WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema Serikali imepanga kujenga uwanja wa ndege wa kimataifa katika eneo la Ngungungu – Mamire wilayani Babati, mkoani Manyara ili uweze kurahisisha mawasiliano kwa mikoa mitano inayozunguka mkoa huo.
Ametoa ahadi hiyo leo mchana (Jumatano, Februari 22, 2017) wakati akizungumza na watumishi na viongozi mbalimbali wa mkoa huo kwenye kikao cha majumuisho ya ziara yake ya siku sita mkoani Manyara.
Waziri Mkuu amesema upembuzi yakinifu ili kubaini gharama za ujenzi wa uwanja huo utafanyika mwaka 2019 na ujenzi halisi utaanza katika bajeti ya mwaka 2020/2021.
“Tumechagua eneo la Ngungungu-Mamire kwa sababu liko karibu na mbuga za wanyama; lakini pia tuna hospitali yetu kule Haydom ili kama kuna mgonjwa amezidiwa iwe rahisi kumpakia na kumpeleka kwenye hospitali za rufaa.”
“Tumechagua eneo lile ili liwe ni eneo la kupumulia la Makao Makuu ya nchi Dodoma. Ikitokea kule kumejaa, itakuwa ni rahisi kwa ndege kutua hapa Babati na mtu anasafiri kwa gari na ndani ya muda mfupi atajikuta yuko Dodoma,” aliongeza.
Tanzania (TANESCO) walioko kwenye wilaya za mkoa huo waache kukaa ofisini na badala yake waende vijijini ili kuwahamasisha wananchi na kuchukua malipo yao stahiki.
“TANESCO wekeni mpango wa kuwafuata wananchi huko vijijini kwa ajili ya kuwaandikisha na kuchukua malipo stahili. Ni rahisi kwenu kwenda na polisi wa kuwalinda kuliko kumsubiri mwananchi mmoja aje hadi mjini kulipia sh. 27,000. Tena yeye anaweza kutumia hadi sh. 40,000/- akiweka nauli na chakula,” ameonya.
Wakati huohuo, Waziri Mkuu amewataka waku wa idara na wakurugenzi wa halmashauri nchini wafanye kazi kwa ukaribu na vyombo vya habari ili taarifa za kazi wanazozifanya ziweze kuwafikia wananchi kwa haraka.
“Kwenye baadhi ya wilaya kuna redio na televisheni ambazo zinaendeshwa na Halmashauri au na watu binafsi. Ni rahisi kupata nafasi ya kurusha mambo yenu mkifanyanao kazi kwa karibu.”
“Wakuu wa idara nendeni studio mkaelezee mafanikio yaliyopatikana katika wilaya zenu na mkoa wenu kwa ujumla,” ameongeza.
Akitoa shukrani kwa niaba ya viongozi na watendaji wa mkoa huo, Mbunge wa Hanang, Bibi Mary Nagu amesema anaishukuru Serikali kwa jitihada zinazofanywa kuuendeleza mkoa huo na kwamba wana imani kuwa wataweza kuuzidi mkoa wa Arusha ambao uliizaa Manyara.
“Tunakushukuru kwa kutembelea mkoa wetu na kuona hali ya maendeleo ilivyo pamoja na changamoto zinazotukabili. Ninaamini maelekezo uliyoyatoa hapa, yataongeza ari na kuwafanya watumishi wa mkoa huu wajiamini zaidi, na sisi tumepata faraja uliposema tuko sawasawa kiutendaji,” amesema.
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
JUMATANO, FEBRUARI 22, 2017.
Hakuna maoni :
Chapisha Maoni