.

.

.

.

.

.

.

.
KARIBUNI TUHABARIKE, TUELIMISHANE, TUPEANE HABARI ZA KUKUFANYA UTABASAMU KIDOGO NA MATUKIO YALIYOFANYIWA UCHUNGUZI WA KINA TOKA KILA PEMBE CONTACTS: +255 787 377 722 Email: drweyunga@gmail.com PIA UNAWEZA KUNI FOLLOW KUPITIA INSTAGRAM YANGU @drweyunga | TANGAZA NASI ILI UWAFIKIE WATU WENGI ZAIDI.

Jumamosi, 10 Februari 2018

BALOZI SEIF AFUNGUA MAONYESHO YA SHERIA MJINI ZANZIBAR

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif akikata utepe kuashiria kuyafungua rasmi Maonyesho ya Siku ya Sheria Zanzibar hapo katika Viwanja vya Maisara Suleiman Mjini Zanzibar. Kushoto ya Balozi Seif ni Jaji Mkuu wa Zanzibar Mh. Omar Othman Makungu, Kulia ya Balozi Seif ni Naibu Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Katiba, Sheria, Utawala Bora, na Utumishi wa Umma Mh. Khamis Juma Maalim na Nyuma ya Jaji Mkuu ni Mkuu wa Mkoa Mjini Magharibi Mh. Ayoub Mohamed Mahmoud.
Balozi Seif akiangalia baadhi ya Vitabu, Machapisho na Makaprasha yaliyopo kwenye Banda ya Mahkama ya Watoto hapo Maisara Suleiman .
Mh. Balozi Seif akifahamishwa baadhi ya Vitabu katika Banda la Mahkama ya Ardhi Zanzibar.
Mmoja wa Wanasheria wa Serikali Bwana Ramadhan Ali Nassib akimpatia Maelezo Balozi Seif kwenye Banda la Maonyesho ya Ofisi ya Mkurugenzi Mashtaka Zanzibar.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi akiridhika na kufurahia baadhi ya bidhaa zinazozalishwa na Kikosi cha Mafunzo Zanzibar kwenye Maonyesho ya Siku ya Sheria Zanzibar hapo Maisara Suleiman.

Picha na – OMPR – ZNZ.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi ametoa wito kwa Wananchi kuitumia fursa iliyotolewa na Mawakili waliojitolea kutoa huduma za Kisheria kwenye maonyesho ya Siku ya Sheria Maisara kuwasilisha kero zinazowakiabili ili kupata ushauri wa bure wa Kisheria.

Alisema hiyo ni fursa muhimu na adimu kupatikana ambayo hata Wananchi kama hawana matatizo ya kisheria wanapaswa kuichangamkia kwa lengo la kupata mwanga utakaowawezesha kujua Historia ya Taasisi za kisheria na kuepukana na tabia ya kulalamika mitaani.

Balozi Seif Ali Iddi alitoa kauli hiyo wakati akiyafungua Maonyesho ya Siku Tatu ya Siku ya Sheria yanayofanyika katika Viwanja vya Michezo vya Maisara Suleiman Mjini Zanzibar na kushirikisha wadau tofauti wa masuala ya Kisheria wakiwemo pia Wafanyabiashara na Wajasiri amali mbali mbali.

Alisema Mawakili wa Kujitegema wameamua kutoa ushauri wa Kisheria Bure kwenye maonyesho hayo ikiwezekana kwa wale ambao wanamekumbwa na matatizo ya Kesi Mahakamani na hawana uwezo wa kifedha wa kuajiri Mawakili wa Kujitegemea.

Balozi Seif alisema wapo Wananchi wengi wenye malalamiko ya kudhulumiwa fedha, ardhi, mirathi, malezi ya watoto, mgawanyo wa mali iliyopatikana wakati wa ndoa lakini wanashindwa kufungua kesi kwa kutokufahamu taratibu za kisheria.

Alisema baadhi ya wananchi wanaofungua kesi au kufunguliwa kesi hushindwa kwenye kesi husika na badala ya kukata rufaa Mahakama ya juu kwa mujibu wa taratibu za kisheria huamua kwenda kulalamika kwa viongozi wa ngazi mbali mbali wawasaidie.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar alitahadharia kwamba mpaka Mwananchi au mlalamikaji akifahamishwa taratibu za kufuata kwa mujibu wa sheria muda wa rufaa yake unakuwa umeshamalizika na hatimae anapoteza haki yake.

Alisema maonyesho hayo ya Siku ya Sheria yamelenga kutoa Elimu klwa Wananchi jambo ambalo Serikali imekuwa ikisisitiza sana, hasa ikijua kwamba Wananchi wengi hawana ufahamu wa mambo ya Sheria.

“ Siku hii ya leo ni muhimu sana kwa Jamii yetu kuweza kujifunza na hatimae katika miaka ya baadae matatizo na lawama kama zinazotokezea zisiweze kujichomoza ndani ya Jamii yetu”. Alisema Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar.

Balozi Seif alielezea faraja ya Serikali kuona Mwaka huu wafanyabiashara na Wajasiri amali mbali mbali wameshirikishwa katika hayo ya Siku ya Sheria kwa mara ya kwanza, taswira inayojionyesha wazi kwamba Jamii iko tayari kushiriki kikamilifu kama inashirikishwa mapema.

Aliwapongeza Majaji, Wanasheria na Mawakili kwa kuandaa Maonyesho hayo ya Siku ya Sheria ambapo kwa upandew wake Serikali itahakikisha inatoa msaada unaohitajika ili kuwezesha maonyesho kama hayo yanafanyika mika mwaka na kwa ubora unaostahiki.

Hata hivyo Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar aliwashauri wadau hao wa Masuala ya Sheria Nchini kufikiria zaidi namna ya kuwafikishia huduma kama hizo Wananchi wa Vijijini kwani nao wana mahitaji mengi ya Kisheria wanayolazimika kuyapata.

Akizungumzia kesi zinazofunguliwa na watu mbali mbali katika nia ya kupata haki zao Mahakamani na katika vyombo vya Sheria Balozi Seif aliwatanabahisha Majaji na Mahakimu kuhakikisha kwamba haki ya kila Mwananchi au Raia inapatikana katika misingi ya Kisheria.

Alisema zipo baadhi ya kesi zinazofunguliwa zikiwa na ushahidi kamili wa watu wanaodai haki zao ikiwemo masuala ya nyumba, Ardhi na hata mirathi lakini kinachofikia hatima yake ni wale wasio na haki ndio wanaomilikishwa mali au haki hizo jambo ambalo linatoa taswira mbaya kwa Majaji na Mahakimu wanaosimamia kesi hizo.

Mapema Jaji Mkuu wa Zanzibar Mheshimwa Omar Othman Makungu alisema Maonyesho ya Mwaka huu ambayo ni ya pili tokea kuasisiwa kwake yamepanua wigo zaidi wa kwa kuwashirikisha Wafanyabiashara pamoja na Wajasiriamali tofauti Nchini.

Jaji Mkuu Omar alisema hatua hiyo imekuja kwa kuzingatia umuhimu wa ushirikishwaji Jamii katika masuala yanayowahusu sambamba na kuheshimu Ujumbe wa Mwaka Huu wa Siku ya Sheria unaoelezea Tudumishe Utawala Bora Kisheria ili kukuza Uchumi na Pato la Taifa.

Alisema Wiki ya Sheria iliyoamb`tanisha mambo mbali mbali ya Kisheria yamelenga pia kutoa Elimu ya kisheria kwa Wananchi ili welewe haki zao za msingi zilizowazunguuka kila siku.

Maonyesho hayo ya Siku ya Kisheria yatakayochukuwa muda wa Siku Tatu yatakayotoa fursa kwa Wananchi mbali ya kuelimika kupitia masuala yanayohusu Sheria lakini pia watapata nafasi ya kujinunulia bidhaa mbali mbali na adimu zilizotayarishwa na Wafanyabiashara pamoja na Wajasiri amali Nchini.

Othman Khamis Ame
Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar

Hakuna maoni :

Chapisha Maoni