Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi wa Pili kutoka Kulia akiwasili katika Kijiji cha Kibaoni alipozaliwa Waziri Mkuu Mstaafu wa Tanzania Mh. Mizengo Peter Pinda kuwafariji Wananchi wa Kijiji jirani cha Kasansa waliokumbwa na mafuriko usiku wa kuamkia Tarehe 31 Machi.
Wa kwanza kulia ni Mkuu wa Mkoa Mjini Magharibi Mh. Ayoub Mohamed Mahmoud, kulia ya Balozi Seif ni Waziri Mkuu Mstaafu wa Tanzania Mh. Mizengo Peter Pinda, Naibu Waziri Wizara ya Nchi Ofisi ya Makamu wa Pili Mh. Mihayo Juma N’ hunga na nyuma ya Mh. Ayoub ni Mkurugenzi wa Uratibu Ofisi ya Makamu wa Pili Ng. Khalid Bakar Amran.
Kikundi cha Utamaduni na Kilimo cha Lalamayo Kwenye Kijiji cha Kibaoni kikitoa burdani wakati wa Ziara ya Balozi Seif ya kuwafariji wananchi wa Kijiji cha Kasansa waliopata mafuriko ya mvua.
Baadhi ya Wananchi wa Kibaoni wakimsikiliza Balozi Seif ambae hayupo pichani wakati akiwafariji kufuatia Mvua kubwa iliyowaletea maafa.
Balozi Seif akiwahutubia Wananchi wa Kibaoni na Vijiji jirani alipofika kuwafariji kufuatia mvua kubwa iliyosababisha Vifo,Nyumba pamoja na na mifugo kuathirika.
Ujumbe wa Viongozi wa Zanzibar uliokuwepo Mkoani Katavi ukicheza Ngoma ya Utamaduni ya akina mama ya Zinduka Mama Kwnye uwanja wa ndege wa Mpanda Mkoani Katavi ukijitayarisha kurejea Zanzibar.
Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imetoa mkono wa pole kwa Wananchi wa Kijiji cha Kasansa Wilaya ya Mlele Mkoani Katavi kufuatia mafuriko makubwa ya Mvua yaliyosababishwa na Upepo mkali ilioacha maafa Kijijini humo.
Inakisiwa kwamba Wananchi wapatao Sita wamefariki Dunia na wengine 47 kujeruhiwa kutokana na janga hilo akiwemo Mtoto wa skuli ya Maandalizi, Nyumba 27 kubomolewa kabisa pamoja na Mifugo kadhaa kusombwa na mafuriko hayo.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alitoa salamu za mkono wa pole alipofanya ziara maalum ya kuwafariji Wananchi hao wakati akizungumza kwenye Mkutano wa hadhara uliofanyika katika Skuli ya Msingi ya Kakuni katika Kijiji cha Kibaoni Mkoani Katavi.
Balozi Seif alisema maafa hayo yamemgusa kila Mtanzania kiasi kwamba Wananchi wote wanalazimika kuwaunga mkono katika kuwapunguzia machungu yaliyowakumba.
Aliwataka waathirika wote wa Kijiji cha Kasansa kuwa na moyo wa subra na wale waliojeruhiwa mwenyezi mungu atawaponyesha haraka ili warudi katika harakati zao za kimaisha kama kawaida.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar alisema katika kuungana na Wananchi hao ameahidi kuchangia shilingi Milioni 5,000,000/- ili zisaidie yale mambo ya msingi ambayo wananchi hao wanahitaji kuyapata katika kipindi hichi kigumu ya maafa.
Aliwataka Wananchi hao wa Wilaya ya Mlele hasa Wakulima waendelee na msimamo wao wa kuimarisha sekta ya kilimo ili kuwa na mazao ya kutosha na kupata ya ziada licha ya mashamba yao kukumbwa na mafuriko hayo.
Akigusia suala la Muungano Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar aliwataka Wananchi hao kuwa makini katika kuendelea kuulinda na kuudumisha Muungano wa Tanganyika na Zanzibar uliozaa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania.
Alisema ni vyema kwa Watanzania wote wakaelewa kwamba atakayeta kuudhofisha Muungano huo ahesabiwe kuwa ni adui wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania.
Balozi Seif alimpongeza na kumshukuru Waziri Mkuu Mstaafu wa Tanzania Mh. Mizengo Pinda kwa moyo na jitihada zake kubwa alizochukuwa za kukubali kuwatumikia Wananchi wa maeneo hayo wakati alipokuwa Mbunge wao.
Alisema Mh. Pinda anastahiki kuendelea kuheshimiwa kutokana na kazi kubwa anayoendelea kuifanya ya kuwatumiakia wananchi wa lililokuwa Jimbo lake licha ya kwamba wakati huu ameshastaafu utumishi wa Umma.
Mapema Mkuu wa Wilaya ya Mlele Bibi Recha Kasanga alisema Wataalamu wa Masuala ya Maafa na Mazingira wa Wilaya ya Milele pamoja na Mkoa wa Katavi wanaendelea kufanya tathmini ya maafa ya mafuriko yao ili kujua hasara sahihi iliyotokea.
Bibi Recha alisema hatua hiyo itatoa nafasi kwa Serikali kuangalia njia na maarifa ya kuwasaidia Wananchi hao pamoja na kuangalia jinsi ya kurejesha baadhi ya miundombinu iliyoharibiwa na maafa hayo.
Alisema zipo changamoto nyengine zinazoikabili Wilaya ya Mlele likiwemo suala la mauaji ya mara kwa mara yanayotokana na wivu wa mapenzi, uchawi na baadhi ya matukio ya ujambazi.
Bibi Recha alisema hata hivyo juhudi zimeendelea kuchukuliwa na Serikali ya Wilaya kwa Kushirikiana na Kamati ya Ulinzi na Usalama katika kujaribu kukabiliana na mtandao wa majambazi unaoleta taharuki katka baadhi ya Vijiji.
Akitoa salamu katika Mkutano huo wa Hadhara hapo Kibaoni Waziri Mkuu Mstaafu Mh. Mizengo Peter Pinda alisema amelazimika Kuongeza ujenzi wa Madarasa mengine Sita zaidi na kufikia 26 ya Skuli Mpya ya Kakuni anayojenga ili ikidhi mahitaji halisi ya sasa.
Mh. Pinda alisema ongezeko la idadi ya wanafunzi kwenye skuli hiyo ya Wanafunzi 600 kwa madarasa saba ya mwanzo limetokana na hamasa kubwa ya wazazi kuamua kuwapeleka watoto wao kupata elimu ya maandalizi na msingi.
Mkoa wa Katavi ulioasisiwa mwaka 2012 ukiwa na idadi ya wakaazi zaidi ya Laki Sita umebahatika kuwa na ardhi yenye rutba kubwa inayoweza kutoesha mazao mbali mbali pamoja na kushika nafasi ya Tatu ya hifadhi ya Taifa.
Othman Khamis Ame
Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar
Hakuna maoni :
Chapisha Maoni