.

.

.

.

.

.

.

.
KARIBUNI TUHABARIKE, TUELIMISHANE, TUPEANE HABARI ZA KUKUFANYA UTABASAMU KIDOGO NA MATUKIO YALIYOFANYIWA UCHUNGUZI WA KINA TOKA KILA PEMBE CONTACTS: +255 787 377 722 Email: drweyunga@gmail.com PIA UNAWEZA KUNI FOLLOW KUPITIA INSTAGRAM YANGU @drweyunga | TANGAZA NASI ILI UWAFIKIE WATU WENGI ZAIDI.

Jumatatu, 6 Machi 2017

POMBE ZA VIROBA ZENYE THAMANI YA SHILINGI BILIONI 10.8 ZIMEKAMATWA JIJINI DAR ES SALAAM

Na: Lilian Lundo – MAELEZO
 

Pombe kali zilizofungashwa katika vifungashio vya plastiki maarufu kama ‘viroba’ zenye thamani ya shilingi Bilioni 10.8 zimekamatwa Jijini Dar es Salaam katika msako wa pombe hizo uliofanyika kuanzia Machi 01 mpaka 03, mwaka huu.
 

Hayo yamesemwa na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) January Makamba leo Jijini, Dar es Salaam alipokuwa akiongea na waandishi wa habari kuhusu operesheni ya utekelezaji wa maelezo ya Serikali ya kusitisha pombe hizo za viroba hapa nchini kuanzia Machi 01, mwaka huu.
 

“Jumla ya katoni 99,171 za pombe kali zilizofungashwa kwenye vifungashio vya plastiki (Viroba) zimekamatwa ambapo katoni 69,045 ni zenye ujazo wa na mililita 50, katoni 29,344 zenye ujazo wa mililita 100, katoni 782 zenye ujazo wa mililita 90 pamoja na katoni 10,625 za chupa zenye ujazo wa mililita 100. Thamani yake ni Shilingi Bilioni 10.83,” alifafanua Makamba.
 

Aliendelea kwa kusema kuwa, jumla ya viwanda 16 vya kuzalisha pombe kali, maduka ya jumla 18, maghala 4, baa 3 na kiwanda kimoja cha kuzalisha bidhaa za plastiki ikiwemo vifungashio vya plastiki vya kufungashia viroba vilikaguliwa katika opesheni hiyo.
 

Makamba amesema kuwa, pombe zilizokamatwa zimezuiliwa kuuzwa au kusambazwa kutoka katika maeneo ambayo yamehifadhiwa yaani viwanda, maghala pamoja na maduka ya jumla mpaka hapo Serikali itakapotoa tamko.
 

Aidha wananchi wametakiwa kushiriki katika utekelezaji wa maelekezo ya Serikali kwa kutoa taarifa zitakazowezesha kubaini wanaokaidi agizo la Serikali la kuzalisha, kusambaza, kuuza au kutumia pombe hizo kupitia namba ya simu 0685 333 444 kwa kutuma ujumbe mfupi wa meseji au whatsapp au kwa kupiga simu.
 

Vile vile amesema kuwa zawadi kati ya shilingi laki 5 hadi milioni 1 zitatolewa kwa mwananchi atakayetoa taarifa itakayowezesha kukamatwa na kushtakiwa kwa mtu yeyote mwenye ghala au aliyehifadhi shehena ya pombe za viroba kinyume cha sheria, watu au mtu anayeingiza pombe za viroba nchini kutoka nje ya nchi kinyume na sheria na utaratibu, anayehamisha au kusafirisha pombe za viroba kinyume na sheria, mtu mwenye kiwanda/mtambo wa kuzalisha pombe za viroba ambao hautambuliki na Serikali pamoja na mtu anayetumia stempu feki za TRA .
 

Pombe za viroba zimechangia kwa kiasi kikubwa uchafuzi wa mazingira, kupotea kwa nguvu kazi ya Taifa, ajali na vifo vinavyosabaishwa na unywaji uliokithiri wa pombe hizo, kuongezeka kwa vitendo vyauhalifu na kupotea kwa mapato yanayosababishwa na wafanyabiashara wasio waamini.
 

Kutokana na athari hizo, Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Kassim Majaliwa alipokuwa Mkoani Manyara, Februari 16 mwaka huu alitoa tamko la kusitisha uzalishaji, usambazaji, uuzaji na utumiaji wa pombe kali za viroba kwa nchi nzima kuanzia Marchi 01, mwaka huu.

Hakuna maoni :

Chapisha Maoni