UTANGULIZI
1. Mheshimiwa
Spika, naomba kutoa Hoja
kwamba kutokana na taarifa zilizowasilishwa leo katika Bunge lako Tukufu
na Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Katiba na Sheria, Mwenyekiti wa
Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Bajeti na Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge
ya Masuala ya UKIMWI zilizochambua Bajeti ya Ofisi ya Waziri Mkuu, Bunge lako
sasa lipokee na kujadili Taarifa ya Mapitio ya Utekelezaji wa Kazi za Serikali
kwa mwaka 2016/2017 na Mwelekeo wa Kazi za Serikali kwa mwaka 2017/2018. Aidha,
ninaliomba Bunge lako Tukufu likubali kupitisha Makadirio ya Mapato na Matumizi
ya Fedha ya Ofisi ya Waziri Mkuu na Taasisi zilizo chini yake pamoja na Mfuko
wa Bunge kwa mwaka 2017/2018.
2.
Mheshimiwa Spika, katika mwaka
2016/2017, Bunge lako Tukufu limeondokewa na Wabunge wenzetu, Mheshimiwa Hafidh
Ally Tahir aliyekuwa Mbunge wa Jimbo la Dimani - CCM na Mheshimiwa Dkt. Elly
Marko Macha, aliyekuwa Mbunge wa Viti Maalum - CHADEMA. Pia, Taifa lilimpoteza Mheshimiwa
Samwel John Sitta aliyekuwa Spika Mstaafu wa Bunge la Tisa la Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania. Aidha, nchi yetu imekumbwa na majanga na maafa
yaliyosababisha vifo, majeruhi na uharibifu wa mali. Ninaomba Mwenyezi Mungu
awajalie nafuu ya haraka wale wote waliopata majeraha, na kuwapumzisha kwa
amani wale waliopoteza maisha, Amina!
Ninatoa pole kwa familia za wote waliopoteza ndugu, jamaa na marafiki. Pia
ninatoa pole kwa Mheshimiwa Aida Khenani aliyepata ajali ya kugongwa na
pikipiki wakati akitoka Bungeni. Tunamuombea apone haraka na aweze kurejea
Bungeni ili kuendelea na majukumu yake.
PONGEZI NA SHUKRANI
3.
Mheshimiwa Spika, nitumie
fursa hii kumpongeza Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,
Mheshimiwa Makamu wa Rais na Mheshimiwa Rais wa Zanzibar kwa kutimiza mwaka
mmoja wa uongozi wao. Sisi tunaowasaidia tunajivunia uongozi wao mahiri,
uzalendo uliotukuka na dhamira njema waliyonayo kwa Watanzania.
4. Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2016/2017, Bunge lako
Tukufu limepokea na kuwaapisha Wabunge wapya watano, ambao ni Mheshimiwa
Abdallah Majura Bulembo (Mb.), Mheshimiwa Anne Killango Malecela (Mb.),
Mheshimiwa Juma Ali Juma (Mb.), Mheshimiwa Prof. Palamagamba John Aidan Mwaluko
Kabudi (Mb.) na Mheshimiwa Salma Rashidi Kikwete (Mb.). Ninawapongeza sana
Waheshimiwa Wabunge wapya kwa heshima waliyoipata ya kujumuika nasi kwenye
Bunge hili. Kama ilivyo ada, tutatoa ushirikiano unaotarajiwa kwa Waheshimiwa
Wabunge hawa ili watekeleze majukumu yao kwa ufanisi na tija. Kipekee,
ninampongeza Mheshimiwa Prof. Palamagamba John Aidan Mwaluko Kabudi (Mb.) kwa
kuteuliwa kuwa Waziri wa Katiba na Sheria.
Pia
ninatumia nafasi hii kuwapongeza Waheshimiwa Wabunge wote walioteuliwa kuingia
kwenye Bunge la Afrika Mashariki, Makatibu Wakuu wapya walioteuliwa na
Mheshimiwa Rais yaani Profesa Kitila Alexander Mkumbo, Dk. Leonard Akwilapo,
Maimuna Tarishi na Dk. Ave Maria Semakafu. Nawapongeza sana wote walioteuliwa
kushika nyadhifa hizo.
5.
Mheshimiwa Spika, nitumie
fursa hii kuwashukuru Wajumbe wa Kamati za Kudumu za Bunge kwa kazi kubwa ya
kupitia Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara, Mikoa, Wakala, Idara za
Serikali zinazojitegemea na Mamlaka za Serikali za Mitaa. Ninawashukuru kipekee
sana Wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Katiba na Sheria inayoongozwa na
Mheshimiwa Mohamed Omary Mchengerwa, Mbunge wa Rufiji; Kamati ya Kudumu ya
Bunge ya Masuala ya UKIMWI inayoongozwa na Mheshimiwa Dkt. Faustine Engelbert
Ndugulile, Mbunge wa Kigamboni na Kamati ya Bajeti inayoongozwa na Mheshimiwa
Hawa Abdulrahman Ghasia, Mbunge wa Mtwara Vijijini kwa kutoa mchango mkubwa
wakati wa maandalizi ya Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Fedha ya Ofisi ya
Waziri Mkuu. Pia, niwapongeze Wenyeviti na Makamu Wenyeviti wa Kamati za Kudumu
za Bunge kwa kuongoza kwa umahiri mkubwa Kamati zao wakati wa kupitia makadirio
ya sekta zote. Maoni na ushauri wao umesaidia sana kuboresha Makadirio ya Bajeti
ya Serikali kwa mafungu yote.
6.
Mheshimiwa Spika, niruhusu pia niwashukuru Waheshimiwa Mawaziri na Naibu
Mawaziri, Katibu Mkuu Kiongozi, Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Makatibu Wakuu, Wakuu
wa Mikoa na Wilaya, Wakuu wa Idara, Mashirika na Taasisi zote za Serikali kwa
ushirikiano wanaoendelea kunipa katika kutekeleza majukumu yangu. Aidha, ninawashukuru
Wafanyakazi wote wa Serikali na Taasisi zake chini ya Uongozi wa Katibu Mkuu
Kiongozi, kwa kukamilisha Bajeti ya Serikali ya mwaka 2017/2018.
7.
Mheshimiwa Spika, kipekee, ninamshukuru Mheshimiwa Jenista Joakim Mhagama (Mb.), Mbunge
wa Peramiho, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge, Kazi, Ajira,
Vijana na Wenye Ulemavu); Mheshimiwa Anthony Peter Mavunde (Mb.), Mbunge wa
Dodoma Mjini na Naibu Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Ajira na
Vijana) kwa ushirikiano wao mkubwa
katika utekelezaji wa majukumu ya Ofisi ya Waziri Mkuu. Aidha, ninamshukuru
Mheshimiwa Dkt. Abdallah Possi aliyekuwa Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri
Mkuu kwa kazi kubwa aliyofanya wakati akiitumikia nafasi hiyo. Ninamtakia kazi
njema kwenye jukumu lake jipya la
kuiwakilisha Tanzania nchini Ujerumani. Vilevile, ninawashukuru wafanyakazi
wote wa Ofisi ya Waziri Mkuu, chini ya Uongozi wa Makatibu Wakuu, Dkt. Hamisi
H. Mwinyimvua; Bwana Eric F. Shitindi na aliyekuwa Katibu Mkuu Bwana Uledi A.
Mussa kwa ushauri wao wa kitaalam kwangu na kwa Waheshimiwa Mawaziri.
8.
Mheshimiwa Spika, ninazishukuru
pia nchi marafiki, Taasisi na Mifuko ya Fedha Duniani, Mashirika ya Umoja wa
Mataifa, Madhehebu ya Dini na Mashirika yasiyo ya Kiserikali kwa kuunga mkono
jitihada za Serikali katika kujenga uchumi wa nchi yetu. Misaada na mikopo iliyopatikana kwa wakati
imechangia kutekeleza miradi ya maendeleo na kuboresha utoaji wa huduma kwa
wananchi.
9.
Mheshimiwa Spika, ninapenda
kutumia fursa hii kuwashukuru kwa dhati wananchi wa Jimbo la Ruangwa kwa
kuendelea kuniunga mkono na kuielewa vizuri dhamana ya Kitaifa niliyonayo ya
kusimamia utendaji wa Serikali katika sekta zote na kuwa Kiongozi wa Shughuli
za Serikali Bungeni. Mwisho ninaishukuru
familia yangu hususan mwenza wangu mpendwa, Mary na watoto wetu kwa upendo, dua
na kuendelea kunitia moyo ili nitekeleze kwa ufanisi zaidi majukumu yangu ya
Kitaifa. Asanteni sana!
MWELEKEO WA BAJETI
10.
Mheshimiwa Spika, ni mwaka mmoja sasa tangu Serikali ya Awamu ya Tano
iingie madarakani. Katika kipindi
hicho, yapo mambo mengi yaliyofanyika kwa mafanikio makubwa ambayo yataanishwa
kwa kina katika bajeti za Sekta pindi Mawaziri husika watakapoziwasilisha.
Baadhi ya mafanikio hayo ni utekelezaji wa ahadi ya Serikali ya Elimu Bila
Malipo; kuongezeka kwa uzalishaji na kasi ya usambazaji wa umeme vijijini; kuimarika
uwajibikaji na nidhamu katika Utumishi wa Umma; kuongeza ukusanyaji wa mapato
na udhibiti wa matumizi ya fedha za Umma; kuboresha huduma za kiuchumi na za kijamii;
na kutekeleza Awamu ya Kwanza ya Mpango wa Serikali Kuhamia Dodoma. Nitumie
fursa hii kuwashukuru Waheshimiwa Wabunge, Viongozi wa Serikali, Watumishi wa
Umma na Watanzania wote kwa ujumla kwa kuendelea kuiunga mkono Serikali katika
utekelezaji wa majukumu yake, kwani bila ushirikiano wao, tusingeweza kupata
mafanikio hayo.
11.
Mheshimiwa Spika, Bajeti ya
Ofisi ya Waziri Mkuu imeendelea kuandaliwa kwa kuzingatia Ilani ya Uchaguzi ya
Chama Cha Mapinduzi ya mwaka 2015; Mpango wa Taifa wa Maendeleo wa Miaka Mitano;
ahadi za Mheshimiwa Rais alizotoa wakati wa Kampeni, pamoja na maelekezo yake
wakati anazindua Bunge la 11 la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania tarehe 20
Novemba, 2015. Bajeti hii itaendelea kuimarisha mafanikio yaliyopatikana katika
mwaka uliopita na kushughulikia utatuzi wa vikwazo vya kukuza uchumi kwa haraka
na baadhi ya changamoto zilizojitokeza. Aidha, Serikali itajikita zaidi katika
maeneo yatakayochangia kuimarisha uchumi wa viwanda na kuboresha huduma za
jamii. Ninawaomba Waheshimiwa Wabunge na wananchi kwa ujumla, kuendelea
kushirikiana na Serikali katika kufikia azma hiyo ili dhamira yetu
ya kuboresha maisha ya Watanzania iweze kutimia. Ni vyema tukakumbuka kwamba
tuna mwaka mmoja tu wa utekelezaji wa yale tuliyopanga kufanya ndani ya kipindi
cha miaka mitano. Tutatumia bajeti ya mwaka ujao wa fedha kukabili changamoto
zilizojitokeza. Ahadi ya Serikali ni kuendelea kuwatumikia wananchi kwa
uadilifu na bila ubaguzi wowote, huku tukitanguliza mbele maslahi ya Taifa.
SERIKALI KUHAMIA DODOMA
12. Mheshimiwa
Spika, tarehe 23
Julai 2016, Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania akihutubia Mkutano Mkuu Maalum wa Chama Cha Mapinduzi, alitangaza
uamuzi wa kuhamishia rasmi Shughuli za Serikali Kuu Dodoma. Kufuatia uamuzi
huo, mipango ya kuhamia Dodoma kwa awamu ilianza baada ya mahitaji halisi yatakayoiwezesha
Serikali kuhamia Dodoma kubainishwa, ikiwa ni pamoja na ofisi na nyumba za
makazi kwa viongozi na watumishi wa umma. Awamu ya kwanza ilipangwa kuhama
ifikapo mwisho wa mwezi Februari, 2017.
13.
Mheshimiwa
Spika, ninafurahi
kuliarifu Bunge lako Tukufu kwamba tayari watumishi 2,069 wakiwemo Mawaziri,
Naibu Mawaziri, Makatibu Wakuu, Naibu Makatibu Wakuu, baadhi ya Wakuu wa Idara
na Vitengo na watumishi wengine wamekwishahamia Dodoma kama ilivyopangwa.
Vilevile, Wizara zote zimepata majengo ya Ofisi yatakayotumika katika kipindi
cha mpito.
14.
Mheshimiwa
Spika, ili Mji
wa Dodoma uweze kuendelezwa kwa mpangilio mzuri, Serikali inaupitia upya Mpango
Kabambe wa Mji wa Dodoma. Mapitio hayo yatasaidia sana kuepuka makosa
yaliyofanyika katika miji mingi hususan ujenzi holela unaochangia katika
uchafuzi wa mazingira na kuharibu mandhari ya miji. Ni wazi kwamba, ujenzi wa
Mji wa Dodoma hautafanywa na Serikali pekee, bali tutaendelea kuhamasisha Sekta
binafsi na wadau wengine kuwekeza Dodoma. Ninalipongeza sana Shirika la Nyumba
la Taifa (NHC) kwa kujenga nyumba 300 za makazi hapa Dodoma ambazo watumishi
wanaweza kununua au kupangishwa. Ninatoa wito kwa Mamlaka ya
Ustawishaji Makao Makuu Dodoma kuongeza kasi ya upimaji wa viwanja, kuboresha
miundombinu na kudhibiti ujenzi holela kwa kushirikiana kwa karibu na Manispaa
ya Dodoma na Taasisi nyingine za Serikali.
SIASA
15.
Mheshimiwa
Spika, mwaka
mmoja baada ya Uchaguzi Mkuu wa Mwaka 2015, hali ya kisiasa nchini imeendelea
kuwa shwari na ya kuridhisha. Aidha, Chaguzi Ndogo zilifanyika tarehe 22
Januari, 2017 katika Jimbo la Dimani - Zanzibar na Udiwani katika kata 20
Tanzania Bara kwa kushirikisha wagombea kutoka vyama 15 vya siasa. Ninavipongeza
vyama vyote vilivyoshiriki katika chaguzi hizo, na kipekee nakipongeza Chama
cha Mapinduzi kwa ushindi wa Jimbo la Dimani na viti 19 vya udiwani katika chaguzi
hizo.
16. Mheshimiwa Spika, baada ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka
2015, mashauri 53 ya kupinga ushindi wa Ubunge na mashauri 194 ya kupinga
ushindi wa Udiwani yalifunguliwa. Mashauri hayo yamekwishasikilizwa na hukumu
kutolewa, isipokuwa shauri moja la kupinga matokeo ya Ubunge katika Jimbo la
Mbagala. Nizipongeze Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali na Tume ya Taifa ya
Uchaguzi kwa kazi kubwa waliyofanya ya kuhakikisha kesi hizo zinaendeshwa kwa
kasi na kwa weledi na hivyo kuwezesha wananchi kuendelea kupata uwakilishi.
17. Mheshimiwa Spika, ili kuendelea kuboresha demokrasia
hapa nchini, hatuna budi kujenga jamii inayoheshimu na kuzingatia sheria, kanuni na taratibu za nchi pamoja na kuwa na
uvumilivu wa kisiasa. Ninatoa rai kwa wadau wa siasa kote nchini kujenga
utamaduni wa masikilizano na kuendesha siasa za maendeleo badala ya siasa za
malumbano; siasa za kuunganisha watu wetu badala ya kuwagawa; na siasa za
uwajibikaji badala ya siasa za mazoea. Serikali itaendelea kulinda na kuheshimu
misingi ya siasa zinazolenga kuleta ustawi wa wananchi na zinazotanguliza
maslahi ya nchi na wananchi.
MUUNGANO
18. Mheshimiwa Spika, Serikali inaendelea kudumisha
muungano wetu ambao ni tunu na mfano wa kuigwa barani Afrika na dunia nzima. Wananchi
wanaendelea kunufaika na matunda ya Muungano wetu ambao ni imara na dhabiti.
Serikali zote mbili zinafanya mashauriano kupitia Kamati ya Pamoja ya Serikali
ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ya kushughulikia
masuala ya Muungano chini ya Uenyekiti wa Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan,
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Vilevile, viongozi na watendaji
wa sekta nyingine zisizo za Muungano wamekuwa wakikutana mara kwa mara ili
kubadilishana uzoefu na kubaini maeneo ya ushirikiano kwa ustawi wa wananchi wa
pande zote mbili. Jumla ya vikao 13 vya sekta ambazo siyo za Muungano
vilifanyika kati ya Julai 2016 na Machi 2017.
19.
Mheshimiwa
Spika, ninapenda
kutumia fursa hii kumpongeza sana Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan, Makamu wa
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuendesha kwa ufanisi mkubwa kikao
kilichofanyika tarehe 13 Januari, 2017 ambapo taarifa kuhusu hoja zilizopatiwa
ufumbuzi, maagizo na maelekezo ya kufuatilia utekelezaji wa changamoto
zilizobaki ilitolewa. Serikali itaendelea kuulinda na kuuenzi Muungano wetu kwa
manufaa ya wananchi wa pande zote mbili.
HALI YA UCHUMI
20.
Mheshimiwa
Spika, mwenendo
wa viashiria vya ukuaji wa uchumi wa nchi yetu kwa mwaka 2016/2017 vinaonesha kuwa
uchumi wetu unakua na kuimarika. Kwa mujibu wa takwimu zilizotolewa na Ofisi ya
Taifa ya Takwimu, ukuaji halisi wa Pato la Taifa ulifikia asilimia 7.0 mwaka 2016. Sekta zilizochangia kwa kiwango kikubwa
kwenye ukuaji huo ni uchimbaji madini na mawe;
usafirishaji na uhifadhi wa mizigo; habari na mawasiliano; pamoja na
shughuli za fedha na bima. Mfumuko wa Bei uliendelea kubakia katika wigo wa
tarakimu moja na kasi ya upandaji bei ilipungua kutoka wastani wa asimilia 5.6 mwaka 2015 hadi asilimia
5.2 mwaka 2016. Kwa upande mwingine,
tathmini ya hali ya Taasisi za Fedha inaonesha kuwa Benki zetu ziko salama na
zina mitaji na ukwasi wa kutosha. Aidha, taarifa za Mashirika mbalimbali ya
Kimataifa zinaonesha kwamba katika mwaka 2016 uchumi wa Taifa letu ulikua
vizuri na hivyo kutufanya kuwa miongoni mwa nchi sita (6) za Bara la Afrika,
Kusini mwa Jangwa la Sahara ambazo uchumi wake unakua kwa kasi kubwa zaidi.
21.
Mheshimiwa
Spika, Serikali
ya Awamu ya Tano imeweka juhudi kubwa katika ukusanyaji wa mapato ya Serikali.
Kutokana na juhudi hizo, makusanyo ya ndani kupitia Mamlaka ya Mapato Tanzania
(TRA) yaliongezeka kutoka wastani wa Shilingi
Bilioni 850 kwa mwezi katika mwaka 2015/2016 hadi Shilingi Trilioni 1.2 kwa mwezi katika mwaka 2016/2017. Pamoja na
kuongeza ukusanyaji wa mapato, juhudi kubwa zimefanyika kudhibiti matumizi ya
rasilimali za umma ikiwa ni pamoja na kuziba mianya ya rushwa, ubadhirifu, wizi
na upotevu wa fedha za umma. Mwenendo huo umeiwezesha Serikali kuanza utekelezaji
wa miradi mikubwa kwa fedha za ndani na pia utoaji huduma kwa wananchi. Serikali
itaendelea kupanua wigo wa vyanzo vya mapato ya ndani na kuongeza kasi ya
ukusanyaji mapato ili kila anayestahili kulipa kodi aweze kuilipa.
22.
Mheshimiwa
Spika, kuimarika
kwa viashiria vya uchumi wa nchi yetu katika kipindi cha mwaka mmoja tangu
Serikali ya Awamu ya Tano iingie madarakani ni dalili njema katika kujenga
uchumi imara na tulivu utakaotusaidia kuelekea katika Uchumi wa Viwanda na
kufikia nchi ya kipato cha kati ifikapo mwaka 2025. Serikali itaongeza juhudi
katika kuchochea ukuaji wa sekta za kipaumbele zenye fursa kubwa ya kukuza
uchumi kwa haraka na kuondoa umaskini kama vile Kilimo na Viwanda. Pia, itahakikisha
kwamba sekta wezeshi kama vile Nishati, Habari na Mawasiliano, Fedha na ujenzi
wa miundombinu muhimu ya barabara, bandari, reli, vivuko na viwanja vya ndege zinaimarishwa.
Vilevile, Serikali itaendelea kuhimiza utekelezaji thabiti wa miradi ya
maendeleo na kuweka mazingira mazuri ya kufanya biashara na kuvutia uwekezaji.
Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi
23. Mheshimiwa Spika,
Serikali imeendelea kuwezesha Wananchi kupitia Mipango na Programu mbalimbali
kwa kuelekeza nguvu zaidi kwa makundi ya wanawake, vijana na wenye ulemavu.
Serikali imeweka mazingira bora kwa vikundi vya kiuchumi na vijana kujiunga na
Mifuko ya Hifadhi ya Jamii, SACCOS na VICOBA. Aidha, Serikali imeanzisha
majukwaa ya uwezeshaji wa wanawake kiuchumi katika mikoa yote na kufanya
mapitio ya Mwongozo wa Mfuko wa Maendeleo ya Wanawake wa mwaka 2007. Mapitio
hayo yana lengo la kuboresha uendeshaji na usimamizi wa Mfuko huo ili kuwezesha
wanawake wengi zaidi kukopesheka.
24.
Mheshimiwa
Spika, tunatambua kwamba asilimia 56 ya
nguvu kazi ya Taifa ni vijana. Hivyo, Serikali inatekeleza Programu ya Kukuza
Ujuzi na Stadi za Kazi ili kuwawezesha vijana kushiriki katika ujenzi wa uchumi
wa viwanda pamoja na kuinua ari ya vijana kupenda kufanya kazi. Katika mwaka
2016/2017, Serikali inatoa mafunzo kwa vijana 9,120 katika fani mbalimbali zikiwemo
stadi za kushona nguo, kutengeneza bidhaa za ngozi, mafunzo ya kurasimisha
ujuzi uliopatikana kwa mfumo usio rasmi na mafunzo ya kukuza ujuzi na stadi za
kujiajiri katika fani mbalimbali. Jumla ya vijana 1,469 wamehitimu mafunzo hayo
na kupata ajira. Vijana 7,651 waliobaki wanaendelea kupata mafunzo kupitia
viwanda vya TOOKU GARMENTS, MAZAVA FABRICS, Taasisi ya Teknolojia Dar es Salaam
(DIT), VETA na Don Bosco. Katika mwaka 2017/2018, Serikali itatoa mafunzo ya
kukuza ujuzi wa kujiajiri na stadi za kazi kwa vijana 15,350 katika fani
mbalimbali.
25.
Mheshimiwa
Spika, Serikali kupitia Mfuko wa Maendeleo
ya Vijana, imetoa mikopo yenye thamani ya Shilingi bilioni 1.5 kwa vikundi vya
vijana 297 katika Halmashauri mbalimbali nchini. Aidha, Mamlaka za Serikali za
Mitaa kupitia mapato yake ya ndani zimetoa Shilingi bilioni 4.6 ikiwa ni mikopo
yenye masharti nafuu kwa vikundi vya vijana 2,356. Hatua hizi zimekwenda
sanjari na utengaji wa maeneo maalum yenye jumla ya ekari 85,603 kwa ajili ya
shughuli za vijana za kilimo, biashara ndogo ndogo, burudani na michezo. Katika
mwaka 2017/2018, Serikali itaendelea kusimamia Halmashauri zote nchini kutenga
asilimia tano (5) ya mapato yao kwa ajili ya vijana na asilimia tano (5) kwa
wanawake.
Ajira na Mahusiano Mahali pa Kazi
26. Mheshimiwa Spika, Serikali imeendelea kuratibu utekelezaji wa juhudi za kukuza ajira nchini kama inavyoelekezwa
kwenye Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya mwaka 2015. Hadi kufikia Machi 2017, jumla
ya ajira 418,501 zimezalishwa nchini. Kati ya ajira hizo, ajira 239,017 sawa na
asilimia 57 zimezalishwa katika sekta binafsi wakati ajira 179,484 sawa na
asilimia 43 zimezalishwa kutokana na shughuli za sekta ya umma ikiwemo miradi
ya maendeleo.
27.
Mheshimiwa
Spika, Serikali
imefanya utafiti na kubaini kuwa asilimia 58 ya migogoro ya kikazi inatokana na
kutozingatiwa kwa taratibu za kuachisha kazi. Sekta zinazoongoza kwa migogoro
ya kazi ni usafirishaji, ujenzi, ulinzi binafsi, elimu, huduma za hoteli na
viwanda. Katika kupunguza migogoro mahali pa kazi, Serikali imefanya kaguzi na
kusimamia uundwaji wa Mabaraza ya Wafanyakazi. Aidha, Tume ya Usuluhishi na Uamuzi imeendelea kutimiza
wajibu wake wa kusuluhisha migogoro ambapo katika kipindi cha Julai 2016 hadi
Februari 2017, Tume imesajili jumla ya migogoro 8,832 kati ya hiyo migogoro
3,319 sawa na asilimia 37.6 ya migogoro yote iliyosajiliwa imesuluhishwa. Kati
ya migogoro hiyo iliyosuluhishwa, migogoro 1,957 ilifikia suluhu (mediation) na
migogoro 1,362 haikufikia suluhu. Aidha, migogoro 5,513 inaendelea kusuluhishwa
katika hatua mbalimbali.
Ninatoa wito kwa waajiri na waajiriwa
wote nchini, kuzingatia Sheria za Kazi na kuimarisha uhusiano mzuri kwenye
maeneo ya kazi, ili muda mwingi zaidi utumike kwenye uzalishaji mali badala ya
kutatua migogoro. Vilevile, ni muhimu sana kuimarisha kaguzi za kazi na
kuendelea kusaini mikataba ya kuunda na kusajili mabaraza ya wafanyakazi ili
kuimarisha zaidi mahusiano mahali pa kazi.
MAENDELEO YA KISEKTA
Sekta za Uzalishaji
Viwanda
28.
Mheshimiwa Spika, ili kujenga
uchumi wa viwanda, Serikali inahamasisha wawekezaji wa ndani na nje kujenga
viwanda vidogo, vya kati na vikubwa. Viwanda vinavyopewa kipaumbele ni vile
vinavyotumia malighafi zinazopatikana hapa nchini, vinavyotoa ajira kwa watu
wengi na vinavyozalisha bidhaa zenye soko hapa nchini na nje ya nchi. Katika
kuhakikisha Watanzania wanashiriki kikamilifu kwenye uchumi wa viwanda,
Serikali inahamasisha zaidi sekta binafsi ya hapa nchini pamoja na mashirika ya
umma kujenga viwanda. Jitihada hizo zimewezesha Mifuko ya Hifadhi ya Jamii ya
NSSF, PPF, LAPF, GEPF, PSPF na NHIF kuanza kufufua, kuendeleza na kujenga
viwanda vipya vipatavyo 27 katika maeneo mbalimbali nchini. Natoa pongezi kwa
Bodi na Menejimenti ya Mifuko hiyo, kwa kuunga mkono jitihada za Serikali
katika ujenzi wa viwanda nchini. Aidha, ninaendelea kuyasisitiza mashirika ya
umma kuhakikisha kwamba mipango yao inaendana na utekelezaji wa Mpango wa Pili
wa Maendeleo wa Taifa ambao dhima yake ni kujenga uchumi wa viwanda.
Maliasili na Utalii
29. Mheshimiwa Spika, sekta ya utalii ni moja kati ya sekta
muhimu sana katika uchumi wa nchi yetu. Kote ulimwenguni, mafanikio ya sekta ya
utalii kwa kiasi kikubwa hutegemea miundombinu thabiti ya utalii, huduma bora
na ulinzi na usalama. Ili kuendelea kunufaika na sekta hiyo, Serikali inaboresha
miundombinu ya utalii, kupanua wigo wa vivutio vipya vya utalii na kuimarisha huduma
ya usafiri wa anga. Vilevile, Serikali inafanya juhudi kubwa za kudhibiti
ujangili na biashara haramu ya wanyamapori ambapo watuhumiwa 897 walitiwa mbaroni na kati yao watuhumiwa
282 wamefikishwa Mahakamani.
30. Mheshimiwa Spika, idadi ya watalii imeongezeka kutoka
1,137,182 mwaka 2015 hadi watalii
1,284,279 mwaka 2016 sawa na ongezeko la
asilimia 12 na kuliingizia Taifa Dola za Marekani bilioni 2. Juhudi zilizoanza
za kuliimarisha shirika letu la ndege zinalenga pia kutoa mchango mkubwa kwenye
sekta ya utalii kwa kusafirisha watalii wa ndani na kutoka nje ya nchi. Shabaha
yetu ni kuongeza idadi ya watalii wanaokuja kutembelea nchi yetu na pia mapato
yatokanayo na sekta hiyo. Nitumie fursa hii kuisihi sekta binafsi kuwekeza
zaidi kwenye miundombinu muhimu ya sekta hii zikiwemo hoteli, kuboresha huduma
na kubuni mbinu mpya za kuvutia watalii.
Kilimo
31.
Mheshimiwa
Spika,
uzalishaji wa mazao ya chakula kwa msimu wa mwaka 2015/2016 ikijumuisha mazao
ya nafaka na yasiyo ya nafaka ulifikia tani
16,172,841 ikilinganishwa na mahitaji ya kitaifa ya tani 13,159,326. Hivyo, katika kipindi hicho nchi ilikuwa na ziada
ya tani 3,013,515 za chakula. Katika
msimu wa kilimo wa mwaka 2016/2017, hali ya upatikanaji wa mvua katika Mikoa
inayopata mvua za vuli haikuwa ya kuridhisha na hivyo kusababisha ukame na
upungufu wa mavuno katika baadhi ya maeneo. Tathmini ya awali imebainisha
kwamba Halmashauri 55 zimeathirika na ukame.
32.
Mheshimiwa Spika, ili kukabiliana na hali hiyo,
Serikali inaendelea kuhamasisha sekta binafsi kununua mazao ya chakula kutoka
katika maeneo yenye ziada na kuyauza katika maeneo yenye uhaba. Aidha, wafanyabiashara waliokuwa wamehifadhi nafaka
katika maghala, walitakiwa kuzisambaza katika masoko ya ndani. Vilevile, Wakuu
wa Mikoa na Wakuu wa Wilaya walielekezwa kuwahamasisha na kuwaelekeza wakulima
kupanda mbegu bora za mazao ya kilimo yanayostahimili ukame na yanayokomaa kwa
muda mfupi kwa kipindi hiki cha mvua za masika. Ili kutoa msukumo katika kazi
hiyo, kiasi cha tani 1,969 za mbegu
bora za mazao yanayostahimili ukame zilinunuliwa na Serikali na kusambazwa
katika Halmashauri zilizobainika kuathirika na ukame. Pia, wakulima wanaendelea
kuhamasishwa kuzitumia vizuri mvua zinazonyesha katika msimu huu wa masika kwa
kupanda mazao hayo yanayostahimili ukame na kukomaa mapema.
33.
Mheshimiwa
Spika, kwa
kutambua umuhimu wa sekta ya kilimo katika uchumi wetu, Serikali imeweka
dhamira ya kuongeza uzalishaji, tija na kukifanya kilimo kiwe cha kibiashara.
Katika mwaka 2016/2017, Serikali ilifanikisha kupatikana kwa tani 277,935 za mbolea na tani 23,333 za mbegu bora. Aidha, hadi Februari
2017, Serikali ilitoa tani 30,773 za
mbolea ya ruzuku ya kukuzia na kupandia kupitia vituo vya mauzo ya mbolea vya
Kampuni ya Mbolea Tanzania (TFC).
34. Mheshimiwa Spika, moja ya ahadi ya Serikali kwa
wakulima wetu ni kupunguza kodi, tozo na ada mbalimbali zinazochangia kupunguza
faida kwa mkulima. Katika mwaka 2016/2017, Serikali ilifuta baadhi ya tozo za
mazao ambazo ni kero kwa wakulima katika mazao ya pamba, chai na kahawa. Tozo
zilizofutwa kwenye zao la pamba ni
mchango wa Mwenge wa Shilingi 450,000 unaotolewa na kila kiwanda cha kuchambua
Pamba na ada ya vikao vya Halmashauri za Wilaya ambayo ni shilingi 250,000. Kwa
zao la chai, kodi ya moto na uokoaji imeondolewa na katika zao la kahawa, ada
ya leseni ya kusindika kahawa ya Dola za Marekani 250 nayo pia imefutwa.
35. Mheshimiwa Spika, Serikali pia imeboresha Mfumo wa
Stakabadhi za Mazao Ghalani kwa kuanzisha utaratibu wa wazi wa ununuzi wa mazao
kupitia minada. Mathalani, katika msimu wa 2016/2017 kwenye zao la korosho,
utaratibu huo umechangia kwa kiasi kikubwa kuongezeka kwa bei ya korosho kwa
kilo kutoka shilingi 1,200 hadi shilingi 3,800, bei ambayo haijawahi kufikiwa
katika historia ya zao la korosho nchini. Aidha, Mfumo wa Stakabadhi za Mazao Ghalani
na utaratibu wa minada umeongeza ushindani na kuvutia wafanyabiashara wa ndani
na nje ya nchi hususan nchi ya Vietnam na nchi nyingine kuja wenyewe kununua
korosho badala ya kutegemea soko la India pekee. Katika mwaka 2017/2018,
Serikali itaendelea na uchambuzi wa kina wa kodi, tozo na ada zilizobaki katika
sekta za kilimo, mifugo na uvuvi kwa lengo la kuziondoa au kuzipunguza ili
kumwezesha mkulima, mvuvi na mfagaji anufaike zaidi na jasho lake na kuongeza mapato
ya Halmashauri zetu. Kwa sasa, tunashughulikia zao la tumbaku kwa kupitia tozo
zake na pia kubaini ubadhirifu unaoendelea kwenye ushirika huo.
Mifugo
36.
Mheshimiwa Spika, Serikali imeongeza uzalishaji wa mitamba na uhimilishaji wa
mifugo ili kuhamasisha ufugaji wa kisasa na wenye tija. Mitamba 546 imezalishwa
kutoka mashamba ya Serikali na mitamba 88 kutoka NARCO na kusambazwa kwa
wafugaji wadogo. Aidha, Kituo cha Taifa cha Uhimilishaji – NAIC Usa River, Arusha
kimeimarishwa na kuongeza uzalishaji wa mbegu bora za ng’ombe hadi kufikia dozi 10,494 ikilinganishwa na dozi 8,000 zilizozalishwa na kusambazwa
katika mwaka 2015/2016. Pia, ng’ombe waliohimilishwa wameongezeka kutoka 221,390 mwaka 2015/2016 hadi ng’ombe 457,557 mwaka 2016/2017.
37.
Mheshimiwa Spika, kwa mwaka 2017/2018, Serikali itaendelea
kuimarisha kituo chetu cha kuzalisha mitamba cha Kitulo wilayani Makete ili
kukiongezea uwezo wake. Aidha, Serikali inatoa nafasi kwa mashamba binafsi
kuzalisha mitamba zaidi kama mashamba ya ASAS kule Iringa ili wafugaji wadogo
wanufaike. Serikali pia itaendelea na
zoezi la kutenga, kupima na kumilikisha wafugaji maeneo ya ufugaji na kujenga
miundombinu ya mifugo kwa kuongeza idadi ya malambo na mabwawa katika mikoa.
Hatua hizo zitasaidia kupunguza uzururaji wa mifugo na migogoro baina ya
wafugaji na wakulima na hifadhi za misitu.
Madini
38. Mheshimiwa
Spika, Sekta ya madini ni muhimu kwa uchumi wetu.
Serikali imetenga maeneo zaidi kwa ajili ya wachimbaji wadogo, kuweka utaratibu
mzuri zaidi wa kutoa ruzuku pamoja na kuimarisha shughuli za ugani. Katika
kipindi cha mwezi Julai 2016 hadi
Februari 2017, Serikali imetenga maeneo 11 yenye ukubwa wa hekta 38,567 kwa ajili ya wachimbaji madini wadogo. Maeneo hayo ni
Msasa na Matabe mkoani Geita, Biharamulo na Kyerwa mkoani Kagera, Itigi mkoani
Singida, D-Reef, Ibindi na Kapanda Mkoani Katavi, Ngapa mkoani Ruvuma, Kitowelo
na Namungo mkoani Lindi pamoja na Nzega mkoani Tabora.
39.
Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2017/2018, Serikali itaimarisha
ukusanyaji wa Mapato ya Serikali yatokanayo na rasilimali za madini na kuimarisha ukaguzi wa shughuli za uzalishaji
na biashara ya madini kwa migodi mikubwa, ya kati na midogo.
Aidha, Serikali itaendeleza wachimbaji wadogo na wa kati wa madini
pamoja na kuhamasisha shughuli za uongezaji thamani wa madini hayo.
Huduma za Kiuchumi
Ardhi
40.
Mheshimiwa Spika, katika mwaka
wa 2016/2017, Serikali iliahidi kuanza ujenzi wa Mfumo
Unganishi wa Kuhifadhi Kumbukumbu za Ardhi. Ninapenda kuliarifu Bunge lako
Tukufu kwamba kazi ya ujenzi wa mfumo huo awamu ya kwanza ilizinduliwa rasmi
Agosti, 2016 na Mkandarasi tayari ameanza kazi. Sambamba na zoezi hilo, Serikali
inakamilisha ujenzi wa Kituo cha Taifa cha Taarifa za Ardhi. Kukamilika kwa
mradi huo kutaboresha utendaji kazi, kuharakisha huduma za utoaji hati miliki,
kuongeza mapato ya Serikali na kuboresha utunzaji wa kumbukumbu za ardhi ambapo
nyaraka zote za ardhi zitakuwa katika mfumo unganishi wa kielektroniki.
41.
Mheshimiwa Spika, Serikali pia
iliidhinisha ramani za upimaji zenye jumla ya viwanja
78,771 na mashamba 239. Aidha,
Serikali imekamilisha upigaji wa picha za anga za Jiji la Dar es Salaam na
inaendelea kutatua migogoro ya
matumizi ya ardhi baina ya wakulima,
wafugaji na hifadhi katika maeneo mbalimbali nchini.
42. Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2017/2018, Serikali itaendelea kujenga Mfumo
Unganishi wa Kuhifadhi Kumbukumbu za Ardhi na kuboresha usimamizi wa sekta ya
ardhi kwa kufanya mapitio ya Sera na Sheria za Ardhi na kutoa elimu kwa wananchi kuhusu sera, sheria,
kanuni na miongozo ya ardhi ili kudhibiti viashiria vya migogoro ya matumizi ya
ardhi nchini. Ninatoa wito kwa Halmashauri zote nchini kuhakikisha kwamba zinashughulikia
migogoro ya ardhi mapema na kuweka mazingira wezeshi ya upimaji wa ardhi katika
Halmashauri zao.
Umeme
43.
Mheshimiwa Spika, Serikali
imechukua hatua thabiti za kuongeza uzalishaji, kuimarisha miundombinu ya
usafirishaji na kuongeza kasi ya usambazaji umeme. Katika mwaka 2016, umeme
uliozalishwa na kuingizwa katika Gridi ya Taifa uliongezeka na kufikia Gigawatt hours (GWh) 7,092 ikilinganishwa na Gigawatt hours (GWh) 6,227 zilizozalishwa mwaka 2015
sawa na ongezeko la asilimia 13.9. Vilevile, Serikali imepanua na
kuboresha njia za usafirishaji umeme kwa kukamilisha ujenzi wa njia ya umeme wa
msongo wa kilovolti 400 na upanuzi wa vituo vya kupoza umeme kutoka Iringa –
Dodoma – Singida – Shinyanga.
44.
Mheshimiwa Spika, Serikali
iliendelea kutekeleza miradi ya kusambaza umeme vijijini kupitia Wakala wa
Nishati Vijijini (REA) katika mikoa yote ya
Tanzania Bara. Katika kipindi cha mwaka
2016/2017, Wakala ulikamilisha ujenzi
wa vituo sita (6) vya kuongeza nguvu ya umeme
kutoka msongo wa kilovolti 11 hadi kilovolti
33 katika miji ya Kigoma, Kasulu, Kibondo, Ngara, Mbinga na Tunduru; ujenzi wa
njia za kusambaza umeme zenye urefu wa kilometa
17,740 za msongo wa kilovolti 33;
ujenzi wa vituo vidogo vya kupoza na kusambaza umeme 4,100; na ujenzi wa njia ndogo ya usambazaji umeme wenye urefu wa kilometa 10,970.
45.
Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2017/2018, Serikali itaongeza
uzalishaji, kuboresha miundombinu ya usafirishaji na kuongeza kasi ya
usambazaji wa umeme nchini. Aidha, Serikali itaendelea na utekelezaji wa Mradi
mkubwa wa Ujenzi wa Bomba la Mafuta kutoka Kabaale (Uganda) hadi Tanga
(Tanzania). Serikali pia, itawezesha uwekaji wa mtandao wa usambazaji wa gesi
asilia kwenye viwanda na matumizi ya majumbani pamoja na uendelezaji wa mradi
wa kusindika gesi asilia (Liquefied
Natural Gas - LNG) mkoani Lindi.
Barabara
46. Mheshimiwa
Spika, kuanzia mwezi Julai 2016 hadi Februari 2017, Serikali imejenga
na kukarabati jumla ya kilometa 430 za barabara
kuu sawa na asilimia 62 ya lengo la kilometa 692. Aidha, ujenzi wa barabara za juu kwenye makutano ya TAZARA unaendelea vizuri pamoja na maandalizi ya
kuitisha zabuni za ujenzi wa Daraja Jipya la Selander na ujenzi wa Barabara ya
Dar es Salaam – Chalinze kwa kiwango cha Expressway.
Vilevile, ujenzi wa barabara za juu (Interchange)
kwenye makutano ya Barabara ya Ubungo ulizinduliwa rasmi tarehe 20 Machi, 2017.
Hizi ni hatua muhimu za kukabiliana na changamoto ya muda mrefu ya msongamano wa
magari katika Jiji la Dar es Salaam ikiwa ni utekelezaji wa Ilani ya CCM ya
mwaka 2015.
Vivuko na Usafiri Majini
47.
Mheshimiwa Spika, katika Mwaka
wa Fedha 2016/2017, Serikali ilipanga kujenga kivuko kipya cha Pangani (MV
Pangani) na kukarabati kile cha Magogoni – Kigamboni. Napenda kuliarifu Bunge
lako tukufu kwamba hadi kufikia Februari, 2017 ujenzi na ukarabati wa vivuko
hivyo ulikuwa umekamilika. Aidha, ununuzi wa boti ndogo za abiria kwa ajili ya
vivuko vya Kilambo – Namoto (Mtwara), Mkongo – Utete (Pwani), Pangani – Bweni
(Tanga) na Msemo – Msangamkuu (Mtwara) utakamilika katika mwaka huu wa fedha. Kwa
upande wa huduma za usafiri kwenye maziwa, Serikali inaendelea na ujenzi wa
meli moja katika Ziwa Victoria, meli mbili katika Ziwa Nyasa zitakazofanya
safari kati ya Kyela na Mbambabay pamoja na ukarabati wa meli za MV Victoria na
Butiama (Ziwa Victoria) na MV Liemba (Ziwa Tanganyika).
Bandari
48.
Mheshimiwa Spika,
Serikali inatekeleza
Mpango wa Uboreshaji wa Bandari nchini kwa kufanya upanuzi na kuimarisha
miundombinu ya Bandari za Dar es Salaam, Tanga na Mtwara. Mifumo ya Ulinzi katika
bandari hizo imeimarishwa na mashine za kisasa za kukagua mizigo zimefungwa.
Kutokana na jitihada hizo, tumeanza kuona mwelekeo mzuri wa kuimarika ufanisi
wa kiutendaji hususan katika Bandari ya Dar es Salaam. Tutaendelea kufanya
maboresho zaidi ili Bandari ya Dar es Salaam iwe chaguo namba moja katika
usafirishaji wa mizigo ndani na nje ya nchi yetu.
Reli
49.
Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2016/2017, Serikali
iliendelea kutekeleza miradi ya uboreshaji wa miundombinu ya Reli ya Kati ili
kuongeza uwezo wa reli hiyo kutoa huduma za uchukuzi nchini na nchi jirani
zinazotumia bandari zetu. Awamu ya kwanza ya ujenzi wa reli mpya ya kati kutoka
Dar es Salaam hadi Mwanza kwa kiwango cha standard
gauge imeanza kutekelezwa kwa kusaini mkataba wa ujenzi wa kipande cha reli
ya Dar es Salaam - Morogoro (kilometa
205). Taratibu za kuwapata makandarasi wa ujenzi wa reli kutoka Morogoro –
Makutupora (kilometa 336),
Makutupora- Tabora (kilometa 294),
Tabora- Isaka (kilometa 133) na Isaka- Mwanza (kilometa 254) zinaendelea.
Usafiri wa anga
50. Mheshimiwa Spika,
katika mwaka
2016/2017, Serikali imetekeleza kwa dhati azma ya kuimarisha Kampuni ya Ndege
Tanzania (ATCL). Katika kipindi hicho, ndege mbili (2) aina ya Dash 8 – Q400
zenye uwezo wa kubeba abiria 76 kila moja zilinunuliwa na kuanza kutoa huduma
mwezi Oktoba, 2016. Aidha, mwishoni mwa mwaka 2016, Serikali iliingia mkataba
wa ununuzi wa ndege nyingine nne (4). Kati ya hizo, ndege moja ya aina ya Dash
8 - Q400 yenye uwezo wa kubeba abiria 76 inatarajiwa kuwasili mwezi Julai, 2017.
Ndege nyingine mbili (2) aina ya CS300 zenye uwezo wa kubeba abiria 127 kila
moja zinatarajiwa kuwasili mwezi Juni, 2018 na ndege kubwa moja ya masafa
marefu aina ya Boeing 787 Dreamliner yenye uwezo wa kubeba abiria 262
inatarajiwa kuwasili mwezi Julai, 2018.
51. Mheshimiwa Spika, kukamilika kwa ununuzi wa ndege hizi
kutaisaidia ATCL kuongeza safari za ndani na nje ya nchi na hivyo kuchangia
katika jitihada za kuongeza watalii wanaokuja nchini kutembelea vivutio vyetu
na kuimarisha usafiri wa anga hapa nchini. Aidha, ATCL imeanzisha safari za
kuja Dodoma na hivyo kuongeza uhakika wa usafiri wakati huu ambapo Serikali
inahamia Dodoma. Wigo wa upanuzi kwa viwanja vyote nchini unaendelea na sasa
hivi tunakamilisha ujenzi wa viwanja vya ndege.
Mawasiliano
52. Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2016/2017, baadhi ya
kazi zilizofanyika kwenye sekta ya mawasiliano ni pamoja na kuendelea na ujenzi
wa Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano; kutekeleza
Mradi wa Anuani za Makazi na Postikadi; na kuanzisha huduma ya kituo cha Jamii Centre kitakachorahisisha utoaji
wa huduma muhimu katika kituo kimoja. Huduma hizo ni kulipa pensheni, ankara na
huduma za kibenki. Aidha, Sekta ya Mawasiliano inatekeleza Programu ya
Miundombinu ya Kikanda ambayo inahusisha Mradi wa Shule Mtandao (e-school),
Mradi wa Video Conference ambao unahusisha ununuzi, usimikaji na
ufungaji wa vifaa vya TEHAMA katika Mikoa 26 na Taasisi za Serikali.
53.
Mheshimiwa
Spika, Serikali pia
inatekeleza mradi wa ujenzi wa miundombinu ya Mawasiliano Vijijini kwa
kushirikiana na Kampuni ya Viettel ya Vietnam.
Mradi huu unatekelezwa kwa kipindi cha miaka mitatu
2015-2017. Viettel wamekwishafikisha
miundombinu ya mtandao wa intaneti kwenye shule 417, Ofisi za
Halmashauri za Wilaya 123, Hospitali za Wilaya 74, Vituo vya Polisi vya Wilaya
131 na Ofisi za Posta 68.
54. Mheshimiwa
Spika, Serikali imekamilisha ujenzi wa kituo cha kuhifadhi
taarifa na mifumo ya Serikali (Government
Data Centre). Lengo ni kuongeza na kuimarisha usalama wa mifumo na taarifa
unaoenda sambamba na uhakika wa upatikanaji wa taarifa za Serikali katika
kutekeleza majukumu yake ya kila siku. Pamoja na ujenzi wa vituo hivyo, matumizi
ya TEHAMA yameongezeka na hivyo kuziwezesha taasisi za Serikali kutoa mchango
mkubwa kwenye uboreshaji na utoaji wa huduma, kuongeza mapato na kuokoa gharama
mbalimbali.
Sekta ya Huduma za Jamii
Elimu
55. Mheshimiwa Spika, Serikali imeendelea kujenga uwezo wa
walimu wa shule za msingi kwa kuwapa mafunzo hasa katika ufundishaji wa stadi
za Kusoma, Kuandika na Kuhesabu (KKK). Jumla ya walimu 22,995 wa shule za
msingi na walimu 519 wanaofundisha elimu maalum kwa wanafunzi wasioona na wenye
ulemavu wa kusikia wamepewa mafunzo hayo. Lengo ni kuhakikisha kila mwanafunzi
anayemaliza darasa la saba anajua kusoma na kuandika.
56.
Mheshimiwa
Spika, katika mwaka
2016/2017, Serikali iliendelea na mpango wa kutoa Elimumsingi bila malipo.
Tangu utekelezaji wa mpango huo uanze, Serikali imekuwa ikipeleka wastani wa Shilingi bilioni 18.77 kila mwezi,
ambapo shule za msingi 16,088 na shule za sekondari 3,602 zimenufaika na mpango
huo. Mpango huo umeleta manufaa kwa Watanzania wengi wa kipato cha chini na cha
kati na umeongeza uandikishaji wa wanafunzi kwenye shule za Msingi na
Sekondari. Kufuatia ongezeko hilo, tulijikuta tukilazimika kupambana na upungufu
wa madawati, jambo ambalo liliifanya Serikali ianzishe kampeni maalum ya kumtoa
sakafuni mtoto wa Kitanzania. Hivi sasa madawati sio tatizo tena kwenye shule
nyingi nchini. Nitumie fursa hii kutoa pongezi kwa Watanzania wote
walioshirikiana na Serikali katika kutatua changamoto ya upungufu wa madawati. Natoa pongezi kwa taasisi binafsi, watu
binafsi na Waheshimiwa Wabunge kwa michango yao yote.
57. Mheshimiwa Spika, uchumi wa viwanda
kwa kiasi kikubwa unahitaji rasilimaliwatu yenye weledi hasa katika masomo ya
hisabati na sayansi. Kama zilivyo nchi nyingine Barani Afrika, Tanzania
inakabiliwa na changamoto ya wanafunzi kutopenda kusoma masomo ya hisabati na
sayansi na hivyo kuchangia katika ufaulu duni kwenye masomo hayo. Ni dhahiri
kuwa watoto wetu wasipoweka bidii katika masomo ya hisabati na sayansi viwanda
vyetu vitalazimika kutegemea wataalamu kutoka nje ya nchi jambo litakalowafanya
Watanzania kuwa watazamaji.
58. Mheshimiwa Spika, ili kukabiliana na changamoto hiyo, Serikali
imefanya juhudi za kuhamasisha wanafunzi kupenda masomo ya sayansi katika ngazi
zote za shule. Aidha, Serikali inaendelea na Mpango wa Ujenzi wa Maabara katika
shule za sekondari na vyuo vikuu pamoja na ununuzi wa vifaa. Katika mwaka
2016/2017, Serikali imenunua vifaa vya maabara kwa ajili ya shule 1,625 za sekondari zilizokamilisha ujenzi wa maabara na
usambazaji wa vifaa umeanza mwezi Machi, 2017 katika Mkoa wa Dar es Salaam na
kazi hiyo inatarajiwa kukamilika mwishoni mwa mwezi Aprili, 2017 kwa nchi
nzima. Aidha, Serikali
inatoa mafunzo kwa walimu 5,920 wanaosoma
Stashahada maalum ya Sayansi, Hisabati na TEHAMA.
59. Mheshimiwa Spika, Serikali inakusudia kuimarisha
ufundishaji wa masomo ya TEHAMA kwa shule za Sekondari. Serikali inaendelea na mpango
wake wa kujenga maabara za kompyuta ili wanafunzi wawe na uelewa wa TEHAMA.
Utekelezaji wake utafanyika hatua kwa hatua.
60.
Mheshimiwa
Spika, Serikali
imetoa vibali vya ajira kwa walimu wa Hisabati
na Sayansi 4,129. Natoa wito kwa
wazazi wenzangu kuhamasisha watoto wetu kupenda masomo ya Hisabati na Sayansi.
Naagiza Wizara ya Elimu Sayansi na Teknolojia kwa kushirikiana na TAMISEMI na
wadau wengine waandae Mkakati Maalum wa kuhamasisha na kuwavutia wanafunzi
kusoma masomo ya Hisabati na Sayansi. Mkakati huo pia uwezeshe upatikanaji wa
walimu watakaofundisha masomo ya Hisabati na Sayansi katika shule za msingi na sekondari
kwa kipindi kifupi bila kuathiri ubora wa ufundishaji.
61.
Mheshimiwa
Spika, Serikali
imeendelea na ukarabati na ujenzi wa miundombinu katika Chuo Kikuu cha Mzumbe,
Chuo Kikuu cha Sayansi na Teknolojia Mbeya, Chuo Kikuu Kishiriki cha Mkwawa na
Taasisi ya Teknolojia Dar es Salaam. Ujenzi wa majengo 20 ya mabweni ya Chuo
Kikuu cha Dar es Salaam yenye uwezo wa kuchukua wanafunzi 3,840 umekamilika. Vilevile, Serikali inaimarisha
miundombinu katika vyuo vya ufundi vya Taasisi ya Teknolojia ya Dar es Salaam,
Chuo cha Sayansi na Teknolojia cha Mbeya na Chuo cha Ufundi Arusha kwa lengo la
kuimarisha mafunzo ya Ufundi na Sayansi nchini. Katika mwaka 2017/2018,
Serikali itaimarisha Vyuo vya Elimu ya Juu ili kuwezesha upatikanaji wa wataalam
mahiri katika nyanja mbalimbali hususan Sayansi na Teknolojia.
Maji
62. Mheshimiwa Spika, Serikali inatambua
umuhimu wa kusogeza huduma za maji karibu zaidi na wananchi ili wasitumie muda
mwingi kutafuta maji badala yake wajikite katika shughuli za uzalishaji mali.
Ili kutimiza azma hiyo, Serikali inatekeleza miradi mbalimbali ya maji mijini
na vijijini ikiwemo miradi ya vijiji 10 chini ya Programu ya
Maendeleo ya Sekta ya Maji. Kati ya mwezi
Julai na Desemba 2016, miradi 90 ya
maji vijijini ilikamilika na kufanya idadi ya miradi iliyokamilika kufikia 1,301 kati ya miradi 1,810
iliyolengwa. Miradi 509 iliyobaki
ipo katika hatua mbalimbali za utekelezaji na yote inatarajiwa kukamilika kabla
ya mwezi Juni, 2017.
63.
Mheshimiwa Spika, Serikali itaendelea kutekeleza miradi ya
maji vijijini katika Halmashauri zote nchini ukiwemo mradi wa maji wa Same –
Mwanga – Korogwe unaolenga kuhudumia wananchi zaidi ya 456,000 katika vijiji 38
kwenye miji ya Same, Mwanga na Korogwe Vijijini. Ili utoaji wa huduma ya maji uwe
endelevu, wananchi waendelee kuelimishwa kuhusu umuhimu wa kutunza vyanzo vya
maji, uvunaji wa maji ya mvua na matumizi bora ya maji. Nitumie fursa hii
kuwakumbusha watendaji katika Halmashauri zote kusimamia kikamilifu sheria
inayokataza shughuli za kibinadamu katika vyanzo vya maji.
Afya
64.
Mheshimiwa
Spika, Serikali
imeendelea kuhamasisha wananchi kujikinga dhidi ya magonjwa ikiwemo kuhimiza
lishe bora. Aidha, Serikali inaboresha upatikanaji wa huduma za afya nchini kwa
kujenga vituo vya kutolea huduma za afya na tiba pamoja na kuboresha
upatikanaji wa dawa na vifaa tiba. Bajeti ya ununuzi wa dawa na vifaa tiba imeongezeka
kutoka Shilingi bilioni 31 mwaka
2015/2016 hadi Shilingi bilioni 251 mwaka 2016/2017. Vilevile, Serikali
imeanzisha utaratibu wa kununua dawa na vifaa tiba moja kwa moja kutoka kwa
wazalishaji kwa lengo la kupunguza gharama. Serikali pia imeanzisha maduka ya
dawa yanayouza bidhaa zake kwa bei nafuu kwa wananchi katika hospitali za mikoa
ambapo hadi sasa maduka manane (8) yameanzishwa, na ujenzi wa maduka mengine
katika mikoa iliyobakia unaendelea.
65.
Mheshimiwa
Spika, Serikali pia
inaimarisha huduma za Afya ya Uzazi na Mtoto nchini kwa kutekeleza Mpango
Mkakati wa Kupunguza Vifo Vitokanavyo na Uzazi na Vifo vya Watoto wa mwaka
2016-2020. Lengo ni kuhakikisha kuwa ifikapo mwaka 2020, asilimia 50 ya vituo
vya Afya nchini vinakuwa na uwezo wa kutoa huduma za dharura kwa matatizo ya uzazi
ikiwemo upasuaji na huduma za watoto wachanga.
Hadi sasa, vituo vya afya 159 vinatoa huduma za upasuaji ambapo vituo
106 ni vya Serikali.
Vilevile, Serikali imeimarisha utoaji
wa huduma za kinga na hivyo kuchangia kutokomezwa kwa ugonjwa wa Polio hapa
nchini na hatimaye nchi yetu kuwa miongoni mwa nchi zilizopatiwa hati ya
kutokomeza ugonjwa huo. Katika mwaka 2017/2018, Serikali itaendelea kuimarisha
huduma za afya nchini kwa kuongeza kasi ya utekelezaji wa Mpango wa Maendeleo
wa Afya ya Msingi na kuimarisha huduma za kinga ili kupunguza vifo vya watoto
na akina mama pamoja na makundi mengine. Naomba
nitoe wito kwa wote Watanzania wajiunge kwa wingi na Mfuko
wa Afya ya Jamii (CHF) ili Serikali iweze kuwachangia kupitia mfumo huo.
BUNGE
66.
Mheshimiwa Spika, Ofisi
ya Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inatekeleza majukumu yake kwa
ufanisi mkubwa. Katika mwaka 2016/2017, Ofisi ya Bunge iliratibu na kusimamia shughuli za Mikutano mitatu ya
Bunge ambapo maswali 1,054 ya
kawaida, nyongeza na ya papo kwa papo kwa Waziri Mkuu yaliulizwa. Miswada kumi (10) ya Sheria ilijadiliwa
na kupitishwa na Bunge. Aidha, Bunge liliratibu na kusimamia shughuli za
Mikutano ya Kamati za Kudumu za Bunge, kutoa huduma za Hansard, utafiti,
utawala na kutoa mafunzo kwa Waheshimiwa Wabunge na Watumishi wa Ofisi ya
Bunge. Ofisi ya Bunge pia ilisimamia kazi ya ukarabati wa jengo la Bunge pamoja
na kuratibu ujenzi wa Ofisi za Waheshimiwa Wabunge. Katika mwaka 2017/2018,
Serikali itaendelea kuliwezesha Bunge kutekeleza majukumu yake ya Kikatiba kama
kawaida.
MAHAKAMA
67. Mheshimiwa
Spika, utendaji wa mhimili wa Mahakama nchini umezidi kuimarika. Katika
mwaka 2016/2017, Mahakama imesikiliza na kukamilisha mashauri 279,331 kati ya 335,962
katika ngazi zote za Mahakama sawa na asilimia
83.1 ya mashauri yote. Pamoja na kazi kubwa ya kusikiliza mashauri, Mahakama
imesogeza huduma zake karibu na wananchi kwa kukamilisha ukarabati na ujenzi wa
majengo ya Mahakama Kuu katika mikoa ya Tanga na Dar es Salaam. Pia, kazi za
ukarabati wa Mahakama Kuu katika Mkoa wa Mbeya inaendelea na ujenzi wa Mahakama
ya Wilaya na Mahakama ya Mwanzo Kibaha Mkoa wa Pwani umekamilika na
kuzinduliwa.
Mheshimiwa
Spika, ni matarajio yangu kwamba, katika mwaka
2017/2018, Mahakama itaendelea kutekeleza majukumu yake kwa ufanisi zaidi ili
kupunguza mlundikano wa mashauri yaliyopo mahakamani. Hata hivyo, ili Mahakama
ifanye kazi zake vizuri, shughuli za upelelezi wa kesi na uendeshaji wa
mashtaka zinatakiwa pia kuimarishwa zaidi. Serikali itafanya kila liwezekanalo
kuimarisha taasisi zote zinazohusika katika mlolongo wa utoaji haki ili
wananchi wapate haki zao kwa wakati.
MASUALA MTAMBUKA
Mfumo wa Ufuatiliaji wa Shughuli za Serikali
68.
Mheshimiwa Spika,
katika mwaka 2016/2017, Serikali iliahidi kuanzisha Mfumo wa Wazi wa
Kielektroniki wa kufuatilia uwajibikaji na utendaji Serikalini. Mfumo huo
utasaidia kuongeza ufanisi katika uratibu wa shughuli za Serikali kwa
kuwawezesha Viongozi kutoa maelekezo na kufuatilia utekelezaji wake. Aidha,
Mfumo huo utasaidia ufuatiliaji wa utekelezaji wa Ilani ya Chama cha Mapinduzi,
Ahadi na Maagizo ya Mheshimiwa Rais na Mpango wa Taifa wa Maendeleo. Napenda
kulialifu Bunge lako Tukufu kwamba, Mfumo huo umekamilika, kuzinduliwa rasmi na
mafunzo kutolewa kwa wataalamu katika Wizara zote. Mfumo huo pamoja na mambo
mengine utaongeza kasi ya utoaji taarifa za utekelezaji wa kazi za Serikali kwa
wakati na pia kuongeza uwajibikaji kwa watumishi wa Umma. Wizara na Taasisi
zote za Serikali zinatakiwa kuutumia Mfumo huo kikamilifu ili kurahisisha
ufuatiliaji wa utekelezaji wa kazi za Serikali na kusaidia viongozi kutatua
vikwazo pale vinapojitokeza.
Vita dhidi ya Rushwa
69.
Mheshimiwa Spika, Serikali inapambana na rushwa kwa nguvu zake zote na haina mzaha wala uvumilivu na vitendo vya rushwa. Hatua zilizochukuliwa kupambana na rushwa tangu
Serikali ya Awamu ya Tano ilipoingia madarakani Novemba, 2015 zimetambulika
hata na Mashirika ya Kimataifa yanayojishughulisha na tafiti kuhusu masuala ya
rushwa Duniani. Taarifa ya Shirika la Transparency
International kwenye utafiti wake kuhusu mtazamo wa
rushwa mwaka 2016 imeonesha kuwa viwango vya rushwa vinaendelea kupungua hapa
nchini.
70. Mheshimiwa Spika, katika Mwaka
2016/2017, Serikali kupitia TAKUKURU imefanya uchunguzi wa majalada 306
ya tuhuma za rushwa na kupata kibali cha Mkurugenzi wa Mashtaka Nchini kuendelea
na mashtaka kwa majalada 104. Katika kipindi hicho, TAKUKURU iliendesha kesi
674 zikiwemo kesi mpya 182, ambapo katika kesi 97 watuhumiwa walipatikana na
hatia na kuhukumiwa kifungo au kulipa faini. Kesi 407 zinaendelea kusikilizwa mahakamani.
Kutokana na operesheni zilizofanywa na TAKUKURU, kiasi cha Shilingi bilioni 9.75 ziliokolewa. Katika Mwaka 2017/2018, Serikali
itaendelea na mapambano yake dhidi ya rushwa hususan katika eneo la ukusanyaji
mapato ya Serikali, kudhibiti matumizi ya fedha za umma, malipo hewa, matumizi
mabaya ya fedha za ushirika na kuimarisha ufuatiliaji na ukaguzi wa miradi ya
maendeleo.
Vita dhidi ya UKIMWI
71.
Mheshimiwa Spika, mapambano dhidi ya UKIMWI yamekuwa yakitegemea kwa
kiasi kikubwa upatikanaji wa rasilimali fedha kutoka kwa Wadau wa Maendeleo. Ninapenda
kulijulisha Bunge lako Tukufu kuwa, Mfuko wa Udhamini wa UKIMWI ulioanzishwa na
Serikali miaka miwili iliyopita, ulizinduliwa tarehe 01 Desemba, 2016 ambapo
kupitia harambee iliyofanyika kwa ajili ya kuchangia Mfuko huo, shilingi
milioni 347 zilipatikana kama ahadi. Vilevile, Serikali imetenga kiasi cha shilingi
bilioni 5.6 kwa ajili ya Mfuko wa UKIMWI.
72.
Mheshimiwa Spika, Serikali inaendelea kutoa huduma kwa Watu Wanaoishi na
Virusi vya UKIMWI (WAVIU) ambapo hadi Desemba, 2016 WAVIU 839,574 sawa na
asilimia 63 ya WAVIU wote, walikuwa wamepatiwa dawa. Juhudi zinaendelea
kufanyika ili kuwahamasisha WAVIU kujitokeza na kuingia kwenye Mpango wa Tiba
ya Kufubaza Athari za UKIMWI. Aidha, Serikali imekamilisha uandaaji wa miongozo minne ya Taifa ya Kudhibiti
UKIMWI ikijumuisha Mpango Kazi wa Kinga, Mkakati wa Kondomu, Mkakati wa
Uwekezaji na Mpango kazi wa jinsia.
73.
Mheshimiwa Spika, Serikali
katika mwaka 2017/2018, itaimarisha uratibu wa afua za UKIMWI kwa wadau wote wa
sekta ya umma na binafsi na kupitia mifumo ya uratibu iliyoanzishwa. Serikali
kwa kushirikiana na wadau pia itazijengea uwezo Kamati zilizo katika ngazi ya
jamii hususan vijiji na kata ili kufikia malengo ya kitaifa na kimataifa ya
kupunguza na kumaliza UKIMWI ifikapo mwaka 2030 kwa kutumia mfumo ulio katika
jamii. Vilevile, Serikali itakamilisha utafiti wa nne wa kubainisha viwango vya
maambukizo ya UKIMWI nchini na kuboresha ushiriki wa sekta binafsi ili kuleta
ufanisi katika kuchangia mwitikio wa Taifa dhidi ya UKIMWI.
Huduma kwa Watu Wenye Ulemavu
74. Mheshimiwa Spika, katika 2016/2017, Serikali imeendelea kutoa huduma pamoja na kuongeza
upatikanaji wa haki na fursa kwa watu wenye ulemavu. Katika kutimiza azma hiyo,
Serikali imewaagiza Wakuu wa Mikoa kuhakikisha kuwa Kamati za Watu wenye
Ulemavu zinaanzishwa katika ngazi za Mikoa, Wilaya, Mitaa na Vijiji. Aidha,
Serikali imeanzisha kampeni za kupinga unyanyapaa na vitendo vya kikatili dhidi
ya watu wenye ualbino katika mikoa ya Shinyanga, Mwanza, Geita, Simiyu, Kagera,
Tabora, Kigoma, Mara, Mbeya, Katavi na Rukwa na kampeni hiyo itaendelea nchi
nzima.
75.
Mheshimiwa
Spika, Serikali pia inahakikisha
kwamba watumiaji wa lugha ya alama wanapata haki ya kupata habari na vituo
vyote vya televisheni vimeelekezwa kutumia wakalimani wa lugha ya alama. Napenda
kuvikumbusha Vituo vya Televisheni kuweka wakalimani wa lugha katika vituo
vyao. Katika mwaka 2017/2018, Serikali itaendelea kutoa huduma kwa watu wenye
ulemavu ikiwa ni pamoja na kutoa vifaa saidizi kwa wanafunzi wenye ulemavu shuleni
na vifaa vya kufundishia.
Vita Dhidi ya Dawa za Kulevya
76. Mheshimiwa spika, dawa za kulevya zinaathiri maisha ya
vijana wetu wengi na hivyo kuzima ndoto za maisha yao na kupunguza nguvu kazi
ya Taifa. Ili kupambana na janga hilo, katika mwaka 2016/2017, Bunge lako
Tukufu lilifanya marekebisho ya Sheria ya Kuzuia na Kupambana na Dawa za
Kulevya Na. 5 ya Mwaka 2015. Marekebisho hayo yameipa Mamlaka ya Kudhibiti na
Kupambana na Dawa za Kulevya nguvu ya kukamata, kupeleleza na kushitaki
watuhumiwa wanaohusika na biashara ya dawa za kulevya. Aidha, hivi karibuni
Mheshimiwa Rais Dkt. John Pombe Magufuli amefanya uteuzi wa Watendaji Wakuu watakaosimamia
Mamlaka hiyo.
77. Mheshimiwa Spika, katika kipindi cha Julai, 2016 hadi
Januari, 2017 watuhumiwa 11,303 walikamatwa kwa tuhuma za kujihusisha na
uzalishaji, usambazaji, uuzaji na matumizi ya dawa za kulevya katika sehemu mbalimbali
nchini. Kati ya watuhumiwa hao, watu
9,811, walikutwa na kesi za kujibu ambapo 9,174 wametiwa hatiani, 238
hawakukutwa na hatia na wengine 478 upelelezi wa kesi zao unaendelea. Pia
alisema tangu Tume mpya iundwe Februari mwaka huu, jumla ya watuhumiwa 79
wametiwa mbaroni na uchunguzi wa kesi zao unaendelea. Ni imani yangu kuwa, Mamlaka ya Udhibiti wa Dawa za
Kulevya itaendeleza kwa kasi zaidi juhudi za kupambana na uingizaji, uzalishaji,
usambazaji na matumizi ya dawa za kulevya hapa nchini. Watanzania wana imani
kubwa na Mamlaka hii na ninaomba wote tuipe ushirikiano wakati wote kwani vita
hii ni kubwa na ni ya Kitaifa! Aidha, nawasihi wazazi wenzangu, tuwe karibu na
vijana wetu na kufuatilia nyendo zao ili wasiingie kwenye mtego huu wa dawa za
kulevya.
Uratibu wa Maafa
78.
Mheshimiwa
Spika, Serikali wakati wote inahakikisha
kuwa nchi ipo katika hali ya utayari wa kukabiliana na maafa na pia kutoa
misaada ya kibinadamu ikiwemo huduma za matibabu, ushauri wa kisaikolojia, na vifaa
pale maafa yanapotokea. Serikali
imejenga vituo vipya 20 vya upimaji wa hali ya hewa katika Halmashauri 11 za Tarime,
Nyamagana, Muleba, Longido, Geita, Maswa, Kigoma, Sikonge, Kongwa, Serengeti,
na Kahama. Kuwepo kwa vituo hivyo kutaongeza ufanisi katika upatikanaji wa taarifa za tahadhari hasa kwa majanga ya
mafuriko na ukame.
79.
Mheshimiwa Spika, kufuatia
tetemeko la ardhi lililotokea katika Mikoa ya Kanda ya Ziwa mwezi Septemba 2016,
Serikali kwa kushirikiana na wadau imechukua hatua za kushughulikia athari zilizotokana
na tetemeko hilo. Huduma za afya na tiba na za kibinadamu za chakula na malazi zilitolewa
kwa walioathirika. Vilevile, Serikali ilirejesha hali ya miundombinu
iliyobomoka, yakiwemo majengo ya Serikali na Taasisi za Umma 686, Kituo cha
wazee Kilima pamoja na kutoa maturubai 6,237, mahema 367, mabati 7,300 na mifuko
ya saruji 1,825 kwa walioathirika. Serikali inaendelea na ujenzi wa Shule za
Ihungo, Nyakato na Omumwani pamoja na ukarabati wa Kituo cha afya Kabyaile
Ishozi. Ninapenda kuwashukuru sana wananchi wote na wadau waliotoa michango yao
kusaidia waathirika wa tetemeko la ardhi.
HABARI NA MICHEZO
Habari
80.
Mheshimiwa Spika, Bunge lako
Tukufu lilipitisha Sheria ya Huduma za Habari Na. 12 ya mwaka 2016 ambayo ni
muhimu katika kuimarisha usimamizi na uwajibikaji katika Sekta ya Habari nchini.
Kanuni za Sheria hiyo zimeandaliwa na tayari zimeanza kutumika. Natoa wito kwa
wadau wa sekta ya habari kuzingatia sheria na kanuni hizo ili kuimarisha weledi
katika tasnia ya habari. Aidha, nashauri wadau wa habari kujikita zaidi katika
kuandika na kutangaza habari za masuala ya maendeleo na uchumi ili kuwasaidia
wananchi kutekeleza azma ya Serikali ya Awamu ya Tano ya kujenga uchumi wa
viwanda na kuboresha huduma za kijamii.
Maendeleo ya Michezo
81.
Mheshimiwa Spika, tumeanza
kuona dalili nzuri za kuimarika kwa shughuli za michezo hapa nchini. Mathalan, timu
ya Mpira wa Miguu ya Serengeti Boys imefuzu
kushiriki Mashindano ya Fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika kwa vijana wenye
umri chini ya miaka 17 yatakayofanyika Gabon, Mei 2017. Napenda nimshukuru sana
Makamu wa Rais, Mama Samia Suluhu Hassan ambaye amewaaga na kuwakabidhi bendera
ya Taifa tayari kwenda kushiriki vita hiyo. Nawaomba Watanzania wote tuungane
pamoja kuiombea na kuiunga mkono timu yetu kwa michango ya hali na mali ili
kuiwezesha kushiriki kikamilifu. Kwa upande wa riadha, Mtanzania
mwenzetu Alphonce Simbu alipata medali katika mbio za marathon huko Mumbai
nchini India. Aidha, mwezi Septemba 2016, Timu ya Taifa ya Mpira wa Miguu ya
Wanawake Tanzania (Twiga Stars) iliweka historia ya kuwa timu ya kwanza kutwaa
taji la CECAFA. Ninatoa pongezi kwa wale wote walioliletea Taifa sifa kupitia
michezo. Naziombea dua ili ziweze kushiriki michuano ya kimataifa.
82.
Mheshimiwa Spika, michezo ni sekta
muhimu katika kuongeza ajira, kuimarisha afya, kukuza uchumi, kuimarisha umoja
wa Kitaifa na kuitangaza nchi Kimataifa. Nchi nyingi zilizofanikiwa kimichezo
ziliwekeza zaidi kujenga vipaji vya vijana katika michezo. Natoa wito kwa TFF ihakikishe
kuwa vijana wa Timu ya Serengeti Boys wanawekewa Mpango Endelevu wa Kukuza
Vipaji Vyao na kutunzwa vyema ili waweze kuiwakilisha nchi yetu katika
mashindano mengine ya kimataifa. Aidha, vyama vingine vya michezo vitoe msukumo
mkubwa kwenye kuwekeza zaidi kwa vijana wa shule za msingi na sekondari kwani
hao ndio watakuwa wawakilishi wetu katika miaka ijayo. Na mwaka huu, michezo ya
shule za msingi na sekondari itarejea na kufanyika mkoani Mwanza kama
ilivyotangazwa mwaka jana. Nazisihi wizara husika za TAMISEMI na Wizara ya
Elimu zianze maandalizi mapema na kuandaa mpango huo na kutoa taarifa timu hizo
ziweze kujiandaa na kushindana ili tupate wachezaji imara wa kushiriki michuano
hiyo.
ULINZI NA USALAMA
83. Mheshimiwa Spika, hali ya ulinzi na usalama nchini ni
shwari kutokana na kazi kubwa na nzuri inayofanywa na vikosi vyetu vya ulinzi
na usalama katika kulinda mipaka ya nchi yetu. Serikali imeendelea kuimarisha
Jeshi la Wananchi wa Tanzania kwa kulipatia zana na vifaa vya kivita na
kukamilisha mradi mkubwa wa ujenzi wa nyumba 6,064 za makazi ya askari ulioanza
mwaka 2013/2014. Kwa upande mwingine, Serikali kupitia Jeshi la Magereza inakamilisha
ujenzi wa nyumba zilizojengwa kwa njia ya ubunifu katika baadhi ya Magereza
ikiwemo ujenzi unaoendelea katika Gereza la Ukonga wa ghorofa 12 zenye uwezo wa
kuishi askari na familia 320.
84. Mheshimiwa Spika, Serikali itaendelea kuimarisha
usalama wa raia na mali zao kwa kufanya
operesheni za kuzuia uhalifu nchini, kufanya upelelezi wa kesi kwa kasi ili
kupunguza mlundikano wa kesi zilizopo mahakamani, na kusimamia sheria za barabarani ili
kupunguza ajali zinazoleta madhara kwa wananchi. Aidha, Serikali itaendelea
kutoa mafunzo kwa askari na maafisa wa jeshi ili kuboresha utoaji wa huduma kwa
wananchi, kupambana na vitendo vya rushwa na kupambana na biashara ya dawa za
kulevya.
MAMBO YA NJE NA USHIRIKIANO WA KIMATAIFA
85.
Mheshimiwa Spika, kudumisha
uhusiano mzuri na mataifa mengine duniani pamoja na mashirika ya kimataifa ni
moja kati ya Misingi ya Sera yetu ya Mambo ya Nje. Tumeendelea kuimarisha
ujirani mwema baina yetu na nchi jirani, nchi marafiki pamoja na mashirika ya
kikanda na kimataifa, jitihada ambazo zimetuwezesha kuvutia mitaji mikubwa ya
uwekezaji, utalii pamoja na kupanua fursa za kibiashara. Katika mwaka
2016/2017, Serikali imefungua Balozi mpya sita (6) katika
nchi za Algeria, Israel, Korea Kusini, Sudan, Qatar na Uturuki. Balozi hizo
zina kazi kubwa ya kuendeleza juhudi za kuitangaza Tanzania kama nchi yenye
vivutio vingi vya utalii na rasilimali zinazoweza kutumika kuvuta uwekezaji
kutoka mataifa hayo ikizingatiwa utulivu na amani iliyopo. Serikali itaendelea
kulinda na kutetea maslahi ya Tanzania nje ya nchi na kuweka mikakati ya
kunufaika na nafasi ya nchi yetu kihistoria.
Hivyo, ninatoa wito kwa mabalozi wetu wote waendelee kuitangaza nchi
yetu kama eneo mwafaka lenye fursa nyingi za utalii, uwekezaji na biashara.
HITIMISHO
86. Mheshimiwa Spika, ili kujenga uchumi wa viwanda tunahitaji
nidhamu ya kazi, ubunifu, elimu na matumizi makubwa ya sayansi na teknolojia.
Vilevile, tunahitaji kuimarisha sekta binafsi, miundombinu ya huduma za
kiuchumi na jamii na kuondoa urasimu usio wa lazima. Nafarijika kwamba misingi
tunayoendelea kujenga katika kutekeleza azma hiyo imeanza kuzaa matunda kama
nilivyoeleza awali. Ili kufanya mafanikio hayo yawe endelevu, naomba
nihitimishe hotuba yangu kwa kusisitiza mambo makuu yafuatayo:-
(i)
Mosi, ustawi wa nchi yetu na mafanikio ya
mipango yetu ya maendeleo vinategemea amani na utulivu. Hivyo, kila mmoja wetu
aweke nadhiri ya kuendelea kuilinda na kuienzi amani ya nchi yetu ili mipango
yetu iweze kufanikiwa. Tunalo jukumu la kuhimiza amani ili tufanye kazi zetu
kwenye mazingira ya amani na utulivu.
(ii)
Pili, jukumu la kujenga uchumi wa nchi yetu
ni wajibu wa kila mwananchi. Njia pekee ya kuijenga nchi yetu ni kufanya kazi
kwa bidii, kulipa kodi kwa hiari na kufichua wakwepa kodi wote na wala rushwa.
(iii)
Tatu, ujenzi wa uchumi wa viwanda
unahitaji wananchi wenye afya njema na maarifa ya kufanya kazi na ubunifu. Tujenge utamaduni wa kupima afya zetu na
kufanya mazoezi ya viungo ili kuepuka magonjwa yasiyo ya kuambukiza ambayo
yanapoteza nguvu kazi kubwa ya Taifa;
(iv)
Nne, rasilimali tulizonazo ipo siku
zitaisha. Hivyo ni wajibu wa kila mmoja wetu kuzitumia kwa uangalifu ili
zitufae sisi na vizazi vijavyo. Tuepuke
matumizi mabaya ya rasilimali zetu kama vile maji, madini na misitu ili
zinufaishe kizazi hiki na vizazi vijavyo;
(v)
Tano, tuongeze nidhamu na uwajibikaji
katika kila jambo la maendeleo tunalolifanya na kuzingatia matumizi ya muda. Tamaduni
na mila zinazohamasisha uvivu na uzembe ni lazima tuzipige vita kwa nguvu zetu
zote; na
(vi)
Mwisho, dawa za kulevya ni janga kubwa
linaloitafuna kwa kasi nguvukazi ya nchi yetu. Tunahitaji ushiriki wa kila
mmoja katika vita hii kwa kufichua mtandao wa wahusika wa dawa za kulevya. Ahadi yetu ni kuwapa ushirikiano na kuchukua hatua kali
dhidi ya wote waliohusika.
MAKADIRIO YA MAPATO NA MATUMIZI YA FEDHA ZA OFISI YA WAZIRI MKUU NA OFISI YA BUNGE KWA MWAKA 2017/2018
87.
Mheshimiwa Spika, kwa mwaka
2017/2018, Ofisi ya Waziri Mkuu na Taasisi zilizo chini yake inaliomba Bunge
lako Tukufu liidhinishe jumla ya Shilingi
Bilioni Mia Moja Sabini na Moja; Milioni Mia Sita Sitini na Nne, na Hamsini na
Tano Elfu (Sh.171,664,055,000). Kati ya fedha hizo, Shilingi Bilioni Sabini na
Nne, Milioni Mia Sita Arobaini na Tatu, na Mia Tatu Thelathini na Tisa Elfu
(Sh.74,643,339,000) ni kwa ajili ya Matumizi ya Kawaida na Shilingi Bilioni Tisini na Saba, Milioni
Ishirini, na Mia Saba na Kumi na Sita Elfu (Sh.97,020,716,000) ni kwa ajili ya Matumizi ya Maendeleo.
Vilevile, ninaliomba Bunge
lako Tukufu liidhinishe jumla ya Shilingi
Bilioni Mia Moja Ishirini na Moja, Milioni Mia sita Hamsini na Mbili na Mia
Mbili Sitini na Mbili Elfu (Sh.121,652,262,000) kwa
ajili ya Mfuko wa Bunge. Kati ya fedha hizo, Shilingi Bilioni Mia Moja Kumi na Nne, Milioni Mia Nne Hamsini na Mbili,
na Mia Mbili Sitini na Mbili Elfu (Sh.114,452,262,000) ni kwa ajili ya
Matumizi ya Kawaida na Shilingi Bilioni
Saba na Milioni Mia Mbili (Sh.7,200,000,000) ni
kwa ajili ya Matumizi ya Maendeleo.
88.
Mheshimiwa Spika, naomba kutoa
hoja.
Hakuna maoni :
Chapisha Maoni