MKUU wa Wilaya ya Nzega mkoani Tabora, Godfrey Ngapula amesema Sayansi na Teknolojia haiwezi kuepukika katika kilimo nchini.
Ngapula ameyasema hayo leo kwenye uzinduzi na kukabidhi mbegu bora za Mahindi ya Wema 2109, mihogo na Viazi lishe kwa ajili ya kuanzisha mashamba darasa katika vijiji vya Shila, Iyombo, Upungu, Lububu na Kapanga wilayani humo.
Mkuu huyo wa wilaya alisema ili kufanya kilimo chenye tija sayansi na teknolojia haiwezi kuepukika kutokana na changamoto mbalimbali zilizopo.
Alisema kilimo cha kisayansi kina tija kwani mkulima anaweza kulima eneo dogo na kupata mavuno mengi kuliko kilimo cha mazoea ambacho mkulima hulima shamba kubwa mazo kidogo.
Ngapula aliipongeza Tume ya Taifa ya Sayansi na Teknolojia (COSTECH) kwa kuwapelekea mbegu hizo kwa kushirikiana na Jukwaa la Bioteknolojia kwa Maendeleo ya Kilimo (OFAB)
Akizungumzia matumizi ya mbegu zilizozalishwa kwa teknolojia ya uhandisi jeni (GMO) alisema hayakwepeki kwa kuwa mbegu hizo zinasifa ya kukabiliana na changamoto mbalimbali ikiwemo ukame na wadudu waharibifu wa mazao.
Alisema wilaya hiyo kupelekewa mbegu hizo kwao ni fursa kubwa na kwa kushirikiana na wakulima na maofisa ugani atahakikisha mashamba darasa hayo yanatunzwa vizuri na kuwa ndio chanzo za kutoa mbegu nyingi na kuzisambaza katika maeneo mengine.
Mtafiti wa mazao ya mizizi kutoka Kituo cha Utafiti wa Kilimo cha Maruku mkoani Kagera, Jojianas Kibura aliwaambia wakulima hao kuwa hekta moja ya mihogo iwapo watalipa kwa kufuata ushauri wa wataalamu wataweza kupata tani 25 hadi 32 kwa zao la mihogo na viazi lishe watapata tani 7 hadi 9 kwa hekta moja.
Alisema matokeo hayo watayapata endapo watafuata kanuni bora za kilimo cha mazao hayo kwa kuzingatia nafasi kati ya mche na mche na mstari kwa mstari na matumizi ya mbolea hivyo wataweza kuongeza uzalishaji zaidi tofauti na sasa ambapo kwenye hekta moja ya mihogo wanapata tani nane hadi kumi wakati kwenye viazi lishe wanapata tani moja hadi 3.
Mtafiti huyo alisisitiza kuwa mbegu hiyo ya Mihogo ya Mkombozi imefanyiwa utafiti na kuonekana kustahimili magonjwa hatari ya mihogo ya batobato kali na michirizi ya kahawia ambayo imekuwa ikiwapatia hasara kubwa wakulima wengi na kupoteza hadi asilimia 90 za mazao.
Akizungumzia kuhusu mbegu Mwakilishi wa Kaimu Mkurugenzi wa COSTECH ambaye ni Ofisa Mwandamizi wa COSTECH, Audax Mutagwa, alisema mbegu hizo ya mihogo aina ya Mkombozi imefanyiwa utafiti na kuonekana ina uwezo mkubwa wa kustahimili magonjwa kama ya batobato kali na michirizi ya kahawia ambayo imekuwa ikiwapatia hasara kubwa wakulima na ya mahindi ikistahimili hali ya ukame na kutoa mazao mengi.
Mutagwa aliwaomba wakulima hao kuyatunza mashamba hayo ambayo yamegharimu fedha nyingi hadi kukamilika kwake hivyo wayaendeleze kwa ajili ya kuja kutoa matunda kwa wakulima wa wilaya hiyo na kupata chakula cha kutosha na ziada kuuza.
Aliongeza kuwa kazi kubwa ya COSTECH ni kuishauri serikali katika masuala mbalimbali ya sayansi na teknolojia na kuhakikisha matokeo ya tafiti zinazofanyika nchini yanawafikia walengwa ambao ni wakulima.
Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi ya Shila ambayo ni shule pekee iliyopata baada ya kuwa na shamba darasa la mihogo katika wilaya hiyo, Gunguti Awadh Mzee alisema shamba hilo litakuwa la mfano na kuwa mradi huo utasaidia kuwapatia wanafunzi wake chakula wakiwa shuleni hapo.
(Imeandaliwa na mtandao wa www.habari za jamii.com)
Hakuna maoni :
Chapisha Maoni