.

.

.

.

.

.

.

.
KARIBUNI TUHABARIKE, TUELIMISHANE, TUPEANE HABARI ZA KUKUFANYA UTABASAMU KIDOGO NA MATUKIO YALIYOFANYIWA UCHUNGUZI WA KINA TOKA KILA PEMBE CONTACTS: +255 787 377 722 Email: drweyunga@gmail.com PIA UNAWEZA KUNI FOLLOW KUPITIA INSTAGRAM YANGU @drweyunga | TANGAZA NASI ILI UWAFIKIE WATU WENGI ZAIDI.

Jumatatu, 24 Julai 2017

MKE WA WAZIRI MKUU AWASIHI WANAFUNZI KUTOKATISHA MASOMO

MKE wa Waziri Mkuu Mama Mary Majaliwa amewasihi wanafunzi wa kike nchini kujiepusha na vitendo vinavyoweza kusababisha kukatisha masomo yao.

Amesema ni vema wanafunzi hao wakatumia muda wao vizuri kwa kusoma kwa mfululizo kutoka kiwango kimoja cha taaluma kwenda kingine.

Mama Mary aliyasema hayo jana (Jumapili, Julai 23, 2017) alipozungumza na wanafunzi wa shule ya Sekondari Vwawa wilayani Mbozi.

Mke wa Waziri Mkuu ambaye ameambatana na Waziri Mkuu Kassim Majaliwa katika ziara ya mkoa Songwe, aliwaasa wanafunzi hao kutumia wakati huu kwa kusoma kwa bidii na kujiepusha na vitendo viovu.

“Nawasihi mtumie muda huu kusoma kwa bidii ili muweke msingi imara kwa ajili ya kujenga maisha yenu ya baadae. Msikatishe masomo yenu.”

Mama Mary aliongeza kwamba “utumieni muda huu vizuri ili msije mkaujutia baadae, kwani wakati ni mali ukipita umepita.”

Alisema ni vizuri wakasoma hadi chuo kikuu na kwamba wasikimbilie kufanya mambo yasiyowahusu kwa sasa kwani mshika mawili moja lazima limponyoke.

Mke wa Waziri Mkuu alisema wanafunzi hao wakisoma hadi elimu ya juu watakuwa na uwezo wa kutambua jambo lipi ni jema na lipi ni baya.

“Kilichonifurahisha zaidi ni kwa sababu mimi pia ni mwalimu kwa hiyo inavyoona wanafunzi wako vizuri kama hivi nafurahi sana, hivyo nawaomba msome kwa bidii.”

Serikali imetunga sheria kali dhidi ya watu wanaosababisha watoto wa kike kukatisha masomo yao kwa kuwapa mimba au kuwaoa.

IMETOLEWA NA: 

OFISI YA WAZIRI MKUU, 
JUMATATU, JULAI 24, 2017

Hakuna maoni :

Chapisha Maoni