Timu ya Taifa ya mpira wa miguu ya Vijana wa Tanzania wenye umri wa chini ya miaka 17 ‘Serengeti Boys’, leo Jumamosi tarehe 04 Machi, 2017, watatembelea Kituo cha vijana wanaopatiwa matibabu baada ya kuathirika na dawa za kulevya.
Kituo hicho kinachoitwa Sober House kipo Bagamoyo mkoani Pwani. Ni kituo maalumu kwa tiba ya vijana kinaendeshwa na kusimamiwa na Shirika la Life and Hope Rehabilitation Centre chini ya Mkurugenzi, Al-Karim Bhanji.
Ikiwa huko, vijana wa Serengeti Boys ambao kwa sasa wako kwenye kipindi cha mabadiliko ya katika sayansi ya mwili hivyo itakuwa somo kubwa kwao katika kujielimisha kuhusu mustakabali wa maisha yao.
Kwa upande wa TFF kuwapeleka vijana hao huko ni utekelezaji Kanuni ya 36 (7) ya Ligi Kuu ya Vodacom inayozungumza kukataa rushwa, madawa, ubaguzi, fujo, kamari na mambo mengine ya hatari kwa mchezo wa mpira wa miguu.
MECHI 4 LIGI KUU YA VODACOM
Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara (VPL), inatarajiwa kuendelea leo Jumamosi vinara wa ligi hiyo Simba inatarajiwa kuialika Mbeya City kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Ukiacha mchezo huo, michezo mingine ya leo Jumamosi Machi 4, mwaka huu itakuwa ni kati ya Toto Africans na Mbao FC kwenye Uwanja wa CCM Kirumba, jijini Mwanza huku Kagera Sugar ikiikaribisha Majimaji ya Songea kwenye Uwanja wa Kaitaba mjini Bukoba.
Azam FC pia itacheza Jumamosi Machi 4, mwaka huu na Stand United ya Shinyanga kwenye Uwanja wa Chamazi. Mchezo huo utaanza saa 1.00 jioni wakati mechi nyingine zitaanza saa 10.00 jioni.
Jumapili Machi 5, mwaka huu Mtibwa Sugar itaialika Young Africans kwenye uwanja huo katika mfululizo wa mechi za Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara.
Mchezo mwingine wa Ligi Kuu ya Vodacom utachezwa Uwanja wa Uhuru ambako African Lyon itaialika Mwadui ya Shinyanga wakati Ndanda FC itakuwa mwenyeji wa Ruvu Shooting kwenye Uwanja wa Nangwanda Sijaona siku ya Jumatatu Machi 6, mwaka huu.
IMETOLEWA NA SHIRIKISHO LA MPIRA WA MIGUU TANZANIA (TFF)
Hakuna maoni :
Chapisha Maoni