.

.

.

.

.

.

.

.
KARIBUNI TUHABARIKE, TUELIMISHANE, TUPEANE HABARI ZA KUKUFANYA UTABASAMU KIDOGO NA MATUKIO YALIYOFANYIWA UCHUNGUZI WA KINA TOKA KILA PEMBE CONTACTS: +255 787 377 722 Email: drweyunga@gmail.com PIA UNAWEZA KUNI FOLLOW KUPITIA INSTAGRAM YANGU @drweyunga | TANGAZA NASI ILI UWAFIKIE WATU WENGI ZAIDI.

Ijumaa, 1 Desemba 2017

BALOZI SEIF AWAKUMBUSHA WAUMINI WA DINI YA KIISLAMU KIJITATHIMINI WANAVYOISHI

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alisema wakati Waumini wa Dini ya Kiislamu wakiadhimisha Uzawa wa Kiongozi wao Mtume Muhammad {SAW} wakumbuke wana wajibu wa kujitathmini kwa kiasi gani wanaishi maisha ya uadilifu na uaminifu kwenye ndoa zao.

Alisema pale ambapo watajigundua wanakwenda kinyume na sifa za uadilifu na uaminifu alizokuwa nazo Kiongozi wao huyo basi wana jukumu la kujirekebisha na tabia hiyo mbaya mara moja.

Balozi Seif alitoa nasaha hizo kwenye maadhimisho ya sherehe za uzawa wa Mtume Muhammad {SAW} yaliyofanyika Kitaifa katika Kijiji cha Rikangala Wilaya ya Ruangwa Mkoani Lindi na kuhudhuriwa pia na Mbunge wa Jimbo la Ruangwa ambae pia ni Waziri Mkuu wa Tanzania Mh. Kasim Majaliwa Kassim.

Alisema sifa ya uaminifu na uadilifu katika ndoa nyingi miongoni mwa Waumini wa Dini ya Kiislamu imetoweka na kupelekea kuibuka kwa michepuko inayosababisha kuvunjika kwa ndoa nyingi na hatimae watoto wanaozaliwa kukosa matunzo mazuri.

Balozi Seif alieleza kwamba Dini ya Kiislamu wakati wote imekuwa ikielekeza namna Waumini wake wanavyopaswa kuoana na kuheshimu ndoa zao ili kundi linalozaliwa liwe kubwa na haipendezi kuona wanakuwepo watoto wa mitaani wasiohusishwa na familia yoyote.

Alifahamisha michepuko ya nje ya ndoa ni mibaya zaidi kwa vile inahatarisha ongezeko la virusi vya ukimwi. Hivyo alitoa rai kwa kila Muumini wa Dini ya Kiislamu kutumia Mwezi aliozaliwa Mtume Muhammad { SAW } kwa kujifanyia tathmini yeye mwenyewe ya mwenendo wa maisha yake kama yanafanana na Kiongozi wake.

Akigusia suala la Rushwa Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar alihimiza kwamba Waislamu wana haki ya kumuunga mkono Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Dr. John Pombe Magufuli katika mapambano yake dhidi ya vitendo vya Rushwa.

Balozi Seif alisema mkakati wa kupinga vitendo vya rushwa lazima Waumini wa Dini ya Kiislamu wanapaswa kuelewa kwamba hiyo ni ibada iliyokuwa ikifanywa na Kiongozi wa Kiislamu Mtume Muhammad {SAW}.

Alieleza kwamba kupungua kwa sifa ya uadilifu na uaminifu katika Jamii ndio iliyompelekea Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Dr. John Pombe Magufuli mara baada ya kuingia madarakani kwa kusaidiana na Waziri Mkuu wake kuanzisha vita endelevu dhidi ya vitendo vya rushwa Nchini kote.

Balozi Seif alifahamisha kwamba Serikali ilikuwa ikitumia Mabilioni ya Fedha kuwalipa wafanyakazi hewa kwa kipindi kirefu kutokana na baadhi ya watendaji wa Serikali kutokuwa waminifu katika majukumu yao na wakasahau kwamba vitendo walivyokuwa wakifanya ni dhambi.

Alisema fedha hizo chafu ziliwanufaisha zaidi watu hao wachache waliotawaliwa na ubinafsi na kuwanyima Watanzania walio wengi huduma za Kijamii zilizokuwa bora ikiwemo Elimu, Afya na masuala mengine ya Ustawi wa Jamii.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar aliwahimiza Waumini wa Dini ya Kiislamu pamoja na Wananchi wote kumuabudu Mwenyezi Muungu pamoja na kufanya kazi iliyo halali.

Alisema Kazi ya halali ni Ibada na Uislamu unakataza waumini wake kupoteza muda kwa mambo yasiyokuwa na maana ambayo kamwe hayawezi kuendeleza mbele Uislamu.

Alfahamisha kwamba bila ya kazi maisha hayatakwenda vyema na hakutakuwa na Maendeleo ambapo mwisho wake watu watajiingiza katika vitendo vya wizi vinavyopelekea Jamii kutumbukia katika dhulma.

Balozi Seif alielezea faraja yake kutokana na kutiwa moyo na Waumini na Wananchi wa Wilaya ya Ruangwa kwa kushirikiana na Mbunge wao kutokana na jitihada zao za kuchapa kazi na matokmeo yake kupatikana mafanikio makubwa.

Alisema mafanikio hayo yameanza kuonekana katika nyanja tofauti za huduma za Jamii ikiwemo sekta Afya, Elimu na Miundombinu pamoja na miradi ya Maji safi na salama ambapo ujenzi wa Vituo vya Afya Vitano vimekamilika na vyengine Tisa viko katika hatua za mwisho kukamilika.

Kuhusu suala la Amani Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar alisema inasikitisha kuona katika Jamii ya Watanzania hivi sasa vitendo vya ukatili vimeongezeka kwa kasi hasa mauaji ya vikongwe, walemavu wa ngozi na hata kudhalilishwa kwa Watoto wadogo.

Balozi Seif aliwakumbusha Wananchi kupitia mikusanyiko mbali mbali kuendelea kuitunza hidaya ya Amani kwa kujifunza mazingatio ya nchi ambazo amani imetoweka na jitihada za kuirejesha imekuwa mtihani kwao.

Alifahamisha kwamba ni vyema Jamii kuwa na hadhari ya Hidaya hiyo vyenginevyo ikiponyoka itakuwa vigumu kuirejesha au urejeshaji wake unaweza kuchukuwa gharama kubwa.

Akiwasilisha salamu za Baraza Kuu la Waislamu Tanzania {BAKWATA } Kaimu Katibu Mkuu wa Baraza hilo Sheikh Salum Ahmed Abeid alitoa wito kwa Taasisi zote zinazosimamia safari za Hija kuanza mapema maandalizi ili kuepuka hitilafu zinazoweza kukimbiwa.

Sheikh Salum alisema zipo kasoro kadhaa zilizokuwa zikiripotiwa katika awamu mbali mbali za usafirishaji wa Mahujaji kwenda kufanya Ibada ya Hijja Makka Nchini Saudia ambazo zinaweza kuondoka iwapo maandalizi hayo yatafanyika mapema iwezekanavyo.

Kaimu Katibu Mkuu huyo wa Bakwata kwa niaba ya Taasisi hiyo ya Kidini Nchini amemshukuru Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Dr. John Pombe Magufuti kwa uamuzi wake wa Kumshawishi Mfalme wa Morocco kukubali kujenga Msikiti Mkubwa Nchini Tanzania.

Alisema Msikiti huo ulioko katika hatua za ujenzi unaotarajiwa kuchukuwa waumini wapatao 6,000 kwa sala Moja umeleta faraja kubwa kwa Waumini wa Dini ya Kiislamu Nchini Tanzania.

Akitoa salamu kwenye maadhimisho hayo ya Baraza la Maulid Mbunge wa Jimbo la Ruangwa ambae pia ni Waziri Mkuu wa Tanzania Mh. Kassim Majaliwa Kassim alikipongeza Kituo cha Matangazo cha Azam Tv kwa uwamuzi wake wa kurusha matangazo hayo moja kwa moja .

Mh. Majaliwa alisema kitendo kinachofanywa na Kituo hicho cha kuwahabarisha Wananchi matukio mbali mbali yanayotokea Mjini na Vijijini jambo ambalo linaleta faraja kwa Wananchi wa rika na hadhi zote.

Akizungumzia Baraza Kuu la Waisalu Tanzania Waziri Mkuu alimshukuru Mufti Mkuu wa Tanzania Sheikh Abubakar Zubeir kwa juhudi zinazochukuwa Uongozi wake wa shughuli za kidini kusogezwa zaidi kwa wahusia wenyewe Mikoani na Wilayani.

Kwa upande wake Mufti Mkuu wa Tanzania Sheikh Abubakar Zubeir alihimiza suala la Wananchi na Waumini kuendelea kuheshimiana ili kinga hiyo kuu ya kuondoa hitilafu na migogoro iendelee kudumu daima.

Sheikh Abubakar alisema Baraza Kuu litaendelea kuwaunganisha Waumini na Wananchi katika muelekeo wa kupenda kuoneana huruma na kusaidiana kama vitabu vya Dini vinavyolingania muda wote.

Othman Khamis Ame
Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar
1/12/2017.

Hakuna maoni :

Chapisha Maoni