.

.

.

.

.

.
KARIBUNI TUHABARIKE, TUELIMISHANE, TUPEANE HABARI ZA KUKUFANYA UTABASAMU KIDOGO NA MATUKIO YALIYOFANYIWA UCHUNGUZI WA KINA TOKA KILA PEMBE CONTACTS: +255 787 377 722 Email: drweyunga@gmail.com PIA UNAWEZA KUNI FOLLOW KUPITIA INSTAGRAM YANGU @drweyunga | TANGAZA NASI ILI UWAFIKIE WATU WENGI ZAIDI.

Jumapili, 13 Agosti 2017

WAZIRI MKUU AKEMEA MAAFISA MISITU

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amekemea tabia ya kutoa vibali vya uvunaji mbao inayofanywa na maafisa misitu wa TFS ambao wako chini ya Wizara ya Maliasili na Utalii.

Ametoa onyo hilo leo mchana (Jumamosi, Agosti 12, 2017) wakati akizungumza na watumishi wa Halmashauri ya Wilaya ya Uyui kwenye mkutano uliofanyika kata ya Goweko, wilayani Uyui mkoani Tabora.

Waziri Mkuu alifikia hatua hiyo baada ya kumhoji Afisa Misitu wa Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) Bw. Juma Kazimoto na Afisa Misitu wa Wilaya, Bw. Jared Nzilorera na kubaini kuwa hawafanyi kazi kwa kushirikiana.

"Hapa kuna uvunaji mkubwa wa misitu. Je kuna mtu anafuatilia kama wanavuna kwa usahihi?" alihoji Waziri Mkuu.

Akijibu swali la Waziri Mkuu, Bw. Kazimoto alisema Uyui hakuna uvunaji lakini wanaovuna wanatoka Sikonge na kuja kuuza mbao Uyui.

Alipoulizwa Afisa Misitu wa Wilaya, ni kwa kiasi gani wanapeana taarifa na mwenzake wa TFS ambao wanaletwa na wizara, alitoa majibu ya kujichanganya hali iliyomfanya Waziri Mkuu aamue kukemea tabia yao ya kutoa vibali bila kuwahusisha wenzao wa Halmashauri.

"TFS mmejiingiza kwenye kuvuna misitu, na mnawaover-power DFOs (wale wa Halmashauri). Hawa walioko kwenye Halmashauri ndiyo wanaolinda misitu yote ambayo iko ndani ya wilaya husika."

"Tatizo hili liko nchi nzima, ni la ushindani kati ya maafisa misitu wa TFS na wale wa Halmashauri. Misitu yetu inakwisha sababu mnaimaliza nyie kwa kutoa vibali bila kuwashirikisha wenzenu.

Alimwagiza Kaimu Mkuu wa Wilaya ya Uyui, Bi. Queen Mlozi asimamie suala hilo. "DC wewe ni Mwenyekiti wa Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Wilaya, simamia jambo hili na usisitize utunzaji wa mazingira na upandaji miti," alisema.

Alisema ukataji miti ovyo umechangia kukauka kwa vyanzo vingi vya maji. "Mhandisi wa Maji anahangaika kuchimba visima lakini hakuti maji sababu miti imekatwa ovyo na ardhi tepetevu imekauka. Watumishi wote nendeni vijijini mkahamasishe utunzaji wa mazingira," alisema.

Kwa mujibu wa hali ilivyo sasa, kila mkoa una Afisa Misitu wa Mkoa, kila wilaya imeajiri Afisa Misitu wa Halmashauri, lakini Wizara pia imeajiri Maafisa wa Misitu kutoka TFS katika ngazi za mkoa na wilaya.
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
JUMAMOSI, AGOSTI 12, 2017.

Hakuna maoni :

Chapisha Maoni