Kamati ya Bodi ya Uendeshaji na Usimamizi wa Ligi za Tanzania (Kamati ya Saa 72), imemwondoa Mwamuzi wa kati, Ahmada Simba katika orodha wa waamuzi watakaochezesha mechi za Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara msimu huu wa 2016/2017.
Hatua hii imefikiwa baada ya utetezi wa Mwamuzi Simba kudai kwamba hakuona tukio la Mchezaji wa Young African, Obrey Chirwa ambaye alifunga bao ambalo hata hivyo, mwamuzi alilikataa na kumwonya mchezaji kwa kadi njano.
Tukio hilo lilitokea katika mchezo ambao Young Africans walikuwa wageni wa Ruvu Shooting kwenye Uwanja wa Taifa, Machi mosi, mwaka huu.
Katika hiyo ya njano ilikuwa ni ya kwanza kwa Chirwa ambayo hata hivyo kamati ya Saa 72 imeifuta kadi hiyo kwa mujibu wa kanuni ya 9 (8) baada ya Kamati ya Saa 72 haikupaswa kutolewa kwa Chirwa kwa sababu hakukuwa na kosa wala mazingira ya kuonywa.
Kadi hiyo ilikuwa ni msingi wa kadi nyekundu baada ya Chirwa kufanya faulo ambayo aliadhibiwa tena kwa kadi ya njano hivyo kutolewa nje kwa mujibu wa taratibu.
Kufutwa kwa kadi ya njano ya kwanza, kunapelekea kufutwa kwa kadi nyekundu ambayo msingi wa kadi hiyo ulisababisha kadi nyekundu hivyo mchezaji angempaswa kukosa mchezo mmoja. Hata hivyo, kadi ya pili ya njano inahesabiwa.
Kadhalika uamuzi mwingine ulikuwa ni kuipiga faini Young Africans iliyocheza na Simba Februari 25, 2017 kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam baada ya Wanajwani hao kuingia uwanjani kwa kutumia mlango usio rasmi.
Kitendo hicho ni kwenda kinyume cha kanuni ya 14 (14) ya Ligi Kuu inayoelekeza kuwa timu zitaingia uwanjani kwa kutumia milango rasmi. Hivyo kwa kuzingatia Kanuni ya 14 (48) ya Ligi Kuu, Kamati imeipiga Young Africans fainali ya Sh 500,000 (lakini tano).
ROBO FAINALI ASFC SIMBA KUCHEZA MACHI 19, 2017
Mechi mbili za kwanza hatua ya Robo Fainali ya Kombe la Shirikisho Azam (Azam Sports Federation Cup 2016/2017), zitachezwa Machi 18 na 19, mwaka huu kwenye viwanja viwili tofauti.
Mechi hizo ni kati ya Kagera Sugar itakayocheza na Mbao FC ya Mwanza kwenye Uwanja wa Kaitaba, mjini Bukoba mkoani Kagera wakati siku inayofuata Machi 19 Simba itacheza na Madini kwenye Uwanja wa Sheikh Amri Abeid jijini Arusha.
Awali Simba ilikuwa icheze Machi 18, mwaka huu, lakini siku hiyo uwanja huo utakuwa na shughuli za kijamii hivyo sasa utachezwa siku ya Jumapili Machi 19, mwaka huu.
Mechi nyingine zitapangiwa tarehe za baadaye. Mechi hizo ni kati ya Azam FC na Ndanda FC kadhalika Tanzania Prisons ya Mbeya itakayocheza na mshindi kati ya Young Africans ya Dar es Salaam na Kiluvya United ya Pwani.
Bingwa wa michuano hiyo kwa mujibu wa kanuni, atazawadiwa Tsh. 50 milioni.
Pia bingwa wa michuano hiyo, ndiye atakayeiwakilisha nchi kwenye michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika ya Total wakati Bingwa wa Ligi Kuu Tanzania Bara ndiye ataiwakilisha nchi kwenye michuano ya Total Ligi ya Mabingwa Afrika.
MAANDALIZI YA MICHEZO YA YOUNG AFRICANS v ZANACO NA AZAM FC v MBABANE
Maandalizi yote kwa michezo miwili ya kimataifa, yamekamilika.
Michezo hiyo ni kati ya Young Africans ya Tanzania na Zanaco ya Zambia utakaochezwa Jumapili kuwania taji la Ligi ya Mabingwa Afrika pia Azam FC ya Tanzania na Mbabane Swalows ya Swaziland kuwania Kombe la Shirikisho barani Afrika.
Kwa upande wa Young Africans dhidi ya Zanaco, mchezo huo utafanyika Jumamosi Machi 11, mwaka huu. Waamuzi kutoka Djibouti ndio watakaochezesha mechi hiyo.
Waamuzi hao ni Djamal Aden Abdi ambaye atapuliza kipenga wakati wasaidizi wake ni Hassan Yacin na Farhan Salime ilihali mwamuzi wa akiba atakuwa Souleiman Djamal. Kamisha katika mchezo huo Na. 61 atakuwa Luleseged Asfaw kutoka Ethiopia.
Kiingilio katika mchezo huo kwa mujibu wa Mratibu wa Mechi za Kimataifa wa Young Africans, Mike Mike ni Sh 20,000 kwa VIP ‘A’, Sh 10,000 kwa VIP ‘B’ na ‘C’ na Mzunguko (Viti vya Rangi ya chungwa, kijani na bluu) ni Sh 3,000.
Azam wao watacheza Jumapili Machi 12, mwaka huu na Mbabane Swallows ya Swaziland kwenye Uwanja wa Azam ulioko Chamazi, Dar es Salaam.
Waamuzi watakochezesha mchezo huo wanatoka Benin ambao ni Mwamuzi wa kati, Addissa Abdul Ligali na wasaidizi ni Medegnonwa Romains Agbodjogbe na Babadjide Bienvenu Dina huku Mwamuzi wa akiba akiwa Moumouni Kiagou na kamisha wa mchezo atakuwa Mohamed Omar Yusud wa Kenya.
Kiingilio katika mchezo huo kwa mujibu wa Mtendaji Mkuu wa Azam FC, Saad Kawemba ni Sh 10,000 kwa VIP, Jukwa Kuu itakuwa ni Sh 5,000 na Mzunguko itakuwa ni Sh 3,000.
Wakati huohuo, tiketi za waamuzi wa Tanzania walioteuliwa na Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF), kuchezesha mechi ya Ligi ya Mabingwa Afrika kati ya timu za AS Porto Louis 2000 ya Mauritius na El Hilal ya Sudan wikiendi ijayo, wamepata tiketi zao za kusafiri.
Katika mchezo huo ambao utafanyika ama Machi 17, 18 au 19 Mwamuzi wa kati atakuwa Israel Mujuni Nkongo wakati wasaidizi wake watakuwa ni Samuel Hudson Mpenzu na Josephat Deu Bulali huku Mwamuzi wa akiba akiwa ni Hery Sasii. Kamisha katika mchezo huo Na. 78 atakuwa Jerome Kelvyn Damon kutoka Afrika Kusini.
IMETOLEWA NA SHIRIKISHO LA MPIRA WA MIGUU TANZANIA (TFF)
Hakuna maoni :
Chapisha Maoni