.

.

.

.

.

.

.

.
KARIBUNI TUHABARIKE, TUELIMISHANE, TUPEANE HABARI ZA KUKUFANYA UTABASAMU KIDOGO NA MATUKIO YALIYOFANYIWA UCHUNGUZI WA KINA TOKA KILA PEMBE CONTACTS: +255 787 377 722 Email: drweyunga@gmail.com PIA UNAWEZA KUNI FOLLOW KUPITIA INSTAGRAM YANGU @drweyunga | TANGAZA NASI ILI UWAFIKIE WATU WENGI ZAIDI.

Jumatatu, 27 Februari 2017

SAMANI ZA NDANI ZAMNG’ARISHA JACQUELINE NTUYABALIWE KWENYE FORBES

KATIKATI ya foleni katika jiji la Dar es Salaam ndani ya gari nyeupe aina ya Mercedes S550, Jacqueline Ntuyabaliwe, mrembo wa miaka 38, macho yake yalikuwa yametulia katika simu yake ya mkononi.

Alikuwa akiangalia seti ya samani za eneo la kulia chakula. Kwa bashasha, baada ya muda kidogo anatanua picha hiyo kisha ananisogezea simu yake ya mkononi kunionesha picha anayoiangalia.

“Hii ni moja ya samani tulizonazo,” anasema huku akinionesha seti hiyo ambayo imetengenezwa na Molocaho by Amorette, kampuni ya kutengeneza samani aliyoianzisha hivi karibuni.

“Samani hizi zimetengenezwa kutokana na mbao zilizotwaliwa kutoka katika mashua za zamani za mizigo kwenye fukwe za Tanzania upande wa bahari ya Hindi,” anasema mjasiriamali huyo.

Samani hizo za eneo la kulia chakula (Dining Table) anasema zimeagizwa na familia moja iliyopo Ulaya ambayo siku za karibuni ilitembelea duka lake (showroom) Dar es Salaam wakati wakiwa likizo na kwamba anajiandaa sasa kuisafirisha seti hiyo ya samani kwa wateja wake wapya wa Ulaya.

Lakini kwanza alichokuwa anakifanya kwa siku ile ni kwenda kiwandani kuangalia seti hiyo ya samani kwa mara ya mwisho kabla ya kusafirishwa ili kujihakikishia kwamba imemaliziwa urembeshaji kwa namna inavyotakiwa kuwa.
                                                                          Jacqueline Ntuyabaliwe Mengi.

Jacqueline Ntuyabaliwe, anayetaka umaridadi uliokamilika, ni binti ambaye huangalia vitu vidogo vidogo kuona kama vipo sawa katika hali inayokubalika viwe.

Pamoja na kuwa na ratiba yenye changamoto sana (Yeye ni Balozi wa WildAid na yumo ndani ya bodi kadhaa; mama wa watoto pacha wavulana; mke kwa mfanyabiashara mwenye mafanikio makubwa na akiendesha taasisi ya hisani ya elimu), Ntuyabaliwe huhakikisha anakagua kila samani inayozalishwa kiwandani kwake kabla ya kuuzwa au kusafirishwa.

“Napenda kitu bora chenye uhakika!” anasema mlimbwende huyo wa zamani wa Tanzania ambaye pia ni mwanamuziki.

“Kila kitu tunachokifanya Molocaho lazima kiwe chenye uhakika hakina makosa wala dhaifu, lazima kiwe kimetulia,” anasema mrembo huyo.

“Tunashindana na watu maarufu duniani wanaofanya vyema kwa hiyo kama sisi tusipofanya vyema kuliko wao tutashindwa,” aliongeza.
                                                                                           The Crown Chair by Molocaho

Ntuyabaliwe, mzaliwa wa Tanzania, aliyefunzwa kubuni uzuri wa ndani, ni mwanzilishi na mbunifu mkuu wa Molocaho by Amorette, kampuni ya Tanzania inayojishughulisha na utengenezaji wa samani bora kwa namna mteja anavyohitaji, samani, nyuzi, taa, urembaji, samani za nje na kwenye bustani.

Molocaho inatengeneza samani zenye mahadhi ya kiafrika ikichanganya utamaduni wa Tanzania katika mazingira ya kisasa na kumalizia na ubunifu wa kimataifa.

Molocaho, moja ya makampuni ya Afrika Mashariki ya samani yanayokua kwa kasi, imejipatia nafasi kubwa ya heshima kwa kuhakikisha kwamba inatumia mali ghafi na mbao njema pekee za Tanzania kutengeneza samani zenye kwenda kimataifa.

“Mpango wetu mkubwa ni kujenga nembo ya biashara ya samani za Tanzania inayotambulika kimataifa.

Ni dhahiri itatuchukua muda kufikia huko , lakini tumedhamiria,” alisema wakati tukizunguka naye katika duka kubwa la maonesho la Molocaho lililopo eneo la Masaki jijini Dar es Salaam.

Ntuyabaliwe ni mojawapo ya watu wanaotambulika kirahisi kabisa nchini Tanzania. Mwaka 2000 alishinda taji la urembo la Miss Tanzania na kuiwakilisha Tanzania katika shindano la ulimbwende la dunia ( Miss World). Baada ya muda alipata heshima ya kuwa mmoja wa wanamuziki mahiri na kuweza kutoa nyimbo kadhaa zilizoshika chati Afrika Mashariki.

Pamoja na kuwa mlimbwende na mwanamuziki anasema mapenzi yake makubwa ni ubunifu wa uzuri wa ndani wa nyumba.

“Mimi ni mbunifu kutoka moyoni,” anasema.

“Kwa namna ninavyokumbuka, mimi ninavutiwa na ubunifu wa ndani na wa samani, sanaa na fasheni na nimekuwa mwanafunzi bora kabisa wa masuala ya ubunifu na historia yake. Kama mtoto mara zote nilikuwa nachora vitu mbalimbali. Ni mojawapo ya vitu ninavyovifanya kwa raha kubwa.”

Wakati muziki wake unakamata chati akajiona amekinai na hivyo kuingia katika awamu nyingine ya maisha yake.
Alitoka na kwenda shule Uingereza. Huko alienda kujifunza ubunifu wa ndani na lengo kubwa ni kuboresha weledi katika hilo na mwaka 2012 alianzisha kampuni ya Amorette, yenye makao makuu Dar es Salaam iliyokuwa inajishughulisha na masuala ya urembaji wa ndani.

Amorette imepata mafanikio makubwa na Ntuyabaliwe amekuwa akifanya kazi na watu wengine wenye kaliba ya juu katika masuala ya ubunifu wawe binafsi au makamapuni ya kimataifa nchini Tanzania, akichanganya mawazo na ubunifu wao kutengeneza bidhaa zenye kaliba ya juu katika ubunifu, staili, rangi ili wateja wake wawe na maisha mazuri ama majumbani mwao au katika mazingira yao ya kazi.

Na katika muda wote wa kufanya hayo, mjasiriamali huyu alikuwa na tabia ya kuchora muonekano wa samani.

“Napenda samani , sijui kwanini labda kwa sababu ya kazi yangu ya ubunifu wa maeneo ya ndani, lakini nadhani ni kwa kuwa naamini samani zako zinakuonesha wewe ni mtu wa namna gani. Awali nilitengeneza michoro ya samani kwa ajili ya kujenga ubunifu tu, lakini mara nyingi mume wangu huangalia michoro hiyo na kunipongeza. Alikuwa akisema kwamba situmii vyema kipaji changu. Mara nyingi amekuwa akinihimiza kujikita katika usanii na kuanzisha kampuni ya kushughulika nao,” anasema Ntuyabaliwe akikumbuka alivyoanza.

Mume wake, Dkt.Reginald Mengi, ni tajiri mwenye mafanikio makubwa nchini Tanzania ambaye ameujenga utajiri wake kwa kufanya karibu kila kitu kuanzia uzalishaji wa kinywaji cha Coca-Cola hadi uchimbaji wa madini na kumiliki vituo vya televisheni na magazeti.

“Ukiwa na mume mwenye mafanikio makubwa namna hii, unashawishika kusaka mafanikio. Kwa hiyo nikatengeneza mpango biashara, kuanza kuajiri wafanyakazi na hivyo kuiweka hai ndoto yangu.”

Amorette, ikiwa ni chata yenye mafanikio makubwa miongoni mwa watu wa daraja la juu nchini Tanzania na huku ikipanda kwa kasi na watu wakiifuata, Septemba 2016 Ntuyabaliwe alizindua Molocaho by Amorette kama kampuni ya kubuni na kutengeneza samani. Miezi michache tu tangu kuundwa kwake kampuni imefanya vyema na inaonekana kunedelea kukua kimafanikio.

“Tumekuwa katika pilikapilika sana,” anasema na kuongeza: ” Sikuwa natarajia kufanya biashara kama tulivyofanya katika miezi michache iliyopita.”

Ntuyabaliwe ndiye mbunifu mkuu wa Molocaho. Akitumia ufundi wa asili katika mazingira ya sasa, Ntuyabaliwe hubuni na kutengeneza samani za kuvutia kwa ajili ya majumbani na maofisini na hata kwa watu binafsi.

Ukiangalia samani za Molocaho utabaini uzuri wake kusukwa kwa namna rahisi lakini yenye hisia kali na hivyo kufanya ubunifu wake kuwa wa bashasha , uliotulia na wenye kutuliza kiu. Lakini ukiangalia kwa karibu zaidi utabaini kwamba kile unachokiona rahisi ni tata, kimeumbwa kwa namna ambayo ni makini na yenye ugumu wa aina yake kwa lengo la kukupatia kitu bora kabisa.
Hivyo ndivyo Ntuyabaliwe anavyotaka unapoangalia samani zake yaani unaziona za kawaida lakini zenye uzuri na ubora wa hali ya juu.

Kwa Ntuyabaliwe,ubunifu wa samani za Molocaho unatokana na wakati mwingine na mambo ambayo hukuyatarajia kabisa. Wakati mwingine tukio asili linaweza kabisa kusababisha ubunifu wa aina Fulani.

Mathalani tukio la radi (mwale na mlipuko) ndio uliotengeneza kiti kinachoitwa radi ambacho kimefanya vyema katika mauzo ya ndani na nje.

Katika kiti hiki sehemu ya kuegemea kuna mwale wa radi.

Molacaho hutengeneza vitu kwa namna ambavyo mteja anataka na maana yake kazi zake nyingi ni za oda.

“Wateja wetu huangalia kitabu chetu cha aina mbalimbali za samani kisha wanachagua wanachotaka na kutueleza kitu gani cha ziada wanataka kiwepo. Na hapa huwa tunafanya mazungumzo na wateja wetu ili tuweze kufahamu hasa wanachofikiria na wanachohitaji,” anasema Ntuyabaliwe.

Samani zinazotengenezwa kutokana na maagizo kwa kawaida ni gharama kwa kuwa hutengenezwa kwa mahitaji ya mteja.

Ntuyabaliwe anakiri kwamba Watanzania wengi hawana uwezo wa kununua bidhaa zake. Wengi wa watanzania ni maskini; Bidhaa za Molacaho zinaanzia kokote kule kuanzia dola za Marekani 250 kama stuli hadi dola za Marekani 6,000 kwa kitanda.

“Bidhaa zetu zimepambanua wateja,” anasema na kuongeza kwamba wao si rahisi lakini pia si ghali sana.

“kazi zetu si rahisi sana na wala si ghali sana hapa mjini. Mwishoni wa siku huwa tunapata taarifa kutoka kwa wateja wetu kwamba tuna bei nzuri kulinganisha na bidhaa tunazotengeneza.”

Wakati Ntuyabaliwe anatengeneza fedha amesema pia anatengeneza mfumo wa kuwaendeleza mafundi nchini Tanzania. Mapema mwaka huu, Amorette, kampuni yake inayoshughulika na ubunifu wa masuala ya ndani ilianzisha programu ya kusimamia mafunzo kwa mafundi wa hapa Tanzania.

Lengo kuu ni kuwafanya mafundi wa Tanzania kufikia uwezo wa kubuni na kutengeneza bidhaa zenye hadhi ya kimataifa.

Chini ya programu hii, mafundi ambao tayari wana ujuzi na kufanya shughuli za useremala au kitu kinachofanana na hicho wanapewa mafunzo ya miezi miwili na mafundi wanaotambulika kimataifa.

Nia ni kuhamisha maarifa, ujuzi na teknolojia kutoka kwa wataalamu hao wa kimataifa na kuwawezesha watanzania kubadilika katika utendaji.

Molocaho pia wamejikita katika kuhifadhi mazingira kwa kuhakikisha kwamba hakuna wanachotupa kinachotokana na mchakato wa kutengeneza samani.

Kampuni hii hutumia bidhaa za mbao kutoka katika vyanzo mbalimbali na pia inaunga mkono kampeni mbalimbali za upandaji miti nchini Tanzania.

“Mwishoni mwa siku biashara si tu iwe inayoleta faida lakini pia lazima ijali maslahi ya jamii ambapo biashara hiyo ipo,” anasema.

Leo hii, Molocaho imeajiri zaidi ya wafanyakazi wa kudumu 30 huku wakiwa katika njia nzuri ya kutengeneza faida katika kipindi cha mwaka mmoja tu tangu kuanzishwa kwake.

“Hakika tumeanza,” anasema Ntuyabaliwe wakati tunaondoka katika duka la Molocaho. “Tutaendelea kumkuza mtoto huyu ili siku moja awe kampuni kubwa. Wewe tufuatilie tu”

Imeandikwa na Mfonobong Nsehe , wa Forbes na kutafsiriwa kwa wasomaji wa Kiswahili na Mzige Media kupitia TheBeauty.co.tz

Hakuna maoni :

Chapisha Maoni