.

.

.

.

.

.

.

.
KARIBUNI TUHABARIKE, TUELIMISHANE, TUPEANE HABARI ZA KUKUFANYA UTABASAMU KIDOGO NA MATUKIO YALIYOFANYIWA UCHUNGUZI WA KINA TOKA KILA PEMBE CONTACTS: +255 787 377 722 Email: drweyunga@gmail.com PIA UNAWEZA KUNI FOLLOW KUPITIA INSTAGRAM YANGU @drweyunga | TANGAZA NASI ILI UWAFIKIE WATU WENGI ZAIDI.

Ijumaa, 17 Novemba 2017

MAJALIWA AAHIRISHA KIKAO CHA BUNGE

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akisoma hotuba ya kuahirisha kikao cha Tisa cha Bunge, bungeni Mini Dodoma Novemba 17, 2017. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akipongezwa na wabunge baada ya kusoma hotuba ya kuahirisha kikao cha bunge, bungeni mjini Dodoma November 17, 2017. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)

UTANGULIZI 

1. Mheshimiwa Spika, tarehe 7 Novemba, 2017 tulianza kikao cha kwanza cha mkutano wa tisa wa Bunge lako tukufu na leo tunafikia tamati. Ni jambo la kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kutuwezesha kuhitimisha kwa amani na afya njema shughuli zote zilizopangwa. 

2. Mheshimiwa Spika, napenda kutumia nafasi hii kukupongeza kwa hekima, busara na uwezo mkubwa wa kuliongoza Bunge hili ukisaidiwa na Mheshimiwa Naibu Spika na Wenyeviti wa Bunge. Vilevile, ninawashukuru Waheshimiwa Wabunge kwa kazi nzuri, michango, maoni na ushauri tulioupokea katika mkutano huu. 

3. Mheshimiwa Spika, wakati tukiendelea na kikao hiki cha Bunge, wapo baadhi ya Waheshimiwa Wabunge na wananchi tunaowawakilisha katika majimbo yetu walipata misiba ya ndugu, jamaa na marafiki. 

4. Mheshimiwa Spika, wakati Bunge lako likiendelea, tarehe 9 Novemba, 2017 tulipokea kwa masikitiko makubwa taarifa za vifo vya wanafunzi watano wa shule ya msingi Kihinga wilaya ya Ngara mkoani Kagera waliopoteza maisha kwa kulipukiwa na bomu wakiwa darasani. Katika tukio hilo, wanafunzi 43 na mwalimu mmoja walijeruhiwa. 

Aidha, tarehe 14 Novemba, 2017, Serikali ilipokea taarifa ya kaya 53 zenye wakazi 320 kutoka kijiji cha Kabegi, wilaya ya Musoma, mkoani Mara, walioathiriwa na maafa ya mvua na upepo mkali. Watu wanne walijeruhiwa na kupatiwa matibabu. Wakazi wote wamepata hifadhi kwa ndugu, na wamepata misaada ya kibinadamu ili waweze kujikimu kwa muda. 

5. Mheshimiwa Spika, vilevile, tumepoteza maisha ya watu 11 katika ajali ya ndege iliyotokea tarehe 15 Novemba, 2017 ambao walikuwa wakisafiri ndani ya ndege aina ya Cessna Grand Caravan wakitoka kwenye Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro (KIA) kwenda kwenye uwanja wa ndege wa Seronera uliopo kwenye Hifadhi ya Serengeti, mkoani Mara. 

6. Mheshimiwa Spika, matukio mengine yaliyowaathiri ndugu zetu ni mafuriko yaliyotokea Zanzibar ambapo watu wawili walipoteza maisha kwa kuangukiwa na ukuta katika eneo la Bububu, Magengeni. Aidha, wanafunzi watatu wa sekondari ya Ndyuda iliyopo katika mji mdogo wa Mlowo, mkoani Songwe walifariki dunia kwa kupigwa na radi katika kipindi cha hivi karibuni. 

Nitumie nafasi hii kuwapa pole, wale wote waliofikwa na misiba pamoja na maafa hayo. Vilevile, sote tunatambua kuwa walimu wote nchini ni zaidi ya asilimia 65 ya watumishi wa umma nchini. 

Mheshimiwa Dkt. John Pombe Joseph Magufuli, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, anawapa pole walimu wote kwa kufiwa na Katibu Mkuu wa Chama cha Walimu Tanzania (CWT), Bw. Yahaya Msulwa ambaye amefariki dunia jana katika Hospitali ya Aga Khan jijini Dar es Salaam alikokuwa akipatiwa matibabu. 

Tunatoa pole kwa mke wa marehemu pamoja na watoto. Check Against Delivery 2 PONGEZI 

7. Mheshimiwa Spika, tarehe 7 Oktoba, 2017 vilevile, Mheshimiwa Dkt. John Pombe Joseph Magufuli, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania alifanya mabadiliko katika Baraza la Mawaziri pamoja na kumteua Bw. Stephen N. Kagaigai kuwa Katibu wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. 

8. Mheshimiwa Spika, tarehe 27 Oktoba, 2017 Mheshimiwa Dkt. John Pombe Joseph Magufuli, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania alifanya uteuzi wa Makatibu Wakuu wapya, Naibu Makatibu Wakuu, Wakuu wa Mikoa pamoja na Mabalozi. 

9. Mheshimiwa Spika, katika mkutano huu, Bunge lako tukufu lilimuapisha Mheshimiwa Janeth Maurice Masaburi aliyeteuliwa tarehe 21 Oktoba, 2017 kuwa Mbunge na Mheshimiwa Dkt. John Pombe Joseph Magufuli, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. 

10. Nitumie fursa hii kuwapongeza Waheshimiwa wote kwa kuteuliwa kushika nyadhifa mbalimbali. Ninawatakia heri katika kutimiza majukumu yao mapya. MASWALI, MISWADA NA KAULI ZA SERIKALI 

11. Mheshimiwa Spika, katika mkutano huu, Waheshimiwa Wabunge wamepata fursa ya kuuliza maswali ya papo kwa papo kwa Waziri Mkuu, maswali ya kawaida ya msingi yapatayo 142 na maswali ya nyongeza 358 na kujibiwa na Serikali. Vilevile, Waheshimiwa Wabunge walipata fursa ya kujadili miswada minne na kupokea kauli mbili za Serikali. 

12. Mheshimiwa Spika, Miswada ya Sheria iliyojadiliwa na kupitishwa na Bunge lako tukufu ni: (i) Muswada wa Sheria ya Shirika la Mawasiliano Tanzania wa Mwaka 2017 (The Tanzania Telecomunications Corporation Bill, 2017); (ii) Muswada wa Sheria ya Marekebisho ya Sheria mbalimbali (Na. 4) wa Mwaka 2017 (The Written Laws (Miscellaneous Amendments - No.4), Bill, 2017); (iii) Muswada wa Sheria ya Wakala wa Meli Tanzania wa Mwaka 2017. (The Tanzania Shipping Agencies Bill, 2017). (iv) Muswada wa Marekebisho ya Sheria ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya wa Mwaka 2017. (The Drugs Control and Enforcement (Amendments) Bill, 2017). 

13. Mheshimiwa Spika, pamoja na kazi za msingi zilizopangwa, katika mkutano huu Waheshimiwa Wabunge walipata fursa ya kupata Kauli za Mawaziri ikiwemo kauli ya Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia kuhusu udahili na utoaji wa Mikopo kwa Wanafunzi wa Elimu ya Juu kwa mwaka 2017/2018 na kauli iliyotolewa na Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo kuhusu fursa kwa wasichana kujipima uwezo katika riadha ili waweze kuiwakilisha nchi yetu katika mashindano yajayo ya kimataifa ya Jumuiya ya Madola, Olimpiki, “All – Africa Games” na mengineyo. Check Against Delivery 3 MPANGO WA MAENDELEO NA MWONGOZO WA MPANGO NA BAJETI 

14. Mheshimiwa Spika, katika kukidhi matakwa ya Ibara ya 63(3)(c) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Ibara ya 94(1) ya Kanuni za Kudumu za Bunge lako tukufu, mnamo tarehe 7 Novemba 2017, Serikali iliwasilisha Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo unaokusudiwa kutekelezwa kwa mwaka 2018/19. Hoja hiyo ilijadiliwa kwa siku tano na kuhitimishwa tarehe 13 Novemba 2017. 

15. Mheshimiwa Spika, napenda pia kumshukuru Mheshimiwa Waziri wa Fedha na Mipango, Mheshimiwa Dkt. Philip Mpango (Mb.) na Naibu Waziri wa Fedha na Mipango, Mheshimiwa Dkt. Ashatu Kachwamba Kijaji (Mb.) kwa maelezo mazuri ya ufafanuzi waliyotoa wakati wa kuhitimisha hoja hiyo. Vilevile, nawashukuru Waheshimiwa Mawaziri wa Wizara za Kisekta kwa mchango mzuri waliotoa wakati wa mjadala wa hoja hiyo unaokusudiwa kutekelezwa na Serikali katika mwaka 2018/2019. 

Naamini mtakubaliana nami kwamba katika mjadala huo, tulipata darasa zuri ambalo limetupa uelewa mpana wa upangaji wa Mipango na Bajeti katika nchi yetu. 

16. Mheshimiwa Spika, Mpango wa mwaka 2018/19 utakuwa wa tatu katika mpangilio wa utekelezaji wa Mpango wa Maendeleo wa miaka mitano, ulioanza 2016/17 - 2020/21. Mpango huo utaendelea kutekeleza maeneo manne ya kipaumbele ya Mpango wa Maendeleo wa Miaka Mitano, yaani: 

(i) Viwanda vya kukuza uchumi na ujenzi wa msingi wa uchumi wa viwanda; (ii) Kufungamanisha ukuaji wa uchumi na maendeleo ya watu; 

(iii) Ujenzi wa mazingira wezeshi kwa uendeshaji biashara na uwekezaji; na 

(iv) Kuimarisha usimamizi wa utekelezaji wa Mpango. 

17. Mheshimiwa Spika, pamoja na mapendekezo ya mpango huo, uliwasilishwa pia Mwongozo wa Maandalizi ya Mpango na Bajeti kwa Mwaka 2018/2019. Mambo muhimu yaliyoainishwa katika Mwongozo ambayo yanapaswa kuzingatiwa kikamilifu na Maafisa Masuuli wote wakati wa maandalizi ya bajeti ya mwaka 2018/19 ni pamoja na haya yafuatayo: 

Moja: Ukusanyaji wa Mapato ya Ndani: Maafisa Masuuli wote wahakikishe kuwa makusanyo yote yanawekwa kwenye Mfuko Mkuu wa Serikali; Kuendelea kuboresha mifumo ya ukusanyaji wa mapato;

 Kuhakikisha zabuni za watoa huduma na makandarasi zinatolewa kwa wanaotumia mashine za kielektroniki; na kuhakikisha kuwa kampuni zote ambazo Serikali ina hisa zinaendeshwa kwa ufanisi na hivyo kutoa gawio stahiki kwa Serikali. 

Mbili: Kudhibiti Matumizi na Kupunguza Gharama: Maafisa Masuuli wote waendelee kufanya uhakiki wa watumishi ili kuhakikisha kuwa mishahara inalipwa kwa watumishi wanaostahili. Aidha, uhakiki wa kina uendelee kufanywa kwa waliokwama madaraja ili wapandishwe, na malimbikizo ya Watumishi yabainishwe na pia madeni ya Watumishi yawekwe vizuri ili kufikia hatua ya kuanza kulipa. 

Pamoja na hatua hiyo, maafisa masuuli waendelee kuchukua hatua za kupunguza matumizi ya Serikali kwa kufanya tathmini ya gharama za uendeshaji wa taasisi za Serikali ili kuchukua hatua stahiki, na kuhakikisha kuwa taasisi za Serikali zinazojiendesha kibiashara, zinapata faida na kuacha kutegemea ruzuku kutoka Serikali Kuu. 

Tatu: Kulipa na Kuzuia Ongezeko la Madeni ya Serikali: Maafisa Masuuli wote wahakikishe madai ya watoa huduma yote yamehakikiwa na Mkaguzi wa Ndani Mkuu Check Against Delivery 4 wa Serikali na kuingizwa kwenye hesabu za fungu husika, kutoingia mikataba ya miradi mipya bila kuwa na uhakika wa upatikanaji fedha; na Kuzingatia matumizi ya hati za ununuzi zinazotolewa kwenye Mfumo wa Malipo ili kudhibiti ulimbikizaji wa madai. 

18. Mheshimiwa Spika, uandaaji wa Mpango na Bajeti una mchakato na ratiba yake ya kila mwaka ambayo inapaswa kufuatwa na kuzingatiwa na wadau wote. Aidha, baada ya kupata maoni na ushauri wa Bunge kuhusu Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo na Mwongozo wa maandalizi ya Mpango na Bajeti kwa mwaka 2018/19, nitumie fursa hii sasa kuiagiza Wizara ya Fedha na Mipango kukamilisha kazi hii na kusambaza mwongozo wa maandalizi wa Mpango na Bajeti kwa Wadau wote ili kuwezesha Wizara, Mikoa, Mamlaka za Serikali za Mitaa na taasisi zote za umma zianze mchakato wa maandalizi wa Mpango na Bajeti wa Mwaka 2018/2019, kwa kuzingatia tuliyokubaliana. 19. Mheshimiwa Spika, napenda kutumia fursa hii kuwakumbusha viongozi na watendaji wote Serikalini kuzingatia kikamilifu Mwongozo wa Maandalizi ya Mpango na Bajeti ya Mwaka 2018/2019 ili kuendeleza mafanikio ya Serikali ya Awamu ya Tano. 20. Mheshimiwa Spika, naomba kutumia fursa hii kuwasihi Waheshimiwa Wabunge kwa nafasi zao kama Wajumbe wa Mabaraza ya Madiwani kwenye Halmashauri za Majimbo yao wawasaidie kutoa elimu na ufafanuzi kuhusu mchakato wa maandalizi ya Mpango wa Bajeti wakati wa Baraza la Madiwani. Aidha, napenda kutumia nafasi hii kuwaelekeza Wakurugenzi wa Halmashauri zote nchini wazingatie miongozo hii iliyotolewa na wawashirikishe wananchi na sekta binafsi katika kupanga Mipango ya Maendeleo ya maeneo yao. HALI YA UCHUMI 21. Mheshimiwa Spika, wakati wa mjadala wa mapendekezo ya Mpango wa Bajeti, zipo hoja zilizotolewa na Waheshimiwa Wabunge ambazo zilihitaji kupata ufafanuzi kuhusu mwenendo na hali ya uchumi nchini. Napenda kutumia fursa hii kulifahamisha Bunge lako tukufu kwamba viashiria muhimu vya uchumi jumla vinaonyesha kwamba mwenendo wa uchumi wetu ni wa kuridhisha. Kwa mfano, ukuaji wa uchumi katika robo ya kwanza ya mwaka 2017 ulikua kwa asilimia 5.7; robo ya pili ilikuwa asilimia 7.8 na nusu ya kwanza ya mwaka huu ilikuwa ni asilimia 6.8. Vilevile, kufuatia kuongezeka kwa makusanyo ya kodi na usimamizi thabiti wa matumizi ya Serikali, nakisi ya bajeti ya Serikali imeshuka na kufikia asilimia 1.9 kwa mwaka 2016/2017. Pia akiba ya fedha za kigeni inatosheleza kuagiza bidhaa na huduma nje ya nchi kwa zaidi ya kipindi cha miezi mitano (5); ikiwa ni zaidi ya lengo la miezi minne. 22. Mheshimiwa Spika, kwa upande wa kasi ya upandaji bei, takwimu zinaonyesha kwamba katika nusu ya mwaka 2017, mfumuko wa bei uliendelea kubaki katika kiwango cha tarakimu moja. Aidha, taarifa za hivi karibuni kutoka Taasisi ya Taifa ya Takwimu inaonyesha kwamba mfumuko wa bei nchini kwa mwezi Oktoba 2017 ulikuwa ni asilimia 5.1 ikilinganishwa na asilima 5.3 mwezi Septemba, 2017. Kupungua kwa kasi ya ongezeko la mfumuko wa bei mwezi Oktoba, 2017 kumechangiwa na kupungua kwa mfumuko wa bei wa bidhaa za vyakula, ambavyo vimepungua kutoka wastani wa asilimia 9.3 mwezi Septemba, 2017 hadi asilimia 8.8 mwezi Oktoba, 2017. Check Against Delivery 5 23. Mheshimiwa Spika, baadhi ya bidhaa za vyakula zilizochangia kupungua kwa mfumuko wa bei ni pamoja na mtama kwa asilimia 9.3, viazi mviringo asilimia 6.9, unga wa mtama asilimia 5.5; ndizi za kupika kwa asilimia 4.2, unga wa muhogo asilimia 2.2 na mbogamboga asilimia 1.7. 24. Mheshimiwa Spika, napenda kuwahakikishia Waheshimiwa Wabunge na wananchi wote nchini kuwa Serikali itaendelea kusimamia kwa karibu viashiria vya uchumi jumla ili kuwezesha hali bora ya maisha ya wananchi walio wengi hasa wa vijijini. UBORESHAJI WA MIUNDOMBINU Ujenzi wa Reli kwa Standard Gauge 25. Mheshimiwa Spika, Serikali imeanza utekelezaji wa ujenzi wa reli ya kati kwa kiwango cha Standard Gauge itakayokuwa na urefu wa Km. 1,219. Katika awamu ya kwanza ya ujenzi wa reli hiyo, mkataba wa ujenzi wa reli kutoka Dar es Salaam – Morogoro (Km. 205 na Km. 95 za njia za kupishana) ulisainiwa tarehe 3 Februari 2017 na ujenzi ulizinduliwa tarehe 12 Aprili 2017. Mkandarasi anayejenga reli hii ni kampuni ya Yapi Merkezi ya Uturuki yenye ubia na kampuni ya Mota-Engil Africa ya Ureno kwa gharama ya shilingi trilioni 2.73. Mradi huu unatarajiwa kukamilika Agosti, 2019. Aidha, kwa awamu ya pili ya ujenzi wa reli hiyo, kwa kipande cha kutoka Morogoro-Makutupora (Km 442 pamoja na njia za kupishana), mkataba wa ujenzi ulisainiwa tarehe 29 Septemba 2017 na mkandarasi ambaye ni kampuni ya Yapi Merkezi ameanza maandalizi ya kazi. Mradi huu unatarajiwa kukamilika ifikapo Septemba, 2020 kwa gharama ya shilingi trilioni 4.29. Mradi wa Bomba la Mafuta Ghafi kutoka Uganda (Hoima – Tanga) 26. Mheshimiwa Spika, Serikali imeanza utekelezaji wa Mradi wa Ujenzi wa Bomba la Kusafirisha Mafuta Ghafi la Afrika Mashariki kutoka Kabaale-Hoima (Uganda) hadi Bandari ya Tanga (Tanzania). Napenda kukujulisha kuwa maandalizi ya utekelezaji wa mradi huu yanaendelea vizuri ambapo hatua iliyofikiwa kwa sasa ni uwekaji wa jiwe la msingi ili kuanza rasmi ujenzi wa bomba. Uwekaji wa jiwe la msingi kwa upande wa Tanzania ulifanyika tarehe 5 Agosti 2017, katika eneo la Chongoleani lililopo katika Wilaya ya Tanga, Mkoa wa Tanga na Tarehe 11 Novemba 2017 katika eneo la Hoima kwa upande wa Uganda. 27. Mheshimiwa Spika, matokeo chanya kutokana na utekelezaji wa mradi huu yatakuwa ni pamoja na kuzalisha ajira za muda mfupi na za muda mrefu wakati wa ujenzi na katika kipindi chote cha uendeshaji. Ajira za moja kwa moja zinatarajiwa kuwa takribani 10,000 Katika kipindi cha ujenzi na takribani 1,000 katika kipindi cha uendeshaji. Mradi huu utahusisha mikoa minane (8) ya Kagera, Geita, Shinyanga, Tabora, Singida, Dodoma, Manyara, Tanga na Wilaya 24 pamoja na Vijiji 134 vya mikoa hiyo. Manufaa mengine ni pamoja na kuongeza kiwango cha biashara kati ya Tanzania na Uganda, kufunguka kwa biashara kwa ukanda wa Kaskazini (Northern Corridor), kuchochea shughuli za utafutaji wa mafuta hususan katika Ziwa Eyasi na Ziwa Tanganyika na kuongeza matumizi ya bandari ya Tanga hivyo kuongeza mapato katika bandari hiyo kwa takribani Dola za Marekani milioni 200 kwa kipindi cha miaka mitatu (3) ya ujenzi. Check Against Delivery 6 28. Mheshimiwa Spika, gharama za ujenzi wa mradi zinakadiriwa kuwa jumla ya Dola za Marekani bilioni 3.5, sawa na takribani shilingi trilioni 8.09 na utekelezaji wa mradi utachukua muda wa takribani miaka mitatu hadi kuanza kusafirisha mafuta. Mradi huu ulianza rasmi tarehe 12 Oktoba 2015 kwa kusainiwa kwa mkataba wa Makubaliano ya Awali (MoU) kati ya Serikali ya Tanzania na Serikali ya Uganda. Kampuni zinazotekeleza Mradi huu ni TOTAL (Ufaransa), CNOOC (China) na TULLOW (Uingereza). Mradi unatarajiwa kukamilika Mwaka 2020. Uboreshaji wa Bandari 29. Mheshimiwa Spika, Serikali imeendelea kuziboresha bandari za Dar es Salaam, Tanga, Bagamoyo na Mtwara ili kuziongezea ufanisi zaidi wa kuhudumia mizigo. Uboreshaji wa bandari ya Dar es Salaam utasaidia kuongeza usafirishaji wa mizigo kwenda nchi za jirani ambazo hazina bandari. Uboreshaji wa bandari ya Tanga utasaidia kuhudumia mradi wa mafuta pamoja na usafirishaji wa mizigo kwenda nchi jirani. Kwa upande wa bandari ya Mtwara, uboreshaji wake utasaidia huduma za usafirishaji wa gesi, chuma, makaa ya mawe na madini ya viwandani. Mradi wa Bandari ya Bagamoyo upo kwenye mpango wa Special Economic Zone (SEZ) inayojengwa kwa ubia kati ya China na Oman. HIFADHI YA MAZINGIRA 30. Mheshimiwa Spika, naomba uniruhusu nitumie nafasi hii kuzungumzia kidogo kuhusu suala la uhifadhi wa mazingira ambayo ni muhimu kwa nchi yetu. 31. Mheshimiwa Spika, Serikali ya Awamu ya Tano imeandaa mikakati mbalimbali ya kudhibiti na kukabiliana na changamoto ya uharibifu wa mazingira, hususan uharibifu wa vyanzo vya maji, matumizi yasiyo endelevu ya ardhi, misitu na bioanuai nyingine. Mikakati hiyo ambayo inatekelezwa na sekta zote ni pamoja na Mkakati wa Taifa wa kukabiliana na Mabadiliko ya Tabia Nchi, Mkakati wa Taifa wa hatua za haraka za kuhifadhi mazingira ya pwani, bahari, mito na mabwawa. Mikakati mingine ni Mkakati wa Taifa wa kupanda na kutunza miti, Mkakati na Mpango Kazi wa Taifa wa Hifadhi ya Bioanuai na Programu ya Taifa ya kukabiliana na kuenea kwa hali ya jangwa na ukame nchini. 32. Mheshimiwa Spika, ili kuhakikisha kwamba mikakati ya hifadhi ya mazingira inatekelezwa kwa ufanisi na tija, Serikali imeweka utaratibu maalum wa ushirikishwaji wa wananchi na Mamlaka za Serikali za Mitaa katika uhifadhi wa mazingira hasa kuhusu utunzaji wa vyanzo vya maji, uhifadhi wa maeneo ya pwani na fukwe, upunguzaji wa gesijoto pamoja na usimamizi na uhifadhi endelevu wa maliasili zikiwemo rasilimali za misitu, wanyamapori, viumbe wa majini na bioanuai zilizopo nchi kavu na baharini. Hizo ndio jitihada za kukabiliana na mabadiliko ya tabia nchi. 33. Mheshimiwa Spika, kutokana na utekelezaji makini wa Sera, Sheria na mikakati endelevu ya uhifadhi wa mazingira, Serikali ya Awamu ya Tano katika kipindi hiki kifupi imefanikisha mambo yafuatayo: Moja: Serikali imeongeza hamasa na ushirikishwaji mkubwa wa wananchi katika suala la usafi, utunzaji na uhifadhi wa mazingira katika maeneo yote ikiwemo makazi yao. Check Against Delivery 7 Hatua hiyo imetokana na ushiriki mkubwa wa Viongozi wa Kitaifa, Waheshimiwa Wabunge, viongozi wa mikoa na watendaji wa ngazi zote katika shughuli za usafi na uhifadhi wa mazingira. Mbili: Baraza la Taifa na Usimamizi wa Mazingira ambalo lipo chini ya Ofisi ya Makamu wa Rais limekubaliwa kuwa taasisi muhimu duniani ya kusimamia shughuli za Mfuko wa Kuhimili Mabadiliko ya Tabia Nchi (Adaptation Fund). Pamoja na mambo mengine hatua hiyo, imewezesha pia kupatikana kwa rasilimali fedha zaidi ya Dola za Marekani Milioni 100 kutoka Mfuko wa Dunia wa Mabadiliko ya Tabia Nchi kwa ajili ya utekelezaji wa mradi wa kutoa maji kutoka Ziwa Victoria na kuyapeleka katika Mkoa wa Simiyu. Tatu: Kikosi Kazi Maalum kilichoundwa na Serikali kimekamilisha kazi ya kuandaa mapendekezo ya Mkakati wa hatua za haraka na hatua za muda mrefu za kuongoa ikolojia ya bonde la mto Ruaha Mkuu ili kuhakikisha maji yanatiririka mwaka mzima kwenye mabwawa ya uzalishaji umeme ya Kidatu na Mtera na kwenye Hifadhi ya Taifa ya Ruaha. Nne: Ili kuimarisha ukaguzi wa masuala ya hifadhi ya mazingira nchini, Serikali imeongeza idadi ya Wakaguzi wa Mazingira (Environmental Inspectors) kutoka 62 hadi kufikia 512 kwa mwaka 2017. Aidha, Serikali imefanya ukaguzi wa Viwanda 380 Nchini kwa lengo la kufanya tathmini za mazingira pamoja na kutoa elimu na uelewa kuhusu uendeshaji endelevu wa viwanda kwa kuzingatia utunzaji bora wa mazingira. Vilevile, Serikali imetoa vyeti vya mazingira 1,500 kwa wawekezaji kwa ajili ya kuhakikisha uwekezaji endelevu. Tano: Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kushirikiana na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar imefanikiwa kufungua vituo viwili (2) vilivyoko eneo la Ras Mkumbuu huko Pemba na Mafia mkoani Pwani kwa lengo la kuwajengea uwezo wataalam wa maeneo husika kuhusu taarifa za ikolojia ya mawimbi, ukusanyaji wa taarifa za uchafuzi wa mazingira ya maeneo ya pwani na mmomonyoko wa fukwe. Sita: Ofisi ya Waziri Mkuu kwa kushirikiana na ofisi za kisekta imefanikiwa kuongeza usahihi wa taarifa za utabiri wa hali ya hewa. Tumefunga mitambo (AWS-36) jambo ambalo limesaidia kufanya utabiri kuwa sahihi kwa asilimia 82 hadi 87. Barani Afrika, vituo vya namna hii viko katika nchi mbili tu, ambazo ni Tanzania na Ethiopia. 34. Mheshimiwa Spika, mafanikio haya yametokana na uongozi thabiti wa Serikali ya Awamu ya Tano chini ya uongozi wa Mheshimiwa Dkt. John Pombe Joseph Magufuli, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambaye ameonyesha uongozi mahiri uliotukuka na wakupigiwa mfano barani Afrika na duniani kote, hasa kwa kuwa amedhihirisha kuwa ana dira, maono na kwamba anapenda Watanzania waweze kupata maendeleo endelevu na kuishi katika mazingira bora na tulivu. Aidha, napenda kutumia fursa hii kumpongeza Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan, Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa uongozi wake mahiri wa kumsaidia Mheshimiwa Rias ikiwa ni pamoja na kuhakikisha usimamizi makini wa masuala ya Hifadhi ya Mazingira unakuwa endelevu. SEKTA YA KILIMO Check Against Delivery 8 Mwelekeo wa Upatikanaji wa Mvua na Msimu wa Mvua za Vuli 35. Mheshimiwa Spika, msimu wa mvua za vuli ulioanzia mwezi Oktoba 2017 na sasa unaendelea hadi Desemba (vuli) ni mahsusi kwa maeneo yanayopata misimu miwili ya mvua kwa mwaka (Ukanda wa Ziwa Victoria, Nyanda za Juu Kaskazini Mashariki, Pwani ya Kaskazini na maeneo ya Kaskazini mwa mkoa wa Kigoma). 36. Mheshimiwa Spika, katika msimu huu, mvua zinatarajiwa kuwa za wastani katika maeneo mengi ya mikoa ya Kagera, Mara, Mwanza, Geita, Simiyu, Shinyanga, Dar es Salaam, Tanga, Pwani, Kilimanjaro, Arusha na Manyara, pamoja na Kaskazini mwa mkoa wa Morogoro. Napenda kutoa wito kwa wakulima wa maeneo hayo, watumie mvua hizi kulima mazao yanayoendana na msimu huu. 37. Mheshimiwa Spika, Serikali imechukua hatua mbalimbali za kuimarisha sekta ya kilimo ikiwa ni pamoja kuratibu kilimo, maandalizi, pembejeo (mbegu na madawa), kuimarisha ushirika, masoko na, kuimarisha Bodi za Mazao, pale palipo na Bodi. Vilevile, Serikali imekuwa ikitoa matamko ya kuwahimiza Maafisa Ugani na Maafisa Ushirika wasimamie kilimo cha mazao ya chakula na biashara kwenye maeneo waliyoko. Aidha, Maafisa Kilimo wamekuwa wakihimizwa kutoa elimu ya ugani na kuhimiza matumizi ya pembejeo zenye ubora. Vilevile, Serikali imekuwa ikitenga fedha za kuimarisha vituo vya utafiti vya kilimo kama vile Naliendele, Kilosa, Ukiriguru na Uyole. Pia Serikali imeondoa tozo mbalimbali zisizo na tija kwenye mazao ya biashara na chakula. 38. Mheshimiwa Spika, kumekuwa na malalamiko ya wakulima juu ya tatizo la masoko ya mazao ya tumbaku na mbaazi. Serikali imeendelea kutafuta masoko ya mazao hayo kwa kuzungumza na wafanyabiashara na kwa sasa suala la mbaazi bado tunawasiliana na Serikali ya India ili ikubali kununua mbaazi zote. Mazungumzo hayo yatakapokamilika, tutatoa taarifa. Kwa upande wa tumbaku, tumefanikiwa kuyapata makampuni mawili ya TGTS na Alliance One ambayo yako tayari kununua tumbaku iliyobaki kuanzia Jumanne ijayo, kwa sasa wanaratibu kufahamu vituo tumbaku ilipo ili wakaichukue. SEKTA YA ELIMU a) Hali ya Matokeo ya Darasa la Saba, 2017 39. Mheshimiwa Spika, mwaka huu tulikuwa na watahiniwa 916,885 wa shule za msingi waliosajiliwa kufanya mtihani wa kumaliza elimu ya msingi. Kati yao, watahiniwa 909,950 sawa na asilimia 99.24 ya waliosajiliwa, walifanya mtihani. Watahiniwa 6,935 sawa na asilimia 0.76 ya wote waliosajiliwa hawakufanya mtihani kutokana na sababu mbalimbali, zikiwemo utoro na ugonjwa. Taarifa ya matokeo ya mtihani huo, inaonyesha kuwa watahiniwa 662,035 kati ya 909,950 waliofanya mtihani huo sawa na asilimia 72.76, ikilinganishwa na asilimia 70.36 kwa mwaka 2016, walikuwa wamefaulu. Hivyo kuna ongezeko la ufaulu kwa asilimia 2.4. 40. Mheshimiwa Spika, takwimu za matokeo zinaonesha kuwa ufaulu katika masomo ya Kiswahili, English Language na Hisabati umepanda kwa asilimia kati ya 4.25 hadi 10.05 ikilinganishwa na mwaka 2016. Napenda kutumia fursa hii kwanza kuwapongeza sana Walimu kwa kazi nzuri na pili kuwahimiza Wakuu wa Mikoa, Wakuu wa Wilaya, Wakurugenzi na watendaji wa sekta ya elimu wasimamie kikamilifu maendeleo ya taaluma katika maeneo yao ili ufaulu Check Against Delivery 9 uongezeke. Pia, nawapongeza wanafunzi waliofaulu kwenye mitihani yao. Ninawatakia heri wakapokwenda kujiunga na masomo yao ya sekondari. b) Uboreshaji wa Mazingira ya Kufundishia na Kujifunzia 41. Mheshimiwa Spika, Serikali imeendelea na uboreshaji wa miundombinu ya shule kwa lengo la kuimarisha mazingira ya kufundishia na kujifunzia. Mkakati wa kuimarisha miundombinu hii imejumuisha ujenzi, upanuzi na ukarabati wa shule za Serikali zilizojengwa na wananchi, maarufu kama shule za kata. Katika miaka miwili ya Serikali ya Awamu ya Tano ujenzi umefanyika wa madarasa, vyoo, mabweni, mabwalo, ofisi za walimu, nyumba, uzio wa shule, visima, maktaba na maabara katika shule mbalimbali za umma zenye mahitaji makubwa pamoja na ukarabati wa miundombinu mingine chakavu katika shule hizo. Napenda kutumia nafasi hii ya kipekee kuipongeza Ofisi ya Rais – TAMISEMI kwa kusimamia ukarabati wa miundombinu chakavu kwenye shule kongwe ili kuziwezesha kutumika kwa ufanisi zaidi. Pia niwapongeze viongozi wote wa Mikoa, Halmashauri za Wilaya kwa usimamizi thabiti wa Mipango ya Elimu kwenye maeneo yao. Malengo yetu ni kuhakikisha kuwa miundombinu hii inatumika vizuri na inadumu kwa muda mrefu. c) Maboresho katika Vyuo vya Elimu ya Juu 42. Mheshimiwa Spika, Serikali imekamilisha ujenzi wa mabweni mapya 20 kwa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam. Mabweni hayo yenye uwezo wa kulaza wanafunzi 3,840, yalizinduliwa tarehe 15 Aprili, 2017 na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. John Pombe Joseph Magufuli. Aidha, ujenzi wa maktaba inayoweza kuchukua wanafunzi 2,500 kwa wakati mmoja unaendelea kujengwa katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam na Serikali inakamilisha ujenzi wa jengo la mihadhara katika Chuo Kikuu Kishiriki cha Elimu Mkwawa. Jengo hili litakapokamilika litakuwa na uwezo wa kuchukua wanafunzi 1,200 kwa mkupuo. Vilevile, Serikali imekamilisha awamu ya kwanza ya ujenzi wa majengo ya Taasisi za Sayansi za Bahari, katika kijiji cha Buyu, Zanzibar. 43. Mheshimiwa Spika, Serikali imeendelea na juhudi za kuongeza wanafunzi wa fani ya udaktari kwa kukamilisha ujenzi wa majengo ya hospitali ya kufundishia ya Mloganzila iliyo chini ya Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili, ambayo itazinduliwa rasmi tarehe 22 Novemba, 2017 na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. John Pombe Joseph Magufuli. Aidha, ujenzi wa mabweni, madarasa, vyumba vya mihadhara, maabara, maktaba na ofisi za walimu katika Kampasi hii umeanza na utakamilika ndani ya miezi 18. 44. Mheshimiwa Spika, kupitia kuimarika kwa mahusiano yetu ya kidiplomasia kati ya mwaka 2016/17 na mwaka 2017/18, Serikali imeratibu upatikanaji wa wanafunzi wa Kitanzania wanaofadhiliwa kusoma nchi za nje hususani China (86), Uingereza (17), Misri (4), Korea (3), Urusi (13) na Thailand (2) ambapo baadhi ya wanufaika ni wahadhiri wa vyuo vikuu na taasisi nyingine za elimu ya juu nchini. Katika mwaka 2017/18, Serikali imepanga kusomesha wahadhiri 100 katika ngazi za shahada za umahiri na uzamivu ili kukabiliana na upungufu wa wahadhiri. Mwezi Septemba, 2017 Serikali ilitia saini makubaliano na nchi ya Hungary ambapo itakuwa inatoa ufadhili wa masomo kwa wanafunzi 30 kwa kipindi cha miaka mitatu kuanza mwaka 2018/2019. d) Maboresho ya Vyuo vya Ualimu nchini Check Against Delivery 10 45. Mheshimiwa Spika, Serikali imeendelea kujenga na kukarabati Vyuo vya Ualimu vya Kitangali, Ndala, Mpuguso na Shinyanga kwa thamani ya shilingi bilioni 36.47. Mradi huu utatekelezwa kwa miaka mitatu (2016/2017 - 2018/2019) na unalenga kuongeza fursa kwa wanafunzi wenye sifa kupata nafasi ya kujiunga na elimu ya ualimu. Ujenzi na ukarabati huu utasaidia kuongeza udahili katika vyuo vya ualimu vya Serikali kutoka wanachuo 20,535 katika mwaka 2017 hadi kufikia wanachuo 23,835 katika mwaka 2019; ikiwa ni ongezeko la wanachuo 3,300. 46. Mheshimiwa Spika, Serikali pia imefanya ukarabati mkubwa wa miundombinu ya kufundishia na kujifunzia pamoja na mabweni katika vyuo 10 vya ualimu, ambavyo ni Morogoro, Mpwapwa, Butimba, Kasulu, Songea, Tukuyu, Marangu, Kleruu, Korogwe na Tabora. Ukarabati huu umewezesha wanachuo 5,920 waliokuwa wanasoma Stashahada maalum ya Sayansi, Hisabati na TEHAMA katika Chuo Kikuu cha Dodoma kuhamishiwa katika vyuo hivyo. Ukarabati wa vyuo hivi uligharimu shilingi bilioni 11.9. 47. Mheshimiwa Spika, Serikali imeanza maandalizi ya awamu ya pili ya ukarabati wa vyuo saba vya ualimu vya Serikali. Vyuo hivyo ni Tandala, Nachingwea, Tarime, Kinampanda, Mandaka, Patandi na Ilonga. Aidha, Vyuo vya Ualimu vya Murutunguru, Kabanga na Mhonda vitajengwa upya kufuatia taarifa ya Wahandisi kubaini kuwa vyuo hivyo havifai kukarabatiwa kutokana na uchakavu mkubwa wa majengo yake. 48. Mheshimiwa Spika, Serikali ya Awamu ya Tano katika kipindi cha miaka miwili imetoa mafunzo kwa wakufunzi 249 wa masomo ya Sayansi na Hisabati ili waweze kufundisha masomo hayo kwa kutumia TEHAMA; imenunua na kusambaza kompyuta 370, kompyuta mpakato 20 na projekta 27 kwa vyuo vya ualimu 12 ambavyo ni Morogoro, Mpwapwa, Tabora, Mtwara Kawaida, Monduli, Butimba, Kleruu, Kasulu, Songea, Marangu, Korogwe na Tukuyu. Sambamba na hatua hiyo Serikali kupitia mradi wa ualimu itanunua vitabu na kuimarisha maktaba; kuimarisha maabara za TEHAMA; kuimarisha ufundishaji wa masomo ya Sayansi na Hisabati; kuimarisha ufundishaji wa walimu wa elimu ya awali na kupitia Mitaala ya Elimu Ualimu ili iendane na mahitaji ya sasa. Lengo la hatua hizi ni kuimarisha vyuo vya ualimu ili tuweze kupata walimu mahiri. SEKTA YA AFYA Watanzania wote kuwa na Bima ya Afya 49. Mheshimiwa Spika, Serikali kupitia Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) imeendelea kutekeleza mikakati ya kuhakikisha wigo wa wanufaika wa bima ya afya nchini inaongezeka. Hadi kufikia Septemba 2017, Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) ulikuwa unahudumia wanufaika 3,346,631 sawa na asilimia 7 ya Watanzania wote. Aidha, Mfuko wa Afya ya Jamii (CHF) ulikuwa na wanufaika 11,779,338 sawa na asilimia 24 ya Watanzania wote. Wananchi wanaonufaika na mpango wa bima ya afya nchini chini ya NHIF and CHF wamefikia 15,125,969 sawa na asilimia 31 ya Watanzania wote ikilinganishwa na asilimia 20 iliyokuwa mwaka 2014/15. Check Against Delivery 11 50. Mheshimiwa Spika, mafanikio hayo yanatokana na kuruhusu makundi mengi kujiunga na mifuko hiyo wakiwemo wajasiriamali, vikundi vya VICOBA, SACCOS, wavuvi, waendesha bodaboda, watoto wenye umri chini ya miaka 18, wanafunzi wa vyuo vya elimu ya juu, n.k. Serikali itaendelea kusisitiza wananchi wajiunge na bima hiyo. 51. Mheshimiwa Spika, Serikali pia kupitia Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya imeendelea kutekeleza mpango wa NHIF/CHF kwa wanawake wajawazito na watoto, kwa kushirikiana na Benki ya Maendeleo ya Ujerumani. Mpango huu una lengo la kupunguza vifo vya akinamama na watoto ili kwenda sambamba na utekelezaji wa Malengo ya Kimataifa ya Maendeleo Endelevu. Kwa kipindi cha Julai hadi Septemba 2017, wanawake 71,102 katika mikoa ya Mbeya, Tanga, Lindi, Mtwara na Songwe wamehudumiwa. Lengo ni kuwafikia wanawake 180,000 na hivyo kufanya jumla ya wanawake 905,938 wanufaike na mpango huo. 52. Mheshimiwa Spika, natoa wito wa viongozi wa Wizara ya Afya, Mkoa, Halmashauri na Waheshimiwa Wabunge katika kuhamasisha wananchi wajiunge na mifuko ya Bima za Afya (NHIF) na (CHF) katika majimbo yetu. Hali ya Upatikanaji wa Dawa nchini 53. Mheshimiwa Spika, hali ya upatikanaji wa dawa nchini imeendelea kuimarika katika Bohari ya Dawa (MSD) na vituo vya kutolea huduma za Afya. Hadi kufikia Oktoba, 2017 Serikali imetoa Shilingi bilioni 53 kwa ajili ya ununuzi wa dawa. Hii iliwezesha upatikanaji wa dawa muhimu (essential medicines) katika bohari kufikia asilimia 80. Aidha, taarifa zilizokusanywa kutoka Halmashauri mbalimbali nchini zinaonyesha kuwa, dawa muhimu (essential medicines) zinapatikana kwa wastani wa asilimia 91.4. Dawa hizi ni pamoja na za kutibu malaria, TB (Kifua Kikuu), maambukizi ya bakteria na (antibiotics), dawa za kupunguza makali ya UKIMWI (ARVs) na dawa za uzazi salama. 54. Mheshimiwa Spika, kwa upande wa upatikanaji wa dawa kwa ajili ya watu wanaoishi na VVU, napenda kulifahamisha Bunge lako tukufu kwamba, kwa mara ya kwanza Mfuko wa Udhamini wa Kudhibiti UKIMWI (AIDS Trust Fund) umetoa shilingi milioni 660 kwa ajili ya kununua dawa za Cotrimoxazole (Septrin) ambazo hutumika kutibu na kuzuia magonjwa nyemelezi (opportunistic infections) kwa watu waishio na virusi vya UKIMWI (WAVIU). Aidha, kiasi cha shilingi milioni 200 kimetolewa kwa mkoa wa Manyara kuchangia ujenzi wa kituo cha afya Mererani katika Halmashauri ya Wilaya ya Simanjiro, ambacho licha ya kutoa huduma nyingine za afya, kitatumika kutoa huduma za kufubaza VVU (ARVs) kwa WAVIU. Kituo hiki pia kitakuwa kitovu cha uelimishaji wa wananchi wote kujiepusha na maambuzi mapya ya VVU. Serikali inaendelea kuwahamasisha wadau wote wa maendeleo waliopo ndani na nje ya nchi waunge mkono juhudi za Serikali kuhakikisha kuwa malengo ya kutokomeza VVU na UKIMWI yanafikiwa. SEKTA YA KAZI NA AJIRA Uwezeshaji wa Wahitimu Check Against Delivery 12 55. Mheshimiwa Spika, Mpango wa Pili wa Maendeleo wa Taifa unatafsiri maelekezo ya Ilani ya Uchaguzi ya Chama cha Mapinduzi kwa kuweka maeneo mahususi ya kuwezesha vijana wawe na ujuzi stahiki wa kuajirika au kujiajiri katika soko la ajira la ndani na la nje ya nchi. Ili kuwezesha vijana hao wawe na ujuzi stahiki, katika mwaka wa fedha 2016/17, Serikali ilianza kutekeleza Programu ya Taifa ya Miaka Mitano ya Kukuza Ujuzi ambayo imejikita katika maeneo muhimu yafuatayo:- Moja: Kutoa mafunzo ya kukuza ujuzi kwa njia ya uanagenzi (Apprenticeship) ambapo mhusika anatumia asilimia 60 ya muda wa mafunzo akiwa kazini na asilimia 40 akiwa darasani. Mbili: Kutoa mafunzo ya ujuzi na uzoefu kazini (Internship) kwa wahitimu wa ngazi mbalimbali za elimu na mafunzo hususan wale wa vyuo vikuu. Mafunzo haya yanahusisha vijana waliohitimu ngazi mbalimbali za elimu ambao wanapatiwa fursa ya kujifunza kwa vitendo katika maeneo ya kazi ili wapate uzoefu wa kazi na kuwawezesha kuajiriwa au kujiajiri. Tatu: Kutoa mafunzo ya urasimishaji ujuzi uliopatikana nje ya mfumo rasmi wa mafunzo. Mafunzo haya yanahusisha kutambua watu wenye ujuzi uliopatikana katika mfumo wa mafunzo usio rasmi, kuwapa mafunzo kutokana na mapungufu yatakayobainika na kuwapatia vyeti. Kwa kutumia vyeti hivyo wanaweza kujiendeleza kielimu, kuboresha huduma wanazotoa na kutafuta ajira. Nne: Kutoa mafunzo ya kukuza ujuzi kwa walio makazini. Mafunzo haya yanalenga kujenga uwezo wa nguvukazi iliyoko kazini ili iendane na mabadiliko ya teknolojia na kufanya kazi kwa weledi zaidi ili kuongeza tija na ufanisi kazini na kuongeza uwezo wa ushindani wa nchi. Mafunzo haya yanawalenga walioajiriwa na wale waliojiajiri katika sekta rasmi na isiyo rasmi. 56. Mheshimiwa Spika, napenda kulitaarifu Bunge lako tukufu kuwa tangu tuanze kutekeleza programu hii katika mwaka wa fedha 2016/17, tumetoa mafunzo kwa jumla ya vijana 11,492 katika fani mbalimbali kupitia vyuo vya umma, binafsi na makampuni mbalimbali. 57. Mheshimiwa Spika, kati ya hao, vijana 3,000 wamepatiwa mafunzo ya kubuni na kutengeneza nguo kwa kutumia teknolojia za kisasa kupitia viwanda vya Tooku (Dar es Salaam) na Mazava (Morogoro). Taarifa tulizonazo zinaonyesha kuwa zaidi ya vijana 2,600 wameajiriwa na viwanda hivyo. 58. Mheshimiwa Spika, Aidha, katika mwaka huu wa fedha (2017/18) Serikali kwa kushirikiana na sekta binafsi imetoa fursa za mafunzo mbalimbali ya vitendo. Serikali imekutana na sekta binafsi kupitia Chama cha Waajiri Tanzania (ATE), Taasisi ya Sekta Binafsi Tanzania (TPSF) na Baraza la Taifa la Biashara (TNBC) na kukubaliana kuwa ifikapo Desemba, 2017 vijana wote wawe wamepatiwa fursa za mafunzo katika maeneo ya kazi. 59. Aidha, katika kujenga ujuzi wa vijana kushiriki kwenye shughuli za kilimo, tumeshirikisha Wakuu wa Mikoa yote na kuwaelekeza waandae maeneo ya kujifunzia vijana hao kwenye Halmashauri zote za mikoa yao. Tayari ofisi yangu imepokea maombi ya kushiriki kutekeleza programu ya kukuza ujuzi katika eneo la kilimo kwa kutumia teknolojia ya kitalu nyumba (Green Check Against Delivery 13 House) kutoka mikoa ya Kagera, Manyara, Ruvuma, Kilimanjaro na Shinyanga. Ofisi yangu imefika katika Halmashauri zote za mikoa hii ili kujiridhisha kuwa imetenga maeneo kwa ajili ya kujenga vitalu vyumba vya kufundishia. Mafunzo haya yataanza rasmi Desemba, 2017 katika Halmashauri zote zilizowasilisha maombi. 60. Mheshimiwa Spika, napenda nilihakikishie Bunge lako tukufu kuwa, Serikali itahakikisha, sekta zote za kipaumbele kama zilivyobainishwa katika Mpango wa Maendeleo wa Miaka Mitano, zinapata nguvukazi yenye ujuzi stahiki kukidhi mahitaji ya soko la ndani na nje ya nchi. Nichukue fursa hii kutoa wito kwa viwanda na taasisi mbalimbali zishirikiane na Serikali kutoa nafasi kwa vijana wetu kujifunza kwa vitendo katika maeneo ya kazi na kupata uzoefu na ujuzi stahiki. Tuna vijana wengi waliomaliza vyuo vikuu walioomba kushiriki mafunzo ya vitendo na kupata uzoefu wa kazi. Natoa wito kwa waajiri watoe nafasi kwa vijana wetu hawa kujifunza kwa vitendo. Serikali itaendelea kugharamia mahitaji ya msingi ya vijana hawa wakati wa mafunzo hayo. SEKTA YA ARDHI 61. Mheshimiwa Spika, Serikali kupitia Tume ya Taifa ya Mipango ya Matumizi ya Ardhi inatekeleza Mpango wa Taifa wa Matumizi ya Ardhi nchini na Sheria ya Upangaji Mipango ya Matumizi ya Ardhi, Sura 116. Katika utekelezaji wa Sheria na Mpango huo, hatua mbalimbali zimechukuliwa ikiwa ni pamoja na: Moja: Kuandaa Mipango ya Matumizi ya Ardhi ya Kikanda kama vile SAGCOT na Mpango wa Matumizi ya Ardhi Kanda ya Kaskazini. Mbili: Kutoa mafunzo kwa Halmashauri za Wilaya 110 kuhusu uandaaji, utekelezaji na usimamizi wa mipango ya matumizi ya ardhi nchini. 62. Mheshimiwa Spika, natoa wito kwa Wizara ya Ardhi kushirikiana na Halmashauri zote nchini kuhakikisha kwamba zinakuwa na mpango wa matumizi bora ya ardhi na kupima ardhi yote kwa kuzingatia mipango hiyo. SEKTA YA MALIASILI NA UTALII Uendelezaji Utalii 63. Mheshimiwa Spika, utangazaji utalii unaongozwa na Mkakati wa Miaka Mitano ya Utangazaji Utalii wa Nje (International Marketing Strategy 2013-2018) ambao ulitayarishwa kwa kushirikiana na sekta binafsi. Kwa mwaka 2016/2017, Wizara ilibaini vivutio vya utalii katika mikoa minne ya Rukwa, Katavi, Singida na Tabora kwa lengo la kuvitambua, kuviendeleza, kuvitangaza na kuvutia uwekezaji katika maeneo hayo. Katika kuongeza idadi ya watalii nchini, Wizara imeendelea kutekeleza shughuli mbalimbali ikiwa ni pamoja na kuboresha miundombinu kwa kukarabati kilometa 2,571.2 za barabara zilizopo ndani ya hifadhi. Juhudi hizi zimesaidia kupata ongezeko la watalii kutoka 1,137,182 mwaka 2015 hadi kufikia 1,284,279 mwaka 2016 sawa na asilimia 12.9; Kuongezeka kwa mapato yatokanayo na utalii kutoka Dola za Marekani bilioni 1.9 mwaka 2015 hadi kufikia Dola za Marekani bilioni 2 mwaka 2016. Check Against Delivery 14 64. Mheshimiwa Spika, Serikali ina mpango wa kuendeleza utalii Nyanda za Juu Kusini ambako kuna vivutio vingi vya utalii lakini pamekuwepo idadi ndogo ya watalii wanaotembelea ukanda huu ukilinganisha na ukanda wa Kaskazini. Katika kutekeleza hilo, Serikali imepokea Dola za Marekani milioni 150 kupitia mradi wa Resilient Natural Resource for Tourism and Growth (REGROW) ambao utaanza kutekelezwa kuanzia mwaka wa fedha 2017/2018. Lengo la mradi huu ni kuongeza mchango wa sekta ya utalii katika uchumi kwa kuongeza ubora wa vivutio vya utalii kwa kuboresha miundombinu ndani ya hifadhi, usimamizi wa maliasili na kuongeza faida kiuchumi kwa jamii zinazoishi kwenye maeneo kuzunguka hifadhi hizo. Hata hivyo, tunaimarisha matangazo ya vivutio kwa kuwaruhusu Wakuu wa Mamlaka za Mapori kuanza kutangaza vivutio vilivyo katika Mamlaka zao. Kazi hiyo watashirikiana na Bodi ya Utalii Tanzania (TTB) ambao wana jukumu la utangazaji. 65. Mheshimiwa Spika, ninamwagiza Waziri wa Maliasili na Utalii kuanzisha Mamlaka ya Fukwe za Bahari na Maziwa ili kutangaza utalii na kuendeleza fukwe zote ambazo hazina shughuli za kitalii. Fukwe za bahari ni eneo mojawapo ambalo likiendelezwa vizuri, linaweza kuwa kichocheo kikubwa cha kukuza uchumi. 66. Mheshimiwa Spika, katika jitihada za kukusanya mapato, Serikali imeboresha mifumo ya ukusanyaji kwa kutumia njia ya kielektroniki ambapo kwa Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro mapato yameongezeka kutoka shilingi bilioni 60.1 mwaka 2014/2015 hadi kufikia shilingi bilioni 102 mwaka 2016/2017. Natoa wito kwa Wizara ya Maliasili na Utalii iongeze kasi ya kuleta mabadiliko katika sekta nzima ya maliasili ili iweze kuchangia zaidi kwenye uchumi. SEKTA YA MIFUGO Upigaji chapa mifugo 67. Mheshimiwa Spika, utambuzi wa mifugo kwa njia ya chapa ya moto ni utekelezaji wa Sheria ya Utambuzi, Usajili na Ufuatiliaji Mifugo Sura Na 184 na Kanuni zake za Mwaka 2011 chini ya G.N. namba 362. Madhumuni ya Mfumo wa Utambuzi na Ufuatiliaji Mifugo kama yalivyoainishwa kwenye Sheria ni kudhibiti magonjwa ya mifugo na magonjwa yanayoambukiza binadamu kutokana na wanyama na hivyo kuboresha afya ya mifugo na jamii, kuimarisha biashara ya mifugo na mazao yake kulingana na mahitaji ya masoko ya ndani na kimataifa na udhibiti wa uhamishaji wa mifugo kiholela. 68. Mheshimiwa Spika, utambuzi wa mifugo unasaidia kutambua na kuboresha mbari (kosaafu) za mifugo, kudhibiti wizi wa mifugo na usafirishaji holela wa mifugo kutoka eneo moja kwenda lingine bila kufuata taratibu zilizopo na hivyo kuepusha migogoro baina ya wafugaji na watumiaji wengine wa ardhi. Aidha, utambuzi utawezesha Serikali kupata idadi ya mifugo hivyo kuiwezesha kupanga mipango ya kuendeleza sekta ya mifugo. Hatua za utekelezaji 69. Mheshimiwa Spika, utekelezaji wa zoezi la utambuzi wa mifugo upo kwenye hatua mbalimbali katika mikoa yote ambapo Mamlaka za Serikali za Mitaa 113 zimeanza utekelezaji wa zoezi hilo na zinaendelea. Hadi kufikia tarehe 15 Novemba 2017, jumla ya ng’ombe 5,939,328 Check Against Delivery 15 wamepigwa chapa ambayo ni sawa na asilimia 30 kati ya ng’ombe millioni 18,957, 227 ambao wana umri zaidi ya miezi sita. Idadi ya ngombe wanaostahili kupigwa chapa ni theluthi mbili ya mifugo yote iliyo nchini ambayo jumla yake ni 28,435,825. Sheria ya Ufuatiliaji na Utambuzi wa Mifugo inasisitiza kuwa ng’ombe na punda wenye umri wa kuanzia miezi sita na kuendelea ndiyo wanaostahili kupigwa chapa. Hadi kufikia tarehe 15 Novemba, 2017, mikoa ya Dodoma, Singida na Iringa imeonyesha mwitikio mzuri, ambapo katika Mkoa wa Iringa, ng’ombe 230,147 wamepigwa chapa kati ya 243,521 (asilimia 98), Singida ng’ombe 837,676 kati ya 1,016,630 (asilimia 82) na Dodoma ng’ombe 1,016,977 kati ya 1,331,308 sawa na asilimia 76. Mikoa ambayo inasuasua katika utekelezaji wa zoezi hili la upigaji chapa ni Arusha, Lindi, Mtwara, Tanga, Tabora na Shinyanga. 70. Mheshimiwa Spika, ng’ombe wanaofugwa kwa mfumo wa ndani (zero grazing) na katika mashamba rasmi ya mifugo wanakadiriwa kufikia 750,000. Hawa wanatambuliwa kwa njia ya hereni masikioni. Hadi kufikia tarehe 15 Novemba, 2017, jumla ya ng’ombe 23,486 walikuwa wamewekewa hereni katika mikoa ya Arusha (11,727); Kilimanjaro (4,577) na Mbeya (7,182). 71. Mheshimiwa Spika, wakati wa utekelezaji wa zoezi la utambuzi wa mifugo, kumekuwepo na changamoto za wadau kutokuwa na uelewa mpana kuhusu dhamira njema ya zoezi hilo. Mikakati ya kukabiliana na changamoto hizi ni pamoja na Serikali kuendelea kutoa elimu kuhusu malengo ya zoezi hili, ikiwa ni pamoja na kufanya vikao na wafugaji na wadau wengine katika ngazi ya Halmashauri, Tarafa, Kata na Vijiji. Ninatoa wito kwa Wizara ya Mifugo na Uvuvi washirikiane na mikoa na Halmashauri zikamilishe zoezi la upigaji chapa kwa haraka na kutoa elimu juu ya malengo ya chapa hizo. Kutenga ardhi ya mifugo 72. Mheshimiwa Spika, Serikali katika juhudi zake za kuhakikisha upatikanaji wa ardhi kwa ajili ya mifugo na kupunguza migogoro kati ya wakulima, wafugaji na watumiaji wengine wa ardhi imeendelea kutekeleza mikakati mbalimbali ikiwa ni pamoja na kuendelea kuandaa mipango ya matumizi bora ya ardhi na kutenga ardhi kwa ajili ya viwanda na uwekezaji. Serikali imeamua kupata suluhisho la kudumu katika migogoro ya wafugaji, wakulima na wahifadhi wa mapori kwa kuainisha mipaka katika maeneo tengwa kwa kuweka alama ili kuwaondolea kero wananchi pamoja na kuzuia mifugo kutoka nje ya nchi. Natoa wito kwa Wakuu Mkoa na Wilaya zinazopakana na nchi jirani kufanya doria mipakani na kwenye mapori kubaini mifugo iliyoingia nchini. HITIMISHO 73. Mheshimiwa Spika, nimalizie kwa kuwashukuru tena wote waliosaidia kufanikisha mkutano tunaomaliza leo. Shukrani za pekee ni kwako wewe Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Naibu Spika pamoja na Wenyeviti kwa kutuongoza vizuri katika kipindi chote cha mkutano huu wa tisa. Aidha, nawashukuru Waheshimiwa Wabunge wote kwa michango yao pamoja na watumishi wote wa Serikali waliosaidia kujibu maswali na kuwasilisha hoja za Serikali hapa Bungeni. Check Against Delivery 16 74. Mheshimiwa Spika, kipekee namshukuru Katibu wa Bunge, Dkt. Stephen Kagaigai pamoja na watumishi wote wa Ofisi ya Bunge kwa kufanikisha mkutano huu. Nawashukuru wale wote waliokuwa na jukumu la ulinzi na usalama ili kuhakikisha mkutano huu unafanyika na kumalizika salama. Napenda pia niwashukuru madereva wote kwa kutekeleza wajibu wao kwa ufanisi mkubwa. Ninawashukuru pia waandishi wa habari kwa kuhakikisha kuwa habari za hapa Bungeni zinawafikia wananchi kwa namna mbalimbali. Mwisho, niwashukuru wananchi wa Dodoma na hasa wa Manispaa ya Dodoma kwa ukarimu wao wa kutupatia huduma zote muhimu na hivyo kukamilisha mkutano huu kwa mafanikio makubwa. 75. Nitumie nafasi hii sasa kuwatakia wote safari njema wakati mnarudi katika maeneo yenu ya kazi. Vilevile, niwatakie Watanzania wote sikukuu njema ya Maulid ambayo kwa mara ya kwanza itafanyika wilayani Ruangwa, mkoani Lindi; sikukuu njema ya Krismas na kheri ya Mwaka Mpya 2018. Ninamwomba Mwenyezi Mungu atuvushe sote salama na atufikishe mwaka 2018 ili tuweze kukutana tena katika Mkutano wa Kumi wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. 76. Mheshimiwa Spika, baada ya kusema hayo, naomba kutoa hoja kuwa Bunge lako tukufu sasa liahirishwe hadi siku ya Jumanne, tarehe 30 Januari, 2018 litakapokutana saa 3.00 asubuhi hapa mjini Dodoma. 77. Mheshimiwa Spika, naomba kutoa hoja.

Hakuna maoni :

Chapisha Maoni