Wimbo wa taifa ukiimbwa. |
Na Dotto Mwaibale
WANAFUNZI nchini wametakiwa kuacha kujiingiza katika makundi yasiofaa ili kujiepusha na kujihusisha na dawa la kulevya.
Mwito huo umetolewa na Mkuu wa Chuo cha Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA) cha Jeshi la Kujenga Taifa (JKT), Mgulani, Meja Haule wakati akifunga mafunzo ya ukakamavu kwa wanafunzi wa kidato cha kwanza wa Shule ya Sekondari ya Jitegemee Dar es Salaam leo.
“Wanafunzi acheni kujihusisha na makundi yasiofaa ili kujiepusha kuingia katika vishawishi vya matumizi ya dawa za kulevya” alisema Meja Haule.
Aliwataka wanafunzi hao kutumia muda wao wote kwa kusoma ili kutimiza ndoto za maisha yao kwa kupata elimu bora.
Meja Haule aliwataka wanafunzi wa kike kujiepusha na tamaa mbalimbali kwani wao wapo katika hatari ya kupata vishawishi na aliwataka kujifunza kwa wanawake waliofanikiwa na kufanya vizuri kwa kuwa viongozi katika taifa.
Haule aliziomba shule zilizopo chini ya jeshi kuiga mfano wa shule ya Jitegemee ya kutoa mafunzo hayo ya ukakamavu kwani yanawafanya wanafunzi hao kuwa wazalendo wa nchi yao.
Makamu Mkuu wa Shule Utawala Kepteni Benitho Lubida alisema wanafunzi waliopata mafunzo hayo ni 604 na walitumia wiki tatu kufuzu.
Alisema mafunzo hayo yamelenga kuwajengea uwezo wanafunzi hao wa kujitegemea, kuwafanya wawe na nidhamu, kujiamini, kuwa wavumilivu na kujiamini.
Aliwaomba wazazi wa wanafunzi hao kuwa wa kwanza kutoa mafunzo mbalimbali kwa watoto wao ili kuwajenga katika misingi mizuri kuanzia ngazi ya familia.
(Imeandaliwa na mtandao wa www.habari za jamii.com-simu namba 0712-727062)
Hakuna maoni :
Chapisha Maoni