Dk. Robert Mhina (kulia) kutoka Taasisi ya Mifupa Tanzania (MOI) , akishiriki mafunzo ya utoaji huduma kwa majeruhi wa ajali kwa njia ya video yaliyoratibiwa na kufanyika kwa njia ya video kwenye kumbi za Wakala ya Mafunzo kwa Njia ya Mtandao, yakijumuisha nchi za Tanzania, Marekani, Pakistani na Brazil . Kushoto ni Dk.Lukwinyo na Dk.Mbaruku Mlinga.
Madaktari wa Tiba ya Mifupa wakishiriki mafunzo hayo. Kutoka kushoto ni Dk.Hamid Masoud, Dk.Valentine Restus na Dk. Joseph Msemwa.
Na Dotto Mwaibale
UMOJA wa Madaktari Bingwa wa Mifupa Duniani (SICOT) ikishirikiana na Wakala ya Mafunzo kwa Njia ya Mtandao (TaGLA), umetoa elimu ya kutoa huduma kwa majeruhi wa ajali kwa njia ya mtandao wa mafunzo kwa njia ya video.
Umoja huo ulitoa elimu hiyo kwa kushirikiana na Madaktari Bingwa na wataalamu wa Mifupa kutoka nchi za Tanzania, Marekani, Pakistani na Brazil.
Akizungumza mara baada ya mafunzo hayo akiwa TaGLA, Dar es Salaam, Mratibu wa Umoja huo hapa nchini, Dk. Robert Mhina alisema kupitia mafunzo haya wameweza kujadili mambo mbalimbali yahusuyo ajali za barabarani.
“Huwa tunajadili mada mbalimbali kama ajali za barabarani kwa kubadilishana uzoefu na Madaktari wa nchi nyingine kwa kutumia mtandao wa mafunzo kwa njia ya video, na wakati wote huwa tunazungumza na nchi kutoka mabara mengine ili kubadilishana uzoefu,”alisema.
Alisema madaktari hao huwa wanakubaliana katika kujadili mada na kujadili kuhusu mambo muhimu yanayohusu tiba ya mifupa huku wakipeana majukumu.
“Kupitia vikao hivi hutusaidia sana hata kwa wale wanafunzi wanaojifunza Ubingwa kuona kitu gani kinaendelea duniani, bila gharama za kusafiri nje ya nchi” alisema Dk Mhina.
Alisema tayari Umoja huu inaangalia uwezekano wa kutoa nafasi kwa wanafunzi kutembela vituo kingine katika nchi hizo ili kuona na kuongeza uzoefu zaidi.
“Mwaka huu kuna vikao kama sita hivi, kikao hiki ni mwazo tu,”alisema na kuongeza kuwa kupitia mkutano huo itawasaidia wananchi kwa kuboreshewa ufanyaji wa tiba sahihi za mifupa hivyo kupata huduma za matibabu zilizoboreshwa kutokana na ajali za barabarani.
Watoa mada katika mkutano huo uliofanyika kwa njia ya video walikuwa ni pamoja na Dk. Syed M. Avais wa King Edward Medical University, Dk. Robert D. Zura wa Louisiana State University Health Science Center na Dk. Robert I. Mhina, wa Taasisi ya Mifupa Tanzania (MOI) kutoka nchini Tanzania.
(Imeandaliwa na mtandao wa www.habari za jamii.com-simu namba 0712-727062)
Hakuna maoni :
Chapisha Maoni