Na Mwandishi Wetu, Mbeya
Wajumbe wa Jumuiya mbalimbali za Chama Cha Mapinduzi (CCM) wametakiwa kuchagua viongozi waadilifu, weledi na wenye maono ya kuziongoza Jumuiya hizo ila kuendana na kasi ya Mwenyekiti wa CCM Taifa ambaye pia ni Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Akizungumza wakati wa Mkutano Mkuu Maalumu wa Umoja wa Wanawake wa CCM Mkoa wa Mbeya uliokuwa na Ajenda ya uchaguzi wa viongozi wa Jumuiya hiyo Mkoa na Taifa, Mhe Mwanjelwa ambaye ni mjumbe Halmashauri kuu ya CCM Taifa, Naibu Waziri wa Kilimo Mhe Mary Mwanjelwa aliwasisitiza wajumbe hao kutochagua viongozi kwa matakwa ya urafiki na kujuana Bali kuchagua viongozi wa kazi watakaoisaidia jumuiya kuendana na mtazamo mpya wa CCM Mpya na Tanzania Mpya.
Mbali na kuwashukuru makada hao kwa kumchagua kuwa Mbunge wa Viti Maalumu Mkoa wa Mbeya jambo lililopelekea Mhe Rais John Pombe Magufuli kumteua kuhudumu nafasi muhimu ya Kuwa Naibu Waziri wa Wizara ya Kilimo, Mhe Mwanjelwa alisema kuwa serikali ya awamu ya tano ni ya kazi hivyo uchaguzi huo ni vyema kumalizika kwa kuwapata viongozi wachapakazi.
"Tunaelekea kwenye Mbeya Mpya, CCM Mpya, UWT Mpya na Tanzania Mpya hivyo msichague viongozi kutokana na makundi au watakaoendeleza makundi baada ya uchaguzi Bali chagueni viongozi shupavu na wachapakazi" Alikaririwa Mhe Mwanjelwa
Mhe Mwanjelwa (MNEC), alisema kuwa atafanya ziara katika maeneo mbalimbali ya Mkoa wa Mbeya ili kuangalia jinsi utekelezaji wa ilani ya CCM inavyotekelezwa.
Mkutano huo Maalumu ulimalizika kwa salama hapo Jana Novemba 28, 2017 katika Ukumbi wa Shule ya Sekondari Mbeya ambapo viongozi mbalimbali walichaguliwa katika ngazi ya Mkoa na Taifa.
Hakuna maoni :
Chapisha Maoni