituo hivyo vitafanya idaidi ya vituo Vinne vya mafunzo ya Amali nchini vitakavyotegemewa kuchukuwa idadi kubwa ya Vijana katika kupata taaluma itayowasaidia kuwa na uwezo wa kujiajiri wao wenyewe hapo baadaye.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar alielezea mpango mwengine wa uhakika uliobuniwa na Serikali wa kupambana na ukosefu wa ajira ni suala la kukuza uchumi kwa njia ya kukaribisha wawekezaji kwenye Sekta ya Utalii.

Alisema mradi mkubwa wa sekta ya Utalii unaotekelezwa na Kampuni ya Penny Royal wa Zanzibar Amber Resort wenye thamani ya Dola za Kimarekani Bilioni 1.6 wa ujenzi wa nyumba za wageni 1,900, viwanja vya michezo, uwanja wa ndege utatoa jira kubwa kwa Vijana.

Mapema akitoa taarifa ya matembezi hayo Kaimu Katibu Mkuu wa UVCCM Tanzania Ndugu Shaka Hamdu Shaka alisema Vijana wengi nchini huingia katika majaribu ya kudanganywa historia ya Zanzibar na kupelelekea kukejeli Mapinduzi ya Zanzibar ya Mwaka 1964.

Nd. Shaka alisema Mapinduzi ya Zanzibar yametandikwa kwa zulia la Umoja, Upendo na mshikamano chini ya majemadari waliofanya mapinduzi hayo ambao wanastahiki kuendelea kuenziwa na wananchi na Vijana wa kizazi cha sasa.

Alisema vilivyokuwa vikifanywa na watawala wa visiwa vya Zanzibar vilisababisha vitendo vya unyanyasaji, uonevu na madhila yaliyochangia kuwakosesha haki zao za msingi wakwezi na wakulima wa Visiwa hivyi yakiwemo masuala muhimu ya huduma za msingi kama afya, elimu na umiliki wa ardhi.

Akitoa salamu Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania anyesimamia Mazingira na Muungano Mh. Januari Yussuf Makamba alisema Mapinduzi ya Zanzibar ni kielelezo tosha cha kujitambua kwa waafrika wa Visiwa vya Zanzibar.

Mh. Januari alisema Wakombozi wa Mapinduzi ya Visiwa vya Zanzibar wameacha urithi mkubwa kwa vijana wa Kizazi kipya unayostahiki kulindwa na kuendelezwa kwa faida na maslahi ya Wananchi wake.

Alisema njia pekee na sahihi ya kuendelea kuimarika kwa Muungano wa Tanganyika na Zanzibar ni kudumisha Mapinduzi ya Zanzibar kupitia njia ya kuipatia ushindi CCM katika chaguzi zote zinazoendelea kufanyika hapa Nchini.

Matembezi ya Umoja wa Vijana wa Chama cha Mapinduzi { UVCCM } kuadhimisha miaka 53 ya Mapinduzi ya Zanzibar yaliyoshirikisha Vijana 400 yameanza juzi katika Kijiji cha Donge Mkoa wa Kaskazini Unguja na kumalizikia Afisi Kuu ya CCM Kisiwanduzi.

Othman Khamis Ame 
 Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar 
 10/1/2017.

Hakuna maoni :

Chapisha Maoni