.

.

.

.

.

.

.

.
KARIBUNI TUHABARIKE, TUELIMISHANE, TUPEANE HABARI ZA KUKUFANYA UTABASAMU KIDOGO NA MATUKIO YALIYOFANYIWA UCHUNGUZI WA KINA TOKA KILA PEMBE CONTACTS: +255 787 377 722 Email: drweyunga@gmail.com PIA UNAWEZA KUNI FOLLOW KUPITIA INSTAGRAM YANGU @drweyunga | TANGAZA NASI ILI UWAFIKIE WATU WENGI ZAIDI.

Jumatatu, 17 Julai 2017

BENKI YA KILIMO KUFANYA KAZI NA MKOA WA SIMIYU

IMG_0100
Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mhe.Anthony Mtaka akizungumza katika kikao kilichofanyika Mjini Bariadi kati ya uongozi wa Mkoa huo, wataalam wa kilimo, mifugo na ushirika na Uongozi wa Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania.
IMG_0101
Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania (TADB), Francis Assenga akizungumza na Uongozi wa Mkoa wa Simiyu pamoja na wataalam wa Kilimo, ushirika na Mifugo (hawapo pichani) Mjini Bariadi.
IMG_0102
Mkurugenzi wa Biashara na Mikopo, Augustino Matutu Chacha wa Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania(TADB), akizungumza na Uongozi wa Mkoa wa Simiyu pamoja na wataalam wa Kilimo, ushirika na Mifugo (hawapo pichani) Mjini Bariadi.
IMG_0103
Mkuu wa Idara ya kilimo wa Halmashauri ya Wilaya ya Busega Juma Chacha akichangia katika kikao kilichofanyika katika uongozi wa Mkoa wa Mkoa wa Simiyu na Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania(TADB) Mjini Bariadi.
IMG_0104
Mkuu wa Idara ya Kilimo wa Halmashauri ya Wilaya ya Bariadi, Wilbert Siogopi akichangia katika kikao kilichofanyika kati ya Uongozi wa Mkoa wa Mkoa wa Simiyu na Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania(TADB) Mjini Bariadi.
IMG_0105
Baadhi ya Wataalam na Wanahabari wakifuatilia masuala mbalimbali yaliyokuwa yakiwasilishwa katika kikao kilichofanyika Mjini Bariadi kati ya Uongozi wa Mkoa wa Simiyu na Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania(TADB).
IMG_0106
Baadhi ya Wataalam na Wanahabari wakifuatilia masuala mbalimbali yaliyokuwa yakiwasilishwa katika kikao kilichofanyika Mjini Bariadi kati ya Uongozi wa Mkoa wa Simiyu na Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania (TADB).
 
Na Mwandishi wetu, Simiyu

Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania (TADB) imeuhakikishia uongozi wa Mkoa wa Simiyu kuwa itafanya kazi kwa karibu katika kutoa fursa ya mikopo itakayowasaidia wakulima mkoani humo kulima kilimo chenye tija.

Akizungumza na Mkuu wa Mkoa wa Simiyu Anthony Mtaka pamoja na Wakurugenzi na Wataalam kilimo na umwagiliaji, ushirika na mifugo kutoka Halmashauri zote za Simiyu,Kaimu Mkurugenzi wa Banki hiyo Francis Assenga amesema wapo tayari kukopesha na kufanya kazi na Mkoa wa Simiyu kutokana na utayari wao na uwepo wa mwongozo elekezi wa shughuli za kilimo zilizofanyiwa utafiti.

Amesema Benki hiyo ambayo ina lengo la kuleta mapinduzi ya kilimo Tanzania imeridhia kutoa mikopo katika miradi ya kilimo kwa wakulima, vikundi vilivyosajiliwa, vyama vya ushirika na kupitia Benki na taasisi nyingine za kifedha ambazo zinaweza kuwakopesha wakulima, ili kukuza uchumi na kupunguza umaskini kwa wakulima mkoani humo.

Ameongeza kuwa ili kufanikisha azma ya Mkoa wa Simiyu ya kukifanya kilimo kuwa ni biashara na kukuza uchumi wa wakulima wake , Benki ya TADB itasaidia kutoa mikopo itakayoambatana na mafunzo ya kuwajengea uwezo wakopaji hususani wanawake na vijana.

Ameeleza kuwa benki yake imekwisha tenga kiasi cha shilingi milioni 650 kwa ajili ya mafunzo ya kuwajengea uwezo na Bil 42 za mkopo kwa wanawake na vijana, hivyo amezisisitiza Halmashauri za Mkoa wa Simiyu kuwahamasisha vikundi vya wakulima vilivyosajiliwa kuchangamkia fursa hiyo ya mikopo yenye riba ndogo na masharti nafuu.

Mkuu wa Mkoa wa Simiyu , Mhe. Anthony Mtaka amesema Mkoa wa Simiyu uko tayari kufanya kazi na Benki ya TADB kupitia vikundi vya uzalishaji, Halmashauri na Miradi mbalimbali inayotekelezwa mkoani humo, ikiwa ni pamoja na miradi ya umwagiliaji ya Mwamanyili Wilayani Busega ulio katika hatua ya upembuzi yakinifu na Mwasubuya wilayani Bariadi ambao uko katika hatua ya ujenzi wa miundombinu ya umwagiliaji.

“Tungehitaji kuwa Mkoa ambao kupitia Benki ya Maendeleo ya Kilimo tungetengeneza namna ambayo ingewasaidia wakulima na ikasaidia mikoa mingine kuja kuona maendeleo ya kilimo ambayo ni matokeo ya Serikali kuwekeza katika Benki ya Kilimo” amesema Mtaka.

“Sisi kama Mkoa tumejipanga, tumetoa Elimu ya utayari na
namna ya utekelezaji wa shughuli zote kwa wataalam wetu pamoja na wananchi na isitoshe tayari tumeshafanya utafiti na kuandaa mwongozo wa uwekezaji ndani ya mkoa, hivyo tunawakaribisha kuwekeza,” Amesema Mtaka.

Aidha Mtaka ameongeza kuwa Mkoa wa Simiyu unatekeleza Sera ya Uchumi wa Viwanda chini ya Kauli Mbiu ya “Wilaya Moja Bidhaa Moja Kiwanda Kimoja” ambapo hadi sasa kuna kiwanda cha chaki na maziwa na miradi mingine minne ya viwanda iko katika upembuzi yakinifu, hivyo benki inaweza kuwekeza katika miradi hii kwa kuwawezesha wakulima na wafugaji kuzalisha malighafi ya Viwanda hivyo au kuwa mdau katika viwanda hivyo.

Naye Mkurugenzi wa Biashara na Mikopo wa TADB Augustino Matutu Chacha amesema wamefurahishwa na utayari wa Mkoa wa Simiyu juu ya kuwawezesha wakulima na Benki hiyo iko tayari kutoa mikopo pia kwa wakulima wa zao la pamba ambao wanazalisha zaidi ya asilimia 60 ya pamba yote nchini ili izalishwe kwa wingi zaidi na katika ubora wa hali ya juu.

Chacha amesema wataalam wa kilimo wa Mkoa wa Simiyu kwa kushirikiana na wataalam wa benki ya Maendeleo ya kilimo Tanzania (TADB) watakutana ili kuona namna watakavyofanya kazi kwa pamoja ili mikopo itakayotolewa iweze kuwa wa manufaa kwa wakulima na nchi kwa ujumla.

Aidha amewaeleza Wakurugenzi wa Halmashauri zote kuwa, Halmashauri zinaweza kupatiwa mikopo ili ziweze kuendesha miradi ya kilimo itakayoweza kuwa vyanzo vipya vya mapato kwa Halmashauri zao.

Hakuna maoni :

Chapisha Maoni