Wajumbe wa mkutano wa Mabadiliko ya tabia ya nchi na athari zake kiuchumi hapa nchini uliokishirikisha Chuo cha Mipango ya Maendeleo Vijijini –Dodoma na Jumuiya ya Umoja wa Ulaya (EU), wakiingia kwenye ukumbi wa Mikutano mmoja Jijini Dar es salaam, siku ya kwanza ya mkutano huo wa Siku mbili.
Mwenyekiti wa Baraza la Uongozi wa Chuo cha Mipango ya Maendeleo vijijini – Dodoma, Prof. Razack Lokina (kulia) akifafanua jambo wakati wa mkutano uliohusu changamoto za mabadiliko ya tabia ya nchi wakati wa mkutano uliowashirikisha wadau wa maendeleo kutoka ndani nan je ya nchi na kuandaliwa na Chuo cha Mipango ya Maendeleo Vijijini-Dodoma.
Mmoja wa washiriki wa mkutano huo akichangia mada mbalimbali kuhusu mabadiliko ya tabia ya nchi yanavyoathiri uchumi wa wananchi vijijini nchini Tanzania, zilizowasilishwa kwenye mkutano ulioandaliwa na Chuo cha Mipango ya Maendeleo Vijijini-Dodoma, na kufanyika Jijini Dar es salaam.
Baadhi ya wadau wa mkutano uliohusu changamoto za athari za uharibifu wa mazingira na mabadiliko ya tabia ya nchi wakifuatilia kwa makini mjadala kuhusu suala hilo, Jijini Dar es Salaam.
Mwenyekiti wa Baraza la Uongozi wa Chuo cha Mipango ya Maendeleo vijijini – Dodoma, Prof. Razack Lokina (kushoto) na Mkuu wa Chuo hicho Dkt. Frank Hawassi (kulia) wakiwa katika picha ya pamoja nje ya ukumbi wa mkutano kuhusu Mabadiliko ya Tania Nchi uliowashirikisha wadau kutoka ndani na nje ya nchi uliofanyika Jijini Dar es Salaam.
Mkuu wa Chuo cha Mipango ya Maendeleo vijijini – Dodoma Dkt. Frank Hawassi akizungumza na wajumbe wa Taasisi na Washirika wa Maendeleo kuhusu, umuhimu wa kuunganisha nguvu katika kupambana na mabadiliko ya Tabia nchi, katika Mkutano wa Mabadiliko ya Tabia nchi jijini Dar es salaam.
Na Benny Mwaipaja,WFM
Wadau wanaofanya tafiti mbalimbali za Maendeleo ya uchumi nchini hasa maeneo ya vijijini kuhusu Mabadiliko ya Tabia nchi wametakiwa kuwasilisha matokeo ya tafiti hizo Serikalini na katika Mashirika mengine ya Maendeleo ili matokeo yake yafanyiwe kazi na kusudio la tafiti hizo liweze kufikiwa.
Rai hiyo imetolewa Jijini Dar es salaam na Mwenyekiti wa Baraza la Uongozi wa Chuo cha Mipango ya Maendeleo vijijini – Dodoma, Prof. Razack Lokina wakati wa Mkutano uliohusu mabadiliko ya tabia nchi na athari zake kiuchumi uliozihusisha Taasisi za Serikali na Binafsi pamoja na Washirika wa Maendeleo.
Amesema Chuo cha Mipango kimekuwa kikifanya kazi zake vijijini, zikiwemo za tafiti mbalimbali na matokeo hayo huwasilishwa katika ngazi husika ikiwemo Ofisi ya Makamu wa Rais inayoshughulikia mazingira pamoja na Wizara ya Maliasili na Utalii ili kutumia matokeo hayo kwa manufaa ya maendeleo ya jamii hasa vijijini.
“Mkutano wa Mabadiliko ya Tabia nchi ambao umejadili mbinu mbalimbali za kukabiliana na athari za kiuchumi zinazotokana na Mabadiliko hayo, umetokana na andiko la Wanafunzi wa Chuo hicho waliokwenda katika mafunzo kwa vitendo vijijini na kushuhudia namna mabadiliko ya tabia nchi yalivyoathiri maendeleo ya wananchi”. Alifafanua Prof. Lokina
Tayari Chuo kina mradi ujulikanao kama Chololo Ecovillage unaofadhiliwa na Umoja wa Ulaya (EU) Mkoani Dodoma, ambao huwafundisha wanakijiji njia bora za uzalishaji mali, hivyo kuwafanya baadhi ya Wananchi waliokuwa wanakosa chakula, kutokana na hali ya Ukame wa Mkoa huo kuanza kupata mazao ya kutosha na kuongeza pato lao.
Naye Mkuu wa Chuo hicho cha Mipango ya Maendeleo vijijini- Dodoma, Dkt. Frank Hawassi, amezitaka Taasisi na Mashirika ya umma na Binafsi kuunganisha nguvu katika kukabiliana na Mabadiliko ya Tabia nchi kwa kuwa kama juhudi hazitachukuliwa athari zake zitampata kila mmoja.
Aidha, amesema hakuna nchi inayoweza kufanikiwa kukabiliana na tatizo hilo bila kushirikiana hata kama nchi hiyo imeendelea kwa kiasi kikubwa. Pia Jamii inapaswa kujua kuwa hata matatizo ya wafugaji, wakulima na wengine kuhusu ardhi ni matokeo ya athari za Mabadiliko ya Tabia nchi, hivyo kila mmoja anatakiwa kuwa chachu ya utunzaji wa mazingira, ili maendeleo yanayopatikana yawe endelevu.
Ameongeza kuwa Chuo cha Mipango Dodoma kinatoa nafasi kwa wadau kote nchini kukitumia kikamilifu katika kutatua changamoto za kimazingira kwa kuwa ipo Idara iliyo na jukumu la kushughulikia suala la Mazingira na Mabadiliko ya Tabia nchi.
Kwa upande wake aliyekuwa Balozi wa Umoja wa ulaya nchini Tanzania Tim Clarke, ambaye ameongoza timu ya washirika wa Maendeleo katika Mkutano huo ameitaka Serikali kupitia Wizara ya Nishati na Madini kujitahidi kuwahamasisha wananchi kutumia Nishati mbadala ikiwemo Gesi ili kupunguza kasi ya uharibifu wa misitu kwa kukata miti kwa ajili ya kupata Mkaa.
Vilevile ametoa rai kwa Serikali kuwa karibu na jamii na kuwaelimisha kuhusu kutunza mazingira katika shughuli zao za kila siku za kujipatia kipato ili kusaidia kulinda mazingira ya asili yatakayochochea kukua kwa uchumi wa mtu mmoja mmoja na Taifa kwa ujumla.
Hakuna maoni :
Chapisha Maoni