Alisema mradi wa Tasaf ulioongeza chachu ya uzalishaji kwa Wananchi hao kutokana na kuanzishwa kwa miradi mingi ya uzalishaji utaendelea kuongezewa nguvu na Benki ya Dunia katika azma ya kuikomboa Jamii ya Watu wa kipato cha chini.
Bwana Michal Rutkowski alitoa kauli hiyo wakati wa mazungumzo yake na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi Vuga Mjini Zanzibar akiuongoza Ujumbe wa Viongozi wa Benki ya Dunia uliopo Zanzibar kukagua Miradi inayosimamiwa na kufadhiliwa na Taasisi hiyo ya Fedha ya Kimataifa kupitia Mfuko wa Tasaf.
Alisema uwajibikaji wa Wananchi wa Zanzibar hasa katika Miradi ya Kiuchumi umeongeza ushawishi kwa Benki ya Dunia kufikiria kuongeza nguvu zaidi za misaada ili kuona lengo lililokusudiwa la kuikomboa Jamii ya wanyonge linafanikiwa vyema.
Mkurugenzi huyo ambae pia ni Mkuu wa Mtandao wa Masuala ya Kijamii na Ajira wa Benki ya Dunia alizihakikishia Serikali zote mbili za Tanzania kwamba Taasisi hiyo itaendelea kuongeza nguvu katika kuona Miradi ya Wananchi wa kipato cha chini inaendelea kudumu kwa muda mrefu.
Aliipongeza Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa uamuzi wake wa busara iliyochukuwa wa kuwasaidia Wazee wenye Umri wa kuanzia Miaka 70 na kuendelea kwa kuwapatia posho Maalum ya kila Mwezi ili iweze kuwasaidia kupunguza ukali wa maisha.
Mapema Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alisema mabadiliko ya Sera ya Ustawi wa Jamii katika kuwapatia posho Wazee wa Zanzibar yamekuja kufuatia mchango mkubwa walioutoa Wazee hao wakati wa utumishi wao kwa Taifa.
Balozi Seif alisema Wazee wengi hasa wale waliotumikia Taifa kupitia Taasisi za Umma na hata zile Binafsi wana wajibu wa kuendelea kutunzwa na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ili kuwapa faraja kutokana na kazi yao kubwa waliyoifanya ya kujenga Taifa wakati wa Utumishi wao.
Akizungumzia Miradi ya Kijamii Balozi Seif alisema nia ya Serikali Kuu katika kuwajengea uwezeshaji Kiuchumi Wananchi hasa wale walioko katika mazingira magumu zaidi Vijijini umelenga kuwapunguzia ukali wa maisha.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar alimuahidi Mkurugenzi huyo wa Benki ya Dunia anayesimamia Mtandao wa Masuala ya Kijamii na Ajira kwamba Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar itaendelea kushirikiana na Taasisi hiyo katika kuona miradi iliyoanzishwa inafanikiwa vyema .
Wakati huo huo Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alikutana kwa mazungumzo na Uongozi wa Kamati Tendaji ya Taifa ya Jumuiya ya Maulid ya Milad - Nabee Ofisini kwake Vuga Mjini Zanzibar.
Katika mazungumzo yao Mwenyekiti wa Kamati ya Maandalizi ya Maulidi ya Mfuguo Sita Sheikh Sheral Chamsi alisema maandalizi ya Maulidi hayo yanayotarajiwa kufanyika Alhamis ya Tarehe 30 Novemba Mwaka huu katika Viwanja vya Maisara Suleiman yako katika hatua za mwisho za mafanikio.
Hata hivyo alisema endapo zitanyesha mvua siku hiyo ya Maulidi, sherehe hizo zitahamishiwa katika Msikiti Mkuu wa Ijumaa wa Mushawar uliopo Muembe Shauri Mjini Zanzibar.
Sheikh Sheral alisema matayarisho ya kuvipata vyuo vya Madrasa na Wanafunzi watakaosoma kasida kwenye sherehe hiyo yameshakamilika baada ya kufanya mchujo wa upatikanaji wake ulioshirikisha Wilaya zote za Unguja na Pemba ambapo Mwaka huu umeibua Madrasa ya Jojo Pemba na Tumbatu Gomani kwa upande wa Unguja.
Mwenyekiti huyo wa Kamati ya Maandalizi ya Maulidi ya Mfuguo Sita alimueleza Balozi Seif kwamba maandalizi ya mwisho ya Maulidi hayo yatafanyika baada ya sala ya Laasiri katika Msikiti Mkuu wa Ijumaa wa Muembe Shauri.
Akitoa shukrani zake kwa Kamati hiyo, Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi aliupongeza Uongozi wa Kamati hiyo kwa juhudi unazochukuwa wa kufanikisha maadhimisho ya Sherehe za Uzawa wa Mtume Muhammad {SAW} ambazo ni muhimu katika kuendeleza Dini ya Kiislamu.
Balozi Seif alisema Maulid yanaendelea kufanikiwa kila Mwaka na bado haijatokezea kasoro yoyote ile jambo ambalo limeonyesha umahiri wa Kamati hiyo katika utekelezaji wa Majukumu yake iliyopangiwa na Taifa.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar alieleza kwamba ushirikishwaji wa vyuo na Wanafunzi wa Madrasa tofauti Unguja na Pemba umeonyesha jinsi gani Maadhimisho hayo ya uzawa wa Mtume Muhammad {SAW} yanavyokubalika na Wumini wa Dini ya Kiislam katika maeneo mbali mbali Nchini.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi akizungumza na Uongozi wa Benki ya Dunia ukiongozwa na Mkurugenzi ambae pia ni Mkuu wa Mtandao wa Masuala ya Kijamii na Ajira wa Benki hiyo Bwana Michal Rutkowski Ofisini kwake Vuga Mjini Zanzibar.Balozi Seif akjibadilishana mawazo na Mkurugenzi ambae pia ni Mkuu wa Mtandao wa Masuala ya Kijamii na Ajira wa Benki hiyo Bwana Michal Rutkowski mara baada ya mazungumzo yao. Balozi Seif kati kati waliokaa Vitini akiwa katika picha ya pamoja na Uongozi wa Benki ya Dunia na Ule wa Ofisi yake mara baada ya mazungumzo yao ya pamoja Mkurugenzi Mtendaji wa Mfuko wa Maendeleo ya Jamii Tanzania { TASAF} Ladislaus Mwamanga kushoto akifafanua jambo mada baada ya mazungumzo ya pamoja kati ya Uongozi wa Benki ya Dunia na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi.
Wa kwanza kulia ni Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif na Mkurugenzi ambae pia ni Mkuu wa Mtandao wa Masuala ya Kijamii na Ajira wa Benki hiyo Bwana Michal Rutkowski. Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi wa kwanza kutoka Kushoto akipokea Taarifa ya matayarisho ya maashimisho ya sherehe za Maulidi ya Mfunguo Sita kutoka kwa Mwenyekiti wa Kamati ya Maandalizi ya Jumuiya ya Maulid ya Milad Nabee Sheikh Sheral Chamsi Ofisini kwake Vuga Mjini Zanzibar. Picha na – OMPR – ZNZ.
Othman Khamis Ame
Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar
9/11/2017.
9/11/2017.
Hakuna maoni :
Chapisha Maoni