Kamati ya Maadili iliyokutana
Januari 18, 2018 imepitia shauri lililowasilishwa na Sekretarieti ya
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania TFF wakiwatuhumu viongozi wanne
kwa makosa ya kughushi na udanganyifu wa mapato kwenye mchezo namba
94 kati ya Ndanda FC na Simba uliochezwa Desemba 30,2017.
Shauri la kwanza lililomuhusu Katibu
msaidizi wa Ndanda Ndugu Selemani Kachele, Kamati imegundua kuwa
mtuhumiwa aliitwa wakati wa kuhesabu mapato kuthibitisha deni dhidi
ya Ndanda lenye thamani ya Shilingi Milioni mbili laki mbili na elfu
hamsini (2,250,000), deni ambalo TFF waliagiza wakatwe kwenye mapato
ya mechi hiyo, Katibu wa Chama cha Mpira wa Miguu mkoa wa Mtwara
alithibitisha kuwa alimuita kuthibitisha uhalali wa deni hilo baada
ya Muhasibu wa Ndanda kugoma kulipa deni hilo ambalo linahusu pango
la Ndanda kwa Mama mwenye Nyumba.
Hata hivyo Kamati ilimuhoji zaidi na
akashindwa kutoa uthibitisho wa kulipwa kwa deni hilo na hakuna
kumbukumbu zozote zinazoonyesha kuwa deni hilo limelipwa.
Kamati imempa onyo kwa mujibu wa
kifungu cha 6(1)(a) kanuni za maadili ya TFF toleo la 2013 na
imeiomba Sekretarieti ya TFF ifuatilie kama deni hilo limeshalipwa
ili kuepusha ulipaji wa zaidi ya mara moja.
Shauri la Pili lilimuhusu Muhasibu
msaidizi wa Simba Ndugu Suleiman Kahumbu.
Kamati haikuendelea na tuhuma dhidi
yake baada ya Sekretarieti ya TFF kuamua kuondoa shauri dhidi yake
kwa kuwa alitoa ushirikiano na kutosheka kuwa hana hatia na badala
yake alitumika kama shahidi wa upande wa washtaki.
Shauri la tatu lilimuhusu Katibu
mkuu wa Chama cha soka Mtwara Ndugu Kizito Mbano.
Kamati ilimuhoji mtuhumiwa na
alikiri kuwepo kwa mawasiliano na msimamizi wa kituo Ndugu Dunstan
Mkundi kuhusu nia ya kughushi fomu ya marejesho ya mapato ya mchezo
kati ya Ndanda FC na Simba SC.
Ndugu Kizito Mbano hakutoa taarifa
yoyote ile wala kuonyesha ushirikiano kwa Sekretarieti ya TFF na Bodi
ya Ligi wakati yeye akiwa msimamizi msaidizi wa kituo na Katibu Mkuu
wa Chama cha Soka cha Mkoa wa Mtwara,hivyo Kamati imemkuta na hatia
na imemuhukumu kutojihusisha na shughuli za Mpira wa Miguu kwa
kipindi cha miaka Mitano(5) kwa mujibu wa kifungu cha 73(7) cha
kanuni za maadili TFF toleo la 2013.
Shauri la nne lililosikilizwa
lilikuwa la Msimamizi wa Kituo cha Mtwara Ndugu Dunstan Mkundi.
Kamati baada ya kusikiliza shauri
hilo imemkuta na hatia kwa kosa la kushindwa kuwasilisha fomu ya
mapato ya mchezo kati ya Ndanda FC na Simba ndani ya saa 48 kama
kanuni inavyotaka.
Hiyo ni kinyume na Kanuni ya 32(2)
Kanuni za Ligi Kuu toleo la 2015,Vilevile Kamati imemkuta na hatia ya
kushindwa kusimamia mauzo ya tiketi za mchezo kati ya Ndanda FC na
Simba kwa kutotoa taarifa ya tiketi zilizotumika na zile zilizobaki.
Kamati ilibaini kuwa Ndugu Dunstan
Mkundi akiwa msimamizi wa kituo hakutoa ushirikiano kwa kutompa
taarifa za mapato na idadi ya watazamaji Kamisaa wa mchezo Salum
Singano kinyume na Kanuni ya 32(4) ya Ligi Kuu toleo la 2017.
Aidha Mkundi ambaye ni msimamizi wa
kituo cha Mtwara ameshindwa kutoa maelezo ya kutosha kuhusu utata wa
fomu mbili zilizowasilishwa zilizoonyesha utofauti wa mapato kwa
kiasi cha shilingi Milioni tatu laki saba kumi elfu(3,710,000).
Washtakiwa wote walihojiwa na Kamati
na kuthibitisha kuwa mapato ya mchezo kati ya Ndanda FC na Simba
yalikuwa ni Shilingi Milioni thelathini na saba laki saba na
themanini elfu(37,780,000) na siyo Shilingi milioni thelathini nne
sabini elfu(34,070,000) ambazo Ndugu Mkundi anadai kuwa ndiyo
yalikuwa mapato ya mchezo huo.
Kulingana na nyaraka
zilizowasilishwa kutoka klabu za Ndanda FC na Simba mapato ya Vilabu
hivyo yalitokana na asilimia ya vyanzo kutokana na milioni thelathini
na saba laki saba themanini elfu(37,780,000) na siyo Shilingi milioni
thelathini nne sabini elfu(34,070,000)kama alivyowasilisha msimamizi
huyo wa kituo cha Mtwara nyaraka za fedha alizoweka kwenye akaunti za
TFF na Bodi ya Ligi.
Kitendo cha kughushi nyaraka na
kupunguza mapato ya mchezo kati ya Ndanda FC na Simba siyo tu
kimeharibu taswira ya mchezo wa Mpira wa miguu,bali pia kimepunguza
mapato ya TFF,Bodi ya Ligi na taasisi nyingine kama Mamlaka ya Mapato
(TRA),Baraza la Michezo la Taifa (BMT),Wamiliki wa Uwanja na Wadau
wengine.
Kamati imemtia hatiani Ndugu Dunstan
Mkundi kwa makosa hayo na inamfungia maisha kutojishughulisha na
mchezo wa Mpira wa Miguu.
Kamati imetoa adhabu hiyo kali ili
iwe fundisho kwa wale wote wanaotaka kufanya ubadhirifu wa ufisadi
katika mchezo wa Mpira wa Miguu.
Kamati inashauri Sekretarieti ya TFF
ifuatilie suala hili kwenye vyombo vya dola na mamlaka husika kwa
hatua zaidi za kisheria.
Pia Kamati imeiomba Sekretarieti ya
TFF na Bodi ya Ligi kutafuta njia bora ya kuimarisha udhibiti wa
mapato kwa kuongeza uwajibikaji wa uwazi kwa wadau wote,Vilevile
Kamati inashauri Sekretarieti ya TFF na Bodi ya Ligi kuharakisha
mchakato wa kukusanya mapato yake kwa njia za kielektroniki ili
kuziba mianya ya upotevu.
IMETOLEWA NA SHIRIKISHO LA MPIRA WA
MIGUU TANZANIA TFF
Hakuna maoni :
Chapisha Maoni