.

.

.

.

.

.

.

.
KARIBUNI TUHABARIKE, TUELIMISHANE, TUPEANE HABARI ZA KUKUFANYA UTABASAMU KIDOGO NA MATUKIO YALIYOFANYIWA UCHUNGUZI WA KINA TOKA KILA PEMBE CONTACTS: +255 787 377 722 Email: drweyunga@gmail.com PIA UNAWEZA KUNI FOLLOW KUPITIA INSTAGRAM YANGU @drweyunga | TANGAZA NASI ILI UWAFIKIE WATU WENGI ZAIDI.

Ijumaa, 3 Machi 2017

OPERESHENI YA VIROBA YAENDELEA JIJINI DAR ES SALAAM

Na: Lilian Lundo – MAELEZO
 

Serikali inaendelea na operesheni ya kukagua viwanda vinavyotengeneza pombe zilizo kwenye vifungashio vya mifuko ya plastiki maarufu kama “viroba” ili kujiridhisha kama viwanda hivyo vimesitisha uzalishaji wa pombe hizo pamoja na kuzuia utokaji wa pombe ambazo bado zipo katika maghala.
 

Hayo yamesemwa na Mwanasheria wa Baraza la Taifa la Usimamizi wa Mazingira (NEMC) Manchale Heche alipokuwa akiongea na waandishi wa habari wakati wa operesheni hiyo ambayo inaendelea Jijini Dar es Salaam.
 

“Zoezi linaendelea kama lilivyoanza jana ambapo tunakagua viwanda vinavyozalisha viroba, na mpaka sasa tumeshatembelea viwanda vitatu ambavyo ni kiwanda cha Kibo Spirit kinachotengeneza pombe ya kiroba aina ya Double Panch, Kiwanda che Blue Nile kinachotengeneza viroba vya Kitoko na Rivella pamoja na kiwanda cha True Bell kinachotengeneza viroba vya Bonanza na Suke,” alifafanua Heche.
 

Aliendelea kwa kusema kuwa lengo la operesheni ni kukagua viwanda vyote vinavyozalisha pombe aina ya viroba ili kujiridhisha ikiwa viwanda hivyo vimetekeleza agizo la Serikali la kusimamisha uzalishaji wa pombe hizo kuanzia Machi 01, mwaka huu.
 

Heche amesema kuwa operesheni hiyo pia inahusisha ukaguzi kutambua idadi ya pombe zilizobaki katika maghala mbalimbali na kuzuia pombe hizo kutotolewa katika maghala hayo mpaka hapo Serikali itakapotoa agizo ya namna ya kuziharibu pombe hizo.
 

Aidha amesema kuwa agizo limetoka katika mipaka yote ya nchi kuzuia uingizaji wa pombe hizo na kuzirudisha nchi zilizotoka kwa gharama za muhusika aliyesafirisha pombe hizo.
 

Kwa upande wake Meneja Uendeshaji wa Kiwanda cha True Bell (T) Limited kilichopo Shekilango, Godwin Mungere amesema kuwa kiwanda hicho bado kilikuwa katika majaribio lakini kutokana na agizo la Serikali wamesitisha uzalishaji wa pombe za viroba ambapo wao walikuwa wakizalisha viroba aina ya Bonanza na Suke.
 

Ameeleza kuwa akiba ya pombe za viroba vilivyobaki katika ghala lao ni katoni 166 za viroba vya Bonanza na katoni 165 za viroba vya Suke ambapo wanasubiri maelekezo kutoka Serikalini namna ya kuharibu pombe hizo.
 

Nae, Mkurugenzi wa Kibo Spirit kilichopo Sinza kwa Remmy Muhid Mwacha amesema kuwa kiwanda hicho kilikuwa bado kipo kwenye majaribio ya kutengeneza viroba aina ya Double Panch lakini kwa sasa hawaendelei na uzalishaji wa pombe hizo ila kiwanda hicho kwa sasa kinazalisha maji ya kunywa ya Kibo Cool.
 

Operesheni ya viroba ilianza rasmi jana kwa mkoa mzima wa Dar es Salaam ambapo ni utekelezaji wa agizo la Serikali la kuzuia uzalishaji, usambazaji na utumiaji wa pombe hizo kuanzia Machi 1, mwaka huu. Adhabu ya kutumia, kusambaza au kuzalisha pombe hizo ni faini inayoanzia shilingi elfu 50 mpaka milioni 5 na kifungo cha kuanzia miezi 3 mpaka miaka 3 jela.

Mwisho.

Hakuna maoni :

Chapisha Maoni