.

.

.

.

.

.

.

.
KARIBUNI TUHABARIKE, TUELIMISHANE, TUPEANE HABARI ZA KUKUFANYA UTABASAMU KIDOGO NA MATUKIO YALIYOFANYIWA UCHUNGUZI WA KINA TOKA KILA PEMBE CONTACTS: +255 787 377 722 Email: drweyunga@gmail.com PIA UNAWEZA KUNI FOLLOW KUPITIA INSTAGRAM YANGU @drweyunga | TANGAZA NASI ILI UWAFIKIE WATU WENGI ZAIDI.

Jumanne, 10 Januari 2017

WASTAAFU KANDA YA ZIWA WATAKIWA KUJITOKEZA KUHAKIKIWA

Mkaguzi Mkuu wa Ndani wa Serikali, Msaidizi, Bw. Stancilaus Mpembe, akizungumza na waandishi wa habari mkoani Mwanza wakati wa Uzinduzi wa zoezi la Uhakiki wa Wastaafu wanaolipwa na Wizara ya Fedha na Mipango Kanda ya Ziwa.
Baadhi ya wastaafu wakiwa wanahakikiwa na Wakaguzi wa ndani wa Serikali mkoani Mwanza katika uzinduzi wa zoezi la Uhakiki wa Wastaafu wanaolipwa na Hazina, huku wengine (waliosimama kulia) wakiwa katika foleni.
Picha ya pamoja ya Wakaguzi wa Ndani wakiendelea na zoezi la Uhakiki wa Wastaafu Wanaolipwa na Wizara ya Fedha na Mipango mkoani Mwanza, huku baadhi ya wastaafu wakiendelea kusubiri zamju zao katika viti.
Baadhi ya wastaafu wakiwa wamepumzika wakisubiri zamu zao za kuhakikiwa wakati wa zoezi la Uhakiki wa Wastaafu wanaolipwa na Hazina, utakao dumu hadi mwishoni mwa juma, jijini Mwanza.

                                                                                    Na Benny Mwaipaja, WFM, Mwanza

Wizara ya Fedha na Mipango yawataka wastaafu wanalipwa na Hazina ambao hawajahakikiwa katika mikoa ambayo zoezi hilo limeshafanyika na wanauwezo wa kufika katika maeneo ambayo zoezi hilo linaendelea , wajitokeze kwa wingi kwa ajili ya kuhakikiwa.

Wito huo umetolewa mkoani Mwanza na Mkaguzi wa Ndani Mkuu wa Serikali, Msaidizi, Bw. Stanislaus Mpembe wakati wa uzinduzi wa zoezi la Uhakiki wa Wastaafu wanaolipwa na Wizara ya Fedha na Mipango katika Kanda ya Ziwa, mikoa ya Mwanza, Kagera, Mara, Shinyanga, Simiyu na Geita.

Mpembe alisema kuwa zoezi hilo ni muhimu kwa wastaafu na Serikali kwa ujumla kwani limelenga kuiwezesha Wizara ya Fedha na Mipango kuhuisha taarifa za Wastaafu, kupata orodha sahihi ya wastaafu wanaolipwa na Wizara hiyo ili Serikali iweze kuwalipa wale wote wanaostahili.

Alifafanua kuwa suala la uhakiki ni la lazima na kuwaomba wastaafu wajitokeze kwa wingi kwani baada ya zoezi hilo kumalizika nchi nzima wastaafu ambao hawatahakikiwa watafutwa katika mfumo wa malipo.

“Naomba wastaafu wote wajitokeze katika Halmashauri zilizotangazwa, hata wasiokuwa na nyaraka wajitokeze wataelekezwa mahali wanapoweza kupata nyaraka zote muhimu” aliongeza Bw. Mpembe.

Alisema kuwa wagonjwa na wasiojiweza wametengewa siku ya Ijumaa ambayo ni siku ya mwisho ya uhakiki, ambapo watakuja ndugu au jamaa zao watakaotoa taarifa sehemu walipo hususani waliopo hospitalini na sehemu ambazo zinaweza kufikika kwa karibu na wahakiki ili nao wahakikiwe.

Naye Mstaafu John Msanja, pamoja na kuomba serikali iwafikirie kuwaongezea pensheni ili waweze kukabiliana na hali ngumu ya maisha inayowakabili, aliipongeza Serikali kupitia Wizara ya Fedha na Mipango pamoja na waratibu kwa kuendesha zoezi hilo kistaarabu pamoja na kutoa kipaumbele kwa wagonjwa na wasiojiweza ambao waliweza kufika katika eneo hilo kwa lengo la kuhakikiwa.

Alisema kuwa zoezi hilo linaonesha ni namna gani Serikali inawajali wazee waliolitumikia Taifa kwa muda mrefu kwa kuhakikisha ni namna gani wanapata stahili zao kwa wakati.

Zoezi hili lilianza Oktoba, 2016 katika Mkoa wa Pwani na kuendelea katika mikoa ya Nyanda za Juu Kusini, Kanda ya Kati na Kanda ya Kaskazini. Mpaka sasa wastaafu wa mikoa 13 ya Tanzania Bara wameshahakikiwa.

Baada ya uhakiki kumalizika Kanda ya Ziwa, zoezi hili litaendelea katika mikoa ya Kigoma na Tabora.

Mwisho

Hakuna maoni :

Chapisha Maoni