.

.

.

.

.

.

.

.
KARIBUNI TUHABARIKE, TUELIMISHANE, TUPEANE HABARI ZA KUKUFANYA UTABASAMU KIDOGO NA MATUKIO YALIYOFANYIWA UCHUNGUZI WA KINA TOKA KILA PEMBE CONTACTS: +255 787 377 722 Email: drweyunga@gmail.com PIA UNAWEZA KUNI FOLLOW KUPITIA INSTAGRAM YANGU @drweyunga | TANGAZA NASI ILI UWAFIKIE WATU WENGI ZAIDI.

Jumatano, 13 Desemba 2017

BALOZI SEIF AKABIDHI VIFAA VYA MICHEZO KWA TIMU ZA WILAYA 11 ZA ZANZIBAR

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi akimkabidhi Waziri wa Habari, Utamaduni, Utalii na Michezo Zanzibar Rashid Ali Juma Kikombe cha mshindi wa kwanza wa mashindano ya ZBC Watoto Cup yanayotarajiwa kutimua vumbi Ijumaa ijayo.

Vifaa na zawadi hizo zimetolewa na Mfanyab iashara Maarufu Nchini ambae pia ni Mwakilishi wa Jimbo la Uzini Moh’d Raza.
Balozi Seif Ali Iddi akimkabidhi Waziri wa Habari, Utamaduni, Utalii na Michezo Zanzibar Rashid Ali Juma Kikombe cha msindi wa Pili wa mashindano ya ZBC Watoto Cuphafla iliyofanyika katika Ukumbi wa zamani wa Baraza la Wawakilishi uliopo Kikwajuni Mjini Zanzibar.
Balozi Seif akizungumza na wadau wa michezo kwenye hafla ya kukabishi zawadi, Vikombe pamoja na Vifaa kwa ajili ya Mashindao ya ZBC Watoto Mapinduzi Cup hapo Ukumbi wa zamani wa Baraza la Wawakilishi uliopo Kikwajuni Mjini Zanzibar.
Baadhi ya Viongozi wa Kamati ya Maandalizi ya ZBC Watoto Mapinduzi Cup pamoja na wadau wa Micheo wakifuatilia mambo mbali mbali yaliyojiri kwenye hafla ya kukabishi zawadi, Vikombe pamoja na Vifaa kwa ajili ya Mashindao ya ZBC Watoto Mapinduzi Cup.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alisema ubunifu uliofanywa na Shirika la Utangazi Zanzibar {ZBC} wa kuandaa Mashindano ya ZBC Watoto Mapinduzi Cup utalisaidia Taifa katika kuibua vipaji vya Soka kwaWatoto hapa Nchini.

Alisema wachezaji wengi wa Kimataifa na wale maarufu wanaotajikana kutokana na umahiri wao wa kusakata soka kwa vipindi vingi vilivyopita wamepata mafanikio hayo kutokana na jitihada zao binafsi bila ya msaada wa Taasisi yoyote kubwa.

Balozi Seif alitoa pongezi hizo wakati wa hafla fupi ya kukabidhi zawadi, Vikombe pamoja na Vifaa mbali mbali kwa Uongozi wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Utalii na Michezo kwa ajili ya Timu za Wilaya 11 za Zanzibar zitakazoshiriki mashindano ya ZBC Watoto Mapinduzi Cup yanayotarajiwa kuanza Ijumaa Ijayo katika Uwanja wa Aman Mjini Zanzibar.

Msaada huo uliokwenda sambamba na utolewaji wa vifaa kwa Timu zinazoshiriki Mapinduzi Cup Taifa vilivyotolewa na Mfanyabiashara maarufu ambae pia ni Mwakilishi wa Jimbo la Uzini Moh’d Raza hafla iliyofanyika katika Ukumbi wa zamani wa Baraza la Wawakilishi uliopo Kikwajuni Mjini Zanzibar.

Balozi Seif alisema Mataifa mbali Duniani hasa yale yaliyoendelea yamekuwa na utaratibu Maalum wa kuwaandaa Vijana wao baada ya kuwabaini Vipaji vyao tokea wakiwa katika skuli za Maandalizi na hatimae kuwa na wanamichezo mahiri wanaotajikana Kimataifa na kuyaletea sifa Mataifa yao.

Makamu wa pili wa Rais wa Zanzibar aliiushauri Uongozi wa ZBC Na Habari, Utamaduni, Utalii na Michezo kuuendeleza utaratibu huo na kuitaka jamii kuunga mkono jambo hilo zuri.

Mapema Mfanyabiashara Maarufu Nchini ambae pia ni Mwakilishi wa Jimbo la Uzini Moh’d Raza aliahidi kuendelea kusaidia sekta ya michezo ambayo iko ndani ya damu yake na kuelezea mategemeo yake katika kuona michezo inakuwa na kuimarika siku hadi siku hapa Nchini.

Raza aliwataka na kuwaomba Wafanyabiashara wenzake hapa Nchini kuunga mkono mashindao mbali mbali yanayoanzishwa Nchini yenye kulenga kuibua vipaji vya Vijana ili kuirejeshea Zanzibar hadhi yake ya Michezo Kimataifa.

Mkereketwa huyo wa Michezo alikabidhi Seti 11 kamili za Jezi kwa Kila Timu ya Wilaya itakayoshiriki mashindano hayo ya ZBC Wazoto Mapinduzi Cup, seti 11 za Mipira, Mipira Minne ya Mechi Vikombe vya Washindi wa Kwanza hadi Watatu pamoja na Medali za Dhahabu, Shaba na Fedha.

Akimkaribisha Mgeni Rasmi katika hafla hiyo Waziri wa Habari, Utamaduni, Utalii na Michezo Rashid Ali Juma alisema msaada wa mfanyabiashara huyo ni muhimu katika kudumisha Michezo ikiwa ni miongoni mwa mambo kukumbuka Mapinduzi Matukufu ya Zanzibar ya Mwaka 1964.

Rashid alisema Visiwa vya Zanzibar vimebarikiwa kuwa na Vijana wenye Vipaji maalum vinavyopaswa kuenziwa ili vilete faida hapo baadae katika kuirejeshea hadhi yake Zanzibar ya soka ndani ya ukanda wa Afrika Mashariki.

Waziri wa Habari alitolea mfano Vijana wa Zanzibar Heroes walivyofanikiwa kuipeperusha Bendera ya Zanzibar katika mashindano ya Kombe la Challenge yanayoendelea Nchini Kenya kwa jinsi walivyoonyesha vipaji vyao vilivyopelekea kutinga Nusu fainali ya mashindano hayo inayotarajiwa kufanyika Ijumaa Ijayo.

Alimpongeza Mfanyabiashara huyo kwa moyo wake wa Kizalendo wa kusaidia vifaa kwa jili ya kuendeleza Sekta ya Michezo msaada ambao ni chachu ya kuwapa faraja Vijana wa Taifa hili waliojikubalisha kuendeleza Michezo Nchini.

Othman Khamis Ame
Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar
13/12/2017.

Hakuna maoni :

Chapisha Maoni