Sheha wa Shehia ya Jang’ombe Bwana Khamis Ahmada akielezea faraja ya Wananchi wa Shehia hiyo kufuati ujio wa Viongozi mbali mbali katika kuzifariji Familia za Watoto Wanne waliokutwa wamefariki kwenye Gari mapema wiki hii. Bwana Ahmada alitoa shukrani hizo mbele ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi wa Pili kutoka Kulia aliyekaa chini akitanguliwa na Mwakilishi wa Jimbo la Jang’ombe Mheshimiwa Abdula Diwani. Picha na – OMPR – ZNZ.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi amezitaka Familia za Watoto Wanne waliofariki Dunia baada ya kukutwa kwenye Gari mapema wiki hii katika Mtaa wa Kidongo Chekundu Mjini Zanzibar kuendelea kuwa na moyo wa subra katika kipindi hichi kigumu cha msiba.
Alisema Jamii kupotelewa na watoto Wanne ni jambo zito linalotia huzuni lakini jamii hiyo hiyo inalazimika kuelewa kwamba Allah amewapenda zaidi Watoto hao Malaika za Mungu.
Balozi Seif Ali Iddi alitoa nasaha hizo wakati alipofanya ziara fupi ya kutoa mkono wa pole pamoja na kuzipa faraja familia za Watoto hao hapo katika Mtaa wa Kidongo chekundu Mkoa Mjini Magharibi.
Alisema tukio hilo la kusikitisha lililopokelewa kwa huzuni ya Serikali Kuu litaendelea kubakia Historia ndani ya nyoyo za Wananchi walio wengi katika Maeneo mbali mbali Nchini.
Kufuatia tukio hilo la maafa, Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar ameliagiza Jeshi la Polisi kufanya uchunguzi wa kina wa tukio hilo ili Serikali ipate kujiridhisha baada ya kupokea taarifa zenye mchanganyiko wa maelezo kutokana na mazingira ya vifo vya Watoto hao.
Balozi Seif ameendelea kuwasisitiza Wananchi na Wazazi wote Nchini kuwafuatilia Watoto wao katika mazingira yao ya kila siku ili kuwaepusha watoto kukumbwa na vitendo viovu pamoja na majanga yanayoweza kuepukika.
Mapema Sheha wa Shehia ya Jang’ombe Bwana Khamis Ahmada alisema Wazazi na Wananchi wa Mtaa huo walikusanyika pamoja baada ya kubaini utoekaji wa Watoto hao mapema asubuhi.
Sheha Ahmada alimueleza Balozi Seif kwamba Timu hiyo ilianza harakati za kuwatafuta Watoto hao kuanzia majira ya saa Tano za Asubuhi na hatimae kufanikiwa kuwagundua ndani ya gari wakiwa tayari wameshafariki Dunia.
Bwana Khamis Ahmada kwa niaba ya Wananchi wa Shehia hiyo na Vitongoji vyake ameishukuru Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa imani ya Viongozi wake wa ngazi mbali mbali kujitokeza kwa wingi katika kutoa faraja na mkono wa pole kwa familia ya Watoto hao.
Bwana Ahmada alisema kitendo hicho cha kiutu na cha kiungwana kwa kiasi kikubwa kimeleta faraja, upendo pamoja na kupunguza machungu kwa wananchi waliopatwa na mtihani huo.
Othman Khamis Ame
Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar
20/7/2017.
Hakuna maoni :
Chapisha Maoni