Kikao cha Kamati ya Nidhamu ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania TFF ilikutana Jumamosi Februari 10, 2018 kupitia mashauri yaliyofikishwa kwenye kamati hiyo.
Shauri namba moja lilihusisha malalamiko dhidi ya wachezaji Saba(7) wa timu ya Transit Camp,shauri ambalo lilihudhuriwa na mchezaji mmoja Mohamed Suleiman Ussi.
Mchezaji Mohamed Suleiman Ussi alituhumiwa kwa kosa la utovu wa nidhamu kwenye mechi namba 48 ya Kundi C Ligi Daraja la Kwanza Tanzania Bara akidaiwa kutaka kumpiga Mwamuzi wa mchezo kinyume na Ibara ya 50(1)(2) na (5)ya Katiba ya TFF toleo la 2015.
Kamati ilipitia ripoti ya kamishna wa mechi ambayo pamoja na kuwataja wachezaji wengine wengine pia ilimtaja Mohamned Suleiman Ussi kuhusika kwenye tukio hilo akiwa amevaa jezi namba 14 ambaye pia alitajwa kwenye ripoti ya mwamuzi ikielezea kitendo cha Mohamed Suleiman Ussi kutaka kumpiga mwamuzi msaidizi namba 2.
Baada ya kupitia ripoti Kamati imejiridhisha kuwa mchezaji Mohamed Suleiman Ussi alitaka kumpiga mwamuzi kinyume na kanuni ya 36 ya Ligi Daraja la Kwanza na ibara ya 50(1)(2) na (5) ya Katiba ya TFF toleo la 2015.
Kamati imemuadhibu Mohamed Suleiman Ussi imemfungia kutocheza michezo mitatu(3) pamoja na faini ya Shilingi laki tatu(300,000) kwa mujibu wa kanuni ya 37(7) na 37(12) kanuni za Ligi Daraja la Kwanza.
KAMATI YA NIDHAMU YAMFUNGIA JUMA NYOSO
Kamati ya Nidhamu iliyokutana Jumamosi Februari 10, 2018 pamoja na mambo mengine pia ilipitia shauri la mchezaji wa Kagera Sugar Juma Nyoso lililofikishwa kwenye kamati akituhumiwa kwa utovu wa nidhamu kwenye mechi namba 112 ya Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara Kagera Sugar dhidi ya Simba Sports Club iliyochezwa kwenye Uwanja wa Kaitaba.
Juma Nyoso alituhumiwa kumpiga shabiki baada ya kumalizika mchezo huo kinyume cha kanuni ya 36 ya ligi Kuu inayozungumzia uchezaji wa kiungwana pamoja na Ibara 50(1)(2) na (5) ya katiba ya TFF toleo la 2015.
Kamati ilipitia ripoti ya kamishna wa mechi ambayo imeeleza tukio hilo la Juma Nyoso kupishana na shabiki aliyekuwa amebeba vuvuzela na ndipo Nyoso aliposimama na kuanza kumpiga na kiatu na kutumia goti mpaka askari wa jeshi la Polisi walipoingilia kumuokoa na kumshikilia mchezaji huyo wakati shabiki akipatiwa huduma kwenye gari la huduma ya kwanza.
Juma Nyoso katika utetezi wake alikana malalamiko dhidi yake akidai kitendo alichofanya ni kukunjana na shabiki.
Kamati kupitia ripoti ya kamishna wa mchezo huo imemtia hatiani Juma Nyoso kupitia kanuni ya 36 ya kanuni ya Ligi kuu na Ibara ya 50(1)(2) na (5) ya katiba ya TFF.
Kamati pia ilipokea taarifa za nyuma za nidhamu za Juma Nyoso ambayo rekodi inaonesha aliwahi kufungiwa kwa makosa ya kinidhamu .
Kupitia kifungu cha 37(10)cha kanuni za ligi Kuu kamati imemtia hatiani Juma Nyoso na imemfungia kutocheza mechi Tano(5) na faini ya Shilingi milioni moja(1,000,000).
MAAMUZI KAMATI YA SAA 72
LIGI KUU YA VODACOM
Mechi namba 122 (Lipuli 0 vs Yanga 2). Klabu za Lipuli na Yanga kila moja imepigwa faini ya sh. 500,000 (laki tano) kwa kutumia milango isiyo rasmi kuingia uwanjani, kitendo ambacho ni ukiukaji wa Kanuni ya 14(14) ya Ligi Kuu. Adhabu dhidi yao imetolewa kwa kuzingatia Kanuni ya 14(49) ya Ligi Kuu kuhusu Taratibu za Mchezo.
Pia klabu ya Yanga imepigwa faini ya sh. 500,000 (laki tano) kwa kutoingia vyumbani, hivyo kwenda kinyume na Kanuni ya 14(13) ya Ligi Kuu kuhusu Taratibu za Mchezo. Adhabu hiyo ni uzingativu wa Kanuni ya 14(49) ya Ligi Kuu kuhusu Taratibu za Mchezo.
Mechi namba 123 (Singida United 3 vs Mwadui 2). Kocha wa makipa wa Mwadui, Lucheke Gaga amefungiwa mechi tatu na kupigwa faini ya sh. 500,000 (laki tano) baada ya kuondolewa kwenye benchi (ordered off) na Mwamuzi kwa kutoa lugha ya matusi katika mechi hiyo iliyofanyika Februari 3, 2018 kwenye Uwanja wa Namfua mjini Singida. Adhabu hiyo imetolewa kwa kuzingatia Kanuni ya 40(11) ya Ligi Kuu kuhusu Udhibiti wa Makocha.
Mechi namba 128 (Ruvu Shooting 0 vs Simba 4). Mchezaji wa Ruvu Shooting, Mau Bofu amefungiwa mechi tatu na kupigwa faini ya sh. 500,000 (laki tano) kwa kumpiga kiwiko Emmanuel Okwi wa Simba katika mechi hiyo iliyofanyika Februari 4, 2018 kwenye Uwanja wa Uhuru jijini Dar es Salaam. Adhabu hiyo imezingatia Kanuni ya 37(3) ya Ligi Kuu kuhusu Udhibiti wa Wachezaji.
LIGI DARAJA LA KWANZA
Mechi namba 53 Kundi A (Kiluvya United 0 vs African Lyon 1). Klabu ya African Lyon imepigwa faini ya sh. 200,000 (laki mbili) kutokana na timu yake kutoingia vyumbani katika mechi hiyo iliyofanyika Februari 5, 2018 kwenye Uwanja wa Filbert Bayi mkoani Pwani.
Kitendo hicho ni ukiukaji wa Kanuni ya 14(13) ya Ligi Daraja la Kwanza kuhusu Taratibu za Mchezo. Adhabu hiyo imetolewa kwa kuzingatia Kanuni ya 14(49) ya Ligi Daraja la Kwanza kuhusu Taratibu za Mchezo.
Mechi namba 53 Kundi B (Mawenzi Market 0 v Coastal Union 2). Klabu ya Mawenzi Market imepigwa faini ya sh. 500,000 (laki tano) kutokana na washabiki wake kuwarushia chupa Waheshimiwa Mawaziri ambao ni washabiki wa Coastal Union katika mechi hiyo iliyofanyika Februari 2, 2018 kwenye Uwanja wa Jamhuri mjini Morogoro.
Adhabu dhidi ya klabu ya Mawenzi Market imetolewa kwa kuzingatia Kanuni ya 42(1) ya Ligi Daraja la Kwanza kuhusu Udhibiti wa Klabu.
Mechi namba 53 Kundi C (Alliance Schools 2 vs JKT Oljoro 1). Wachezaji Ramadhani Yego na Joseph Mkota wa JKT Oljoro wanapelekwa Kamati ya Nidhamu ya TFF kwa kutaka kumpiga Mwamuzi baada ya kumalizika mechi hiyo iliyochezwa Februari 4, 2018 kwenye Uwanja wa Nyamagana jijini Mwanza.
LIGI DARAJA LA PILI
Mechi namba 28 Kundi B (Kilimanjaro Heroes 0 v Pepsi 2). Klabu ya Kilimanjaro Heroes imepigwa faini ya sh. 200,000 (laki mbili) kwa kuhudhuria kikao cha maandalizi ya mechi (pre match meeting) katika mechi hiyo iliyofanyika Februari 3, 2018 katika Uwanja wa Ushirika mjini Moshi, kinyume na Kanuni ya 14(2b) ya Ligi Daraja la Pili kuhusu Taratibu za Mchezo.
Adhabu dhidi ya Kilimanjaro Heroes imetolewa kwa kuzingatia Kanuni ya 14(3) ya Ligi Daraja la Pili kuhusu Taratibu za Mchezo.
Mechi namba 30 Kundi B (African Sports 2 v AFC 0). Wachezaji wa AFC, John George Rasta na Shaibu Salim wanapelekwa Kamati ya Nidhamu ya TFF kwa kutaka kumshambulia Mwamuzi kabla ya kuokolewa na viongozi wa timu hiyo katika mechi hiyo iliyofanyika Februari 3, 2018 katika Uwanja wa Mkwakwani jijini Tanga.
Klabu ya AFC imepigwa faini ya sh. 200,000 (laki mbili) kwa kutoingia vyumbani wakati wa mapumziko, kitendo ambacho ni kinyume na Kanuni ya 14(13) ya Ligi Daraja la Pili kuhusu Taratibu za Mchezo. Adhabu hiyo imetolewa kwa kuzingatia Kanuni ya 14(49) ya Ligi Kuu kuhusu Taratibu za Mchezo.
MALALAMIKO YA NJOMBE MJI
Klabu ya Njombe Mji iliwasilisha malalamiko kuwa Tanzania Prisons ilimchezesha mchezaji James Mwasote katika mechi yao namba 126 ya Ligi Kuu ya Vodacom iliyofanyika Februari 3, 2018 wakati akiwa na kadi tatu za njano.
Kamati imekataa malalamiko ya Njombe Mji FC kwa vile wakati James Mwasote anacheza mechi hiyo iliyofanyika Uwanja wa Kumbukumbu ya Sokoine jijini Mbeya alikuwa na kadi mbili za njano. Mwasote alipata kadi hizo kwenye mechi dhidi ya Majimaji na dhidi ya Singida United.
IMETOLEWA NA SHIRIKISHO LA MPIRA WA MIGUU TANZANIA TFF
Hakuna maoni :
Chapisha Maoni