Mkurugenzi Idara ya Maendeleo ya Vijana ya Wizara ya Kazi Bibi Mwanaidi Mohamed Ali Kulia akipokea msaada wa vitu na vyakula kwa niaba ya Viongozi wa Taasisi za Kijamii uliotolewa na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi huko Kama Nje kidogo ya Mji wa Zanzibar.
Baadhi ya Vyakula na Vifaa mbali mbali vilivyotolewa na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi kwa Taasisi za Kijamii Nchini. Picha na – OMPR – ZNZ.
Mkurugenzi wa Idara ya Maendeleo ya Vijana ya Wizara ya Kazi, Uwezeshaji, Wazee, Vijana, Wanawake na Watoto Bibi Mwanaidi Mohamed Ali alisema makundi ya Watu wenye Mahitaji Maalum bado wanahitaji kuendelea kuungwa mkono na Jamii katika njia ya kujaribu kukabiliana na changamoto zao.
Alisema njia hiyo ikiwemo misaada ya Kibinaadamu, vifaa pamoja na Taaluma zinaweza kuwa chachu ya kuwaondoshea fikra potofu za kujihisi kwamba wanatengwa na Jamii iliyowazunguuka.
Bibi Mwanaidi Mohamed alisema hayo kwa niaba ya Wawakilishi wenzake wa Taasisi za Kijamii wakati alitoa shukrani baada ya kupokea msaada wa Vifaa pamoja na vyakula mbali mbali vilivyotolewa msaada na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar
Balozi Seif Ali Iddi hapo Kama Kaskazini Magharibi ya Mji wa Zanzibar.
Msaada huo wa Vifaa na Vyakula ikiwa ni utaratibu wa mara kwa mara wa kusaidia Makundi Maalum Nchini ni pamoja na Tende, Mchele, Unga wa ngano, Mafuta ya Kupikia, Sukari pamoja na Misahafu.
Bibi Mwanaidi alisema mahitaji ya Makundi maalum yanapaswa kuangaliwa mara kwa mara badala ya tabia ya baadhi ya watu wenye uwezo kuzingatia zaidi utoaji wa misaada yao wakati wa vipindi vya Siku kuu.
Mapema Naibu Katibu wa Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Bibi Fatma Abdulrahman Khatib alisema msaada huo wa vitu na vyakula umeelekezwa kwa watoto wanaolelewa kwenye Nyumba za Mayatima za Mombasa {SOS}, Mazizini pamoja na Wazee wa Sebleni na Welezo.
Bibi Fatma alisema msaada huo ulioelekezwa pia kwa Watu wanaoishi katika Nyumba za kurekebishia tabia { Sober House } umelenga kutoa huduma kwa Jamii ili iweze kujikidhi Kimaisha.
Hakuna maoni :
Chapisha Maoni