WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesifia huduma za tiba zinazotolewa kwenye kituo cha afya Mabada katika wilaya ya Songea licha ya kuwa ni kidogo.
Akizungumza na watumishi wa kituo hicho, mwishoni mwa wiki, Waziri Mkuu alisema licha ya kuwa Halmashauri ya Wilaya ya Madaba ni mpya, bado huduma zinazotolewa ni za kuridhisha na amepata uthibitisho huo kwa baadhi ya wagonjwa waliolazwa kwenye kituo hicho.
“Hali ya usafi ni nzuri, huduma zilizopo zinaridhisha… nimewadadisi baadhi ya wagonjwa wamesema huduma ziko vizuri. Mara nyingi huwa naongea nao kutaka kujua kama kuna rushwa, lugha kali kutoka kwa wauguzi au ukosefu wa dawa, lakini hapa wamenithibitishia kuwa huduma ziko vizuri, hongereni sana,” alisema.
Alisema amelazimika kuyasema hayo mbele ya watumishi wote kwa sababu katika upya wa halmashauri, lazima kungekuwa na mizengwe na usumbufu katika upatikanaji wa huduma hali ambayo huwa inachosha wagonjwa hadi wanalazimika kutoa kitu kidogo ili wapatiwe huduma kwa haraka.
Akizungumzia upatikanaji wa huduma za bima ya afya, Waziri Mkuu aliupongeza Mfuko wa Bima ya Afya (NHIF) kwa kusogeza huduma zake kwa jamii na kusaidia kuwapatia dawa, vifaa tiba na mashuka pea 25.
Akitoa maelezo wakati akikagua majengo hayo, Meneja wa NHIF mkoa wa Ruvuma, Bw. Abdiel Mkaro alimweleza Waziri Mkuu kwamba taasisi hiyo imekisaidia kituo hicho kupata dawa na vifaa tiba vyenye thamani ya sh. milioni 27.
“Tunashukuru sana kwa msaada wenu na ninaomba ufikishe salamu hizi kwa Mkurugenzi Mkuu wa NHIF. Nimeona pia mashuka mliyotoa, tunawashukuru sana.”
Waziri Mkuu alitumia fursa hiyo kwa kuwapongeza viongozi wa Halmashauri ya Wilaya ya Madaba kwa kuwasajili wakazi wengi kwenye Mfuko wa Afya ya Jamii (CHF) jambo ambalo alisema linawapunguzia usumbufu wa kupata huduma za afya wakazi hao.
“Nimewauliza kule mawodini kama wamejiunga na kila niliyeongea naye alikuwa akinionyesha kadi yake. Ninawapongeza Mkuu wa Wilaya, Mkurugenzi wa Halmashauri, Baraza zima la madiwani pamoja na timu yenu kwa hii nzuri ya kuwashawishi wananchi wajiunge na mfuko huu,” alisema.
Mganga Mkuu wa Halmashauri ya Wilaya ya Madaba, Dk. Mustafa Waziri alisema wamekwishasajili kaya zaidi ya 3,000 kwenye Mfuko wa Afya ya Jamii. “Tunaishukuru NHIF ambayo pia ina wanachama 527 ambao ni watumishi wa Halmashauri lakini wana mpango wa kusajili wengine 500 ambao ni wajasiriamali na wanachama wa SACCOS,” alisema Dk. Waziri.
Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu alisema Serikali itaangalia uwezekano wa kukipandisha hadhi kituo hicho cha afya kiweze kutoa huduma za hospitali ya wilaya ili tiba zote za muhimu zipatikane hapo badala ya kuwalazimisha wagonjwa waende Songea mjini ambako ni umbali wa zaidi ya km.120 kutoka Madaba.
“Kituo hiki kipo karibu sana na njia kuu iendayo Dar es Salaam, ikitokea ajali hapa kama hakuna huduma stahiki itakuwa shida kuwahudumia majeruhi; ndiyo maana tunaona ni vema kipandishwe hadhi ili kiweze kutoa huduma zote hapa hapa. Na kama ni kwenda Songea mjni basi iwe kwa dharura haswa,” alisema huku akishangiliwa.
Hata hivyo, Waziri Mkuu aliitaka Halmashauri hiyo iangalie uwezekano wa kuongeza jengo la la ‘Grade A’ ili yawe mawili tofauti kwa ajili ya wanawake na wanaume. “Hali ilivyo hivi sasa, akilazwa mwanaume katika hiyo wodi, mwanamke hawezi kulazwa huko. Angalieni wa kuboresha na kuongeza jengo jingine ili kutoa huduma zote kwa wakati mmoja,” alisisitiza.
IMETOLEWA NA
OFISI YA WAZIRI MKUU
JUMAMOSI, JANUARI 7, 2017.
Hakuna maoni :
Chapisha Maoni